CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimewageuza wakulima kuwa manamba ndani ya mashamba yao wenyewe, kutokana na mazao yao kufaidisha vigogo wa CCM na Serikali yake, badala ya kunufaisha wakulima wenyewe.
Hayo yamesemwa jana na Mchungaji Peter Msigwa, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wa Kanda ya Nyasa, inayojumuisha mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Songwe, katika uzinduzi wa Oparesheni +255 katika Kanda hiyo, iliyoanza leo mjini leo tarehe 22 Oktoba 2023, mjini Tunduma.
Alisema mikoa hiyo ndiyo inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula na mazao mengi ya biashara, lakini bado wananchi wameendelea kuwa maskini kwasababu ya sera mbaya na uongozi mbaya wa CCM katika kilimo.
Alifafanua kuwa wakati CCM inasema kilimo ni uti wa mgongo, Serikali ya Chama hicho, imeshindwa kabisa hata kuajiri na kusambaza maafisa ugani wa kutosha, huku akibainisha kuwa maafisa ugani waliopo ni asilimia saba tu ya hitaji halisi la nchi.
“Wakulima wetu mnalima kwa gharama kubwa, lakini mnauza kwa bei ya hasara. Mnakopeshwa mbolea kwa bei ya juu, lakini mnapangiwa kuuza mazao yenu kwa bei ya chini. Kwasababu ya CCM, wakulima wetu, mmegeuzwa Manamba, ndani ya mashamba yenu wenyewe! Mashamba ni yenu, mazao ni yenu, lakini wanaofaidika ni vigogo wa CCM na Serikali yake, wanaoendesha vyama vya msingi (AMCOs) na wakala wa ghala la Taifa (NFRA”, alisema Msigwa.
Msigwa aliwaomba wananchi wa Tunduma kuzidi kujiunga na Chadema ili kujenga chama imara kitakacho ing’oa CCM madarakani na kuunda Serikali inayojali wananchi wakiwemo wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara.
Kwa upande wao, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar na Katibu wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), Catherine Ruge, walihamasisha wananchi wa Tunduma kuhakikisha wanasajiliwa rasmi kuwa wanachama wa Chadema ili kujenga chama imara kitakachoing’oa CCM madarakani, kwa kuanzia na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na baadaye, uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025.
Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini, aliwataka wananchi wa Tunduma wajenge ujasiri wa kupigania haki na maendeleo yao kupitia Chadema bila kutishwa na vitendo visivyo vya kidemokrasia vinavyoanza kufanywa na baadhi ya viongozi wa CCM.
Mjumbe wa Kamati Kuu, Grace Kihwelu, akisalimia wananchi katika mkutano huo, alisema matatizo ya maji, umeme, barabara na afya, yaliyopo Tunduma, hayawezi kamwe kutatuliwa na wasanii walioletwa na Mkuu wa wilaya hiyo ili kuvuruga mkutano wa Chadema, bali yatakwisha kwa wananchi kujiunga na Chadema na kuiong’oa CCM madarakani.
Kwa upande wake, Patric Ole Sosopi, alisema CCM imeshindwa kuongoza nchi ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan anabadili wakuu wa wilaya karibu kila siku, lakini matatizo ya wananchi bado yapo pale pale na kwamba njia pekee ya wananchi kujikomboa ni kuhakikisha CCM yote inang’olewa madarakani.
Aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), alisema Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia hata vitu vidogo vidogo kama kudhibiti foleni ya malori ya mizigo iliyopo Tunduma.
Aidha, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema na mgombea ubunge wa chama hicho, Frank Mwakajoka, alisema mpaka wa Tunduma unaingiza zaidi ya shilingi bilioni 230 na kwamba DC anayefanya mambo ya kitoto hatoweza kuendana na watu wa Tunduma.
“Atashindwa mwenyewe na kuacha kazi. Tunduma inahitaji kuongozwa na watu wenye akili timamu”, alisema Mwakajoka na kushangiliwa.