IFUATAYO ni hotuba ya Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyotoa kwa taifa tarehe 11 Aprili 2021 akijadili athari za utawala wa Hayati John Magufuli kwa miaka mitano iliyopita, na mustakabali wa taifa katika utawala mpya wa Rais Samia Suluhu Hassan. Kwa sababu ya uzito wake, na kwa ajili ya kuweka kumbukumbu, tumeichapisha yote kama ilivyo. Endelea…
“Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, kwa zawadi ya Uhai wetu. Wako wengi waliokuwa hai miongoni mwetu, mara ya mwisho nilipozungumza na Taifa, mwezi Januari mwaka huu, ambao leo hatunao tena.
“Ni katika kipindi hiki, Taifa letu lilikumbwa na taharuki kubwa. Tulimpoteza Rais wa nchi yetu, Hayati, Dr. John Pombe Joseph Magufuli.
“Nasikitika, binafsi nilishindwa kurejea nchini kwa wakati, kushirikiana na Watanzania wenzangu na Viongozi wa nchi na Jumuia mbalimbali za Kimataifa katika kumsindikiza katika Safari yake ya mwisho.
“Chama chetu kilishiriki kwa hatua zote chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu wetu, Mhe. John John Mnyika. Kwa mara nyingine tena, natoa pole nyingi kwa Mama Mjane, Janet Magufuli, Watoto, Familia, Ndugu na Jamaa yote; Rais na Mama yetu, Samia Suluhu Hassan.
“Hakika ni mwisho wa zama! Bwana Ametoa na Bwana ametwaa, Jina lake lihimidiwe!
“Kila jambo hutokea kwa sababu anazozijua Mwenyezi Mungu. Imani hii, ni kwa wale wenye kuukiri uwepo na ukuu wake. Binafsi na japo kwa maumivu makubwa sana, sasa naamini ilikuwa ni lazima kupitia tuliyopitia ili kujifunza.
“Miaka mitano ya Utawala wa Hayati Magufuli inatupa somo kubwa na la kipekee sisi Watanzania na hata Jamii ya Kimataifa.
“Ni wajibu wetu sote kama Taifa, kwanza kutafakari tumejifunza nini, chanya na hasi; pili, tufikirie kwa utulivu ni yapi ya kuenzi na yapi ya kulaani, tena bila unafiki au upofu wa itikadi zetu za kisiasa, kidini, kikabila au Kikanda.
“Tatu, tujiulize tufanye nini ili kuirejesha nchi yetu kwenye misingi yake ya Utu, Undugu na utengemano, kisha tusonge mbele kwa upya, kwa Pamoja, na kwa umoja wetu.
“Hatimaye tukubaliane, tufanye nini ili Nchi yetu KAMWE, NA KAMWE TENA isirudi kwenye uharibifu, mateso na hofu tuliyopitia kwa miaka mitano Iliyopita.
“Ili kuipata kesho yetu iliyo salama na bora zaidi, hatuna budi sasa kutafakari kwa uwazi, tulipotoka, tulipo na tunakokusudia au kupaswa kwenda. Adui mkubwa wa ustawi wa binadamu ni kuufumbia ukweli macho.
“Pamoja na kuwa kukosea au kutokosea ni mtazamo wa mtu binafsi, ni ukweli pekee ndiyo usiohitaji mtazamo wa mtu, kwani haubadiliki na ndiyo utakaotupa majibu ya wapi tulipokosea na namna bora na salama ya kwenda mbele.
“Nikiri, baada ya taarifa za mimi kukusudia kuhutubia Taifa leo, nimeshtushwa na wingi wa ujumbe na ushauri wa watu mbalimbali, ninaowajua na nisiowajua. Wa vyama mbalimbali na hata waliopo Serikalini.
“Wote wametoa dukuduku zao za
nini nizungumze. Nilichojifunza hapa, ni kuwa Taifa lina mtanziko mkubwa. Nimewasikia na kuwasoma wote.
“Nakusudia kufikirisha umma
hasara za kutisha tulizozipata kwa kipindi kifupi cha miaka mitano “tuliyokubali” kucheza na Katiba yetu na kuruhusu kikundi kidogo kucheza na demokrasia. Hakika wote hatuko salama.
“Hotuba yangu leo inakusudia kulifikirisha Taifa, kujaribu kuleta mawazo ya makundi yote kufikiria pamoja kwa faida ya wote.
“Ni kipindi ambacho kimkakati, tulilishwa propaganda za kutukuza mtu na tukazibomoa taasisi zetu na kuzigeuza kuwa wakala wa kumpamba Rais.Bila aibu, baadhi ya viongozi waandamizi wakafika hatua ya kumlinganisha Rais Magufuli na Mungu!! Laana hii, isingeweza kuliacha Taifa salama!
“Niseme mapema kabisa! Hotuba yangu leo ina lengo kuu moja. Kujenga uelewa wa Taifa kwamba, pamoja na tofauti zetu zote; hatupaswi kuruhusu kwa njia yeyote ile “Umagufuli” kurejea tena. Yaani, NEVER AND NEVER AGAIN!
“Sikusudii, kuandika au kuhutubia Tanzia. Nafanya tathmini ya Kiongozi ambaye maamuzi yake, misimamo yake, busara zake au la; zilitikisa kwa maumivu makubwa mamilioni ya Watanzania, na wengi wao wasipate ujasiri wa kusema au hata kulia.
“Hakuna utawala wowote duniani wenye uwezo wa kufurahisha kila mtu. Wapo waliocheka na kufurahi na utawala huu. Wengi wao kwa mantiki ya “kutumikia kafiri upate mradi wako. Leo tunawasikia kugeuka misimamo yao.
“Watanzania wengi wanashangaa. Mimi sishangai. Wengi niliwajua, tena wakitoka makundi 3 yote; ya wapinzani na ya chama tawala. Hawa ni kansa mbaya na hatari katika kuitafuta kesho yetu iliyo bora.
“Hayati Magufuli atakumbukwa kwa mengi. Mabaya na mazuri. Katika mukhtadha wa Utawala na Uongozi wa nchi, nayajua mambo mawili tu ambayo nadiriki kusema pasipo shaka ni mambo mawili mazuri tunayoweza kumkumbuka kwayo.
“Namuunganisha nayo kwani aliyaishi mambo haya kwa ukamilifu wake, kwa kuyahubiri na kuyatenda bila kujali.”
“(i) Uthubutu wa kufanya maamuzi magumu
(ii) Kuamini na kusisitiza katika kuchapa kazi kwa bidii.
“Hapa sijadili maisha yake binafsi. Namjadili aliyekuwa Rais wa Nchi, aliyekuwa na dhamana kubwa ya Uhuru, haki na maendeleo ya watu na siyo Chifu wa Kabila au mwenyekiti wa Ukoo.
“Najua maneno yangu leo hayatafurahisha wengi. Nasema bila woga kama nilivyosema akiwa hai na kulipa kwa gharama kubwa msimamo wangu huu. Nitakayoongea yote ni kweli na kweli tupu na ushahidi wake tunao.
“Tuko tayari kusimama popote kutetea ukweli huu. Watanzania wanahitaji kuujua ukweli ili uwaweke huru. Wamedanganywa sana kwa muda mrefu na wote tuseme bila woga: Never and Never Again!
“Kipimo cha kiwango cha uharibifu uliofanywa na Magufuli, serikali yake na Chama cha Mapinduzi; ni namna wote kwa pamoja katika ushirika haramu walivyotumia nguvu kubwa kuficha ukweli.
“Hii ni pamoja na kuthibiti sauti yeyote ya kuhoji kwa aidha kutumia vyombo vya dola, bunge, mahakama au idara na taasisi mbalimbali za umma.
“Huyu ni Rais aliyeongoza kwa muda mfupi kuliko wote waliomtangulia, lakini aliyeacha maumivu mengi makubwa kwa wengi na aliharibu mifumo mingi ya Utawala! Hakika, never and never again!
“Nitachambua kwa kifupi kilichojidhihiri katika Mihimili Mikuu mitatu iliyo msingi wa Taifa lolote, kisha baadaye nitajadili sekta chache na taasisi nyeti za umma na namna zilivyotumika kulijeruhi taifa.
“Utawala au Serikali ni mhimili mkuu wenye wajibu wa kuwezesha kirasilimali mihimili mingine. Mihimili yote yapaswa kujitegemea katika utendaji wake. Yote huongozwa na Katiba, Sheria na kanuni. Mhimili huu ukiyumba ni hatari ya haraka na ya moja kwa moja kwa Taifa.
“Hayati Magufuli aliongoza muhimili huu kama mali yake binafsi. Alilea upendeleo wa kifamilia (nepotism) na hakuheshimu kabisa sheria na kanuni za Utumishi wa Umma. Alifukuza kwa kutweza. Hakujali wala kuheshimu haki za watumishi na wafanyakazi.
“Bila kuheshimu Katiba, aligeuza Serikali tawi la CCM. Hakuamini katika watumishi wa Serikali kutofungamana na chama chochote cha siasa, bali yeye aliamini watumishi wote wa umma lazima wawajibike moja kwa moja kwa CCM.
“Aliparua Wahadhiri kutoka vyuo vikuu na kuviacha na uhaba mkubwa wa Waalimu. Aliwaingiza kwenye mambo ya kiutendaji wasio na uzoefu wowote wa kiutawala. Hakuheshimu ‘meritocracy’ bali alikumbatia ‘mediocracy.’
“Alijaza makada wa CCM moja kwa moja kwenye nafasi za kiutendaji za Serikali Kuu. Hali kadhalika, Serikali za Mitaa ikiwemo Wakurugenzi wa Wilaya ambao wana wajibu mkuu wa kusimamia uchaguzi za Rais, Wabunge, Madiwani na hata vijiji, mitaa na vitongoji.
“Aliwaagiza kuwa ni lazima CCM ishinde kila uchaguzi nao walihakikisha hivyo.
“Aliwaagiza bila kuficha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwenda kutumia nguvu zaidi ikiwemo kuweka rumande watu mbalimbali kinyume kabisa na taratibu.
“Hata alipolalamikiwa kuhusu utendaji wa baadhi ya watendaji hao, hakuchukua hatua yeyote zaidi ya kuwazawadia kwa kuwapandisha vyeo. Alipenda na kusifu ukatili wao.
“Aliamini sana katika matumizi ya ziada ya majeshi yetu. Alijijengea hofu kwa Ulinzi wake ambao haujawahi kuonekana kwa watangulizi wake. Alisahau kabisa maneno matakatifu yasemayo “Bwana asipoulinda mji, wakeshao wanafanya kazi bure.
“Silaha za moto na za kivita, doria za anga na nchi kavu, mitambo inayojulikana na isiyojulikana, askari kanzu, makomandoo na askari mbalimbali wa sare toka vikosi tofauti, misururu mirefu ya magari ya gharama yaliyofika zaidi ya 75 mara nyingi.
“Aliwaandamisha Wakuu wetu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama maeneo mengi alipokuwepo ilhali viongozi hawa wana majukumu makubwa sana katika kuongoza Majeshi yetu!.
“Hakuheshimu kabisa Bajeti ya Serikali. Japo alipiga kelele nyingi hadharani, sirini Serikali yake, hadi anatuaga ilikabiliwa na kashfa nzito za matumizi makubwa nje ya bajeti.
“Katika kipindi chake, Deni la Taifa la ndani na nje limekuwa kwa kasi ya kutisha japo wasaidizi wake mara kadhaa, na huku wakijua, wakilidanyanya Taifa uhimilivu wa deni hilo.
“Hayati Magufuli aliamini katika vyombo vya Habari na Asasi za kiraia zenye kumsifu na kumtukuza. Alidhoofisha vyombo hivi muhimu katika azma yake ya kuthibiti habari tofauti na zile za anazozitaka.
“Hakuheshimu uhuru wa Habari, bali alifarijika kwa propaganda za hila. Hakuheshimu wajibu na nafasi ya Asasi za Kiraia katika jamii. Alizidhibiti kwa mabavu na ukatili wa kidola.
“Watanzania wenzangu, Hakika hatupaswi kuruhusu haya tena! Never and Never Again!.
“Alilithibiti Bunge na kuliendesha kwa “remote control” bila kujali Bunge ni Mhimili unaopaswa kujitegemea na kimsingi kuisimamia Serikali. Kwa miaka mitano alizuia Mijadala ya Bunge isisikike kwa wananchi ambao ndiyo wanapaswa kuwakilishwa katika chombo hicho.
“Bila hofu, mara kadhaa aligawa rushwa ya fedha kwa Wabunge wa CCM waweze aidha kupitisha bajeti ya Serikali au sheria ambazo serikali yake ilijua zina walakini.
“Alimgeuza Spika na Naibu wake kama watumishi wa kudumu wa Serikali, kutwa wakishiriki kila hafla ya serikali na mikakati michafu ya kuvuruga na kudhalilisha Wabunge wa Vyama vya Upinzani; ndani na nje ya Bunge!
“Alitumia Uongozi wa Bunge kupitisha au kubadilisha sheria mbalimbali kwa lengo la kuthibiti mawazo mbadala.
“Kwa kutambua hili wakatunga sheria ya kujiwekea kinga za kisheria viongozi wakuu akiwemo, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika wa Bunge na Naibu wake dhidi ya kushtakiwa kwa makosa watakayoyatenda wakiwa madarakani.
“Mara kwa mara Bunge lilifanya kazi ya kupitisha maazimio ya kumtukuza na hata kuthibiti waliojaribu kueleza ukweli kuhusu mapungufu ya Serikali kama CAG aliyeondolewa kinyume na taratibu, Prof Assad.
“Hoja nyingi na makini za Wabunge wa upinzani zilizuiwa na Spika na wasaidizi wake kwa makusudi. Hizi ni Pamoja na Hotuba mbalimbali za Kambi ya Upinzani hususan pale walipoona zinaikosoa serikali kwa kueleza ukweli.
“Ni ushirika huohuo haramu wa Bunge na Serikali unaoweza kudiriki kuivunja Katiba na Sheria waziwazi, kwa kuruhusu Wabunge wasiowakilisha Chama chochote na ambao hawajateuliwa na Chama Chochote kufuja na kuiba pesa za umma Bungeni. Rejea Wabunge 19 walioitwa wa “CHADEMA.
“Nianze kwa kusema, naiheshimu Mahakama. Ina wajibu mkubwa wa kusimamia haki. Chini ya Hayati Magufuli, mhimili huu nao haukubaki salama sana.
“Nasikitika kusema bayana kuwa pamekuwepo kutumika vibaya kwa baadhi ya Mahakimu na hata Majaji kufanya maamuzi yasiyo ya haki kwa lengo la ama kuilinda Serikali au kuhukumu pasipo haki baadhi wa watu kwa maelekezo katika siasa.
“Hayati Magufuli alichukia sana demokrasia. Hakuwa na uvumilivu wa mawazo mbadala au kupingwa kwa njia yeyote. Alijitahidi kwa njia mbalimbali haramu kuua vyama na hata baadhi ya Wanasiasa wa Upinzani, Chama chetu CHADEMA kikiwa wahanga wakubwa!
“Alithibiti Demokrasia hata ndani ya Chama Chake cha Mapinduzi, na hata hakuona haya kutamka kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, Dodoma, utayari wake “kuwapoteza” wale waliokuwa wana mitazamo tofauti na viongozi. Kama hayawani, wajumbe zaidi ya nusu wakamshangilia!
“Alihubiri kuichukia rushwa lakini alikuwa kinara mkubwa wa kutoa rushwa: ya fedha au uteuzi katika kununua wapinzani na baadhi kuwapa uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi wa umma.
“Alitumia Taasisi kadhaa za Umma ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, Jeshi la Polisi, nk kuthibiti uhuru wa kufanya siasa kidemokrasia, ikiwemo kuzuia haki ya Kikatiba kufanya mikutano ya hadhara na vyama kujijenga.
“Kwa kushirikiana na Chama chake, CCM na Serikali yake, waliichezea Tume ya Uchaguzi kama mwanasesere. Bila aibu waliitumia tume kama chombo cha makada wa CCM.
“Tume, Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Wakuu wa Wilaya na vyombo mbalimbali vya Ulinzi na Usalama, vilishirikiana au kusaidiana kwanza kuvuruga Daftari la kudumu la wapiga kura na kisha kuiba uchaguzi mchana kweupe.
“Wizi wa chaguzi zote chini ya Utawala wa Magufuli zitaingia katika historia kama “chafuzi” badala ya chaguzi.
“Kwa miaka mitano iliyopita, uchumi wa nchi yetu umeathiriwa sana na sera mbaya za kodi pamoja na sheria zisizoaminika na kutabirika.
“Mali na mitaji ya wawekezaji ilichukuliwa kwa mabavu, makampuni yalifunga biashara zao na mengine kuondoka nchini. Hili lilihusu wawekezaji wote wa nje na ndani.
“Ajira kwa vijana wetu zilikosekana kutokana na wawekezaji kuondoa mitaji yao na au kuondoka nchini, wapo waliopunguzwa kazi.
“Katika awamu hii dunia ilikumbwa na ugonjwa wa virusi vya Corona hali iliyopelekea kila Taifa kutafuta ufumbuzi wa kisayansi katika kukabiliana na ugonjwa huu.
“Tanzania ilionekana kituko kwa jinsi ambavyo iliamua kupuuzia sayansi na kuamua kujitenga na ulimwengu katika kuunganisha nguvu ili kupambana na ugonjwa huu na badala yake tukaamua kutumia biba za asili zisizokuwa zimefanyiwa utafiti.
“Wengi wamepoteza maisha ikiwamo viongozi wenyewe kwa uzembe wa ungeoweza kuepukika. Dunia inaingia kwenye utaratibu mpya wa Vaccination Passport. Sisi hatuna chanjo. Jambo hili siyo la kusubiri Watu wanakufa. Rais hapa achukue hatua za haraka na dharura.
“Hakuna kipindi nchi yetu iliathirika kwenye mahusiano ya kimataifa kama kipindi cha Serikali ya awamu ya Tano.Itoshe kusema tulionekana kituko kwa Jumuiya ya Kimataifa.Tuliivuruga heshima yetu ya kidiplomasia ambayo tuliijenga kwa muda mrefu na kuheshimika ulimwenguni kote.
“Katika kipindi hiki tulishuhudia marafiki zetu wa muda mrefu wakiwa hawaheshimiwi na badala yake walibatizwa majina ya kubezwa na kudharauliwa.
“Unafiki, Ujinga, Umaskini na Woga ndiyo umetufikisha hapa. Tumeanza kuona dalili za kuyumba kwa mitazamo kwa makada wa CCM na Serikali yao kwa kiwango cha kutisha baada ya yeye kutangulia mbele ya haki.
“Itoshe kusema bila unafiki; Utawala wa Awamu ya Tano umeiumiza na kuipasua nchi yetu kwa kiwango cha kutisha. Kikubwa na kibaya zaidi, umepandikiza chuki na mpasuko wa kutisha miongoni mwa Watanzania. Yes, Never and Never Again!
“Ni rahisi sana kwa kila mtu ndani ya Serikali na CCM leo kumlaumu Marehemu. Kwamba kila baya lililofanyika anatupiwa yeye. Ukweli ni kuwa mfumo mzima wa Utawala ulishirikiana kutekeleza ubatili na ukatili mwingi uliofanyika.
“Magufuli aliasisi utawala wa mabavu, usioheshimu Katiba wala Sheria kupitiliza. Serikali yake yote ilishuhudia na kumsaidia kutekeleza bila kujali madhara waliyosababishia Taifa na Watanzania kwa ujumla wao.
“Wamelikosea sana Taifa hili na Wanastahili kutubu na kuwaomba Watanzania msamaha. Sote lazima sasa tuseme KAMWE NA KAMWE TENA!
“Chama cha Mapinduzi nacho, hakiwezi kabisa kukwepa lawama. Kilibariki ukatili huu maadam ulikihakikishia kubaki madarakani hata kwa kuisigina Katiba inayobeba sheria mbalimbali za nchi zinazotoa Haki na Uhuru kwa Watanzania. Nimekitafakari kwa kina sana CCM.
“Nimetafakari sana Viongozi wake Wastaafu na waliopo kazini. Waliweza vipi kwa miaka mitano kushiriki huku wakilalamika sirini ubakaji mkubwa wa Haki katika nchi yetu. Hawa nao wamelibaka mno Taifa letu na hawastahili tena kupewa dhamana ya kusimamia maisha yetu!
“Makundi mbalimbali yalijenga tabia ya kinafiki ya “kumtukuza kupitiliza” na kuendelea kumuharibu Hayati Magufuli. Hawa ni pamoja na viongozi wetu wengi wa dini, wanazuoni, vyombo vya Habari vya umma na binafsi.
“Kazi hii iliratibiwa kwa ukaribu na idara ya Usalama wa Taifa. Juhudi na gharama kubwa ilitumika kufunika ukweli. Propaganda iligeuzwa sera rasmi ya serikali. Uzalendo uligeuzwa kutoka kuwa mapenzi kwa nchi na kuwa mapenzi kwa Rais.
“Hebu tutafakari kwa Pamoja ukweli ufuatao! Kwamba nchi nzima viongozi wote wa kiserikali wanaostahili kuchaguliwa na wananchi, chini ya awamu ya tano asilimia 98 wanatoka chama cha Mapinduzi.
Bila hofu, Serikali ya awamu ya tano, imepora uchaguzi wa Serikali zote za Mitaa nchi nzima na mwaka jana uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani! Tunaongozwa na ambao hatukuwachagua! Wanaepuka vipi lawama!! Lazima sasa tuseme KAMWE NA KAMWE TENA! Yes, NEVER AND NEVER AGAIN!!
“Nimemwandikia Rais na Mama yetu barua. Pamoja na mambo mengine nimemweleza kuwa maneno yake haya, yamegusa mioyo ya wengi wenye hofu ya Mungu ikiwemo sisi wa CHADEMA.
“Hata hivyo, sisi wa CHADEMA, kwa kiwango kikubwa, bado mioyo yetu inabubujikwa na damu. Macho yetu bado yanatiririka machozi mara kwa mara kwa tuliyopitia na tunayoendelea kupitia.
“Tumepokea ahadi yake hii, kwa tahadhari na mashaka makubwa kwani tunatambua jinsi uhafidhina na ubinafsi ndani ya CCM na Serikali yake unavyoweza kuuwa dhamira na haiba njema ya wachache miongoni mwao wanaojitambua.
“Tumemwomba rasmi kukutana naye, tuweze kumweleza ni kwa vipi mioyo yetu inavuja damu na ni kwa vipi macho yetu yanatiririsha machozi. Hatukusudii kumzingua. Nasi hatutegemei kuzinguliwa.
“Hatuko kwenye biashara ya siasa, bali tunautafuta ufumbuzi utakaotutoa kwenye mkwamo huu na utakaorejesha haki na furaha na ustawi kwa wote.
“Tunategemea kumweleza na kumkabidhi Mhesimiwa Rais mapendekezo kadhaa ya kina ya namna bora ya kuuanza ukurasa mpya katika Nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa kujenga utengemano wa Taifa.
“Kama viongozi na wanasiasa wazoefu tunatambua Rais ana majukumu mazito ya kuipanga Serikali yake. Hata hivyo tunaamini, atatambua vilevile nafasi ya Vyama vya Upinzani katika kuutengeneza mustakabali mwema na mpya wa nchi yetu.
“Rais wetu, ni zao la CCM. Kwa mukhtadha huu, yeye alikuwa mshiriki namba mbili wa Utawala wa awamu ya Tano. Kwa kupenda au kwa bahati mbaya, hawezi kukwepa kwa njia yeyote ile uchafu, mabaya na madhambi yote yaliyofanywa na Serikali hiyo.
“Walipenda kujipongeza kwa sifa nyingi za kipropaganda. Utakwepa vipi uwajibikaji wa pamoja? Baba wa Taifa alizungumza dhana ya kujisahihisha. Rais Samia una nafasi ya kusahihisha makosa makubwa ya mtangulizi wako. Nawe usisite kuomba radhi. Tutakuelewa zaidi.
“Kipekee, tunakushukuru Rais wetu, Samia Suluhu kwamba ulikuwa kiongozi pekee mwandamizi wa Serikali ya awamu ya tano uliyejitwika ujasiri kwenda kumjulia hali kiongozi mwenzetu Mhe. Tundu Lissu alipolazwa hospitali ya Nairobi Kenya baada ya kushambuliwa na wasiojulikana.
“Kauli za Rais, Mama Samia Suluhu Hassan zinatuchanganya na anapaswa kulijua hili. Anapoongea nia yake ya kuenzi sera, mipango na tabia ya Magufuli, Taifa linasinyaa na kuhuzunika.
“Anapotoa kauli na maelekezo yanayopingana na misimamo ya Boss wake wa zamani, Taifa linafurahi na kushangilia. Huhitaji shahada ya uzamivu kujua kwanini hili liko hivi. Ni zao la mbegu alizopanda mtangulizi wake.
“Hatupaswi kumtakia mabaya kwa sababu tu ni zao la CCM. Bali tunatakiwa kuongeza juhudi na maarifa kumkabili kwa ushindani wenye kujenga na siyo wa kubomoa. Tunamwombea afanye mema wakati wa utawala wake ili kupata ustawi wa Taifa letu.
“Hakika kama atamuenzi Hayati Magufuli, ahadi yake ya tarehe 19 Machi baada ya kuapishwa haitakuwa na maana yeyote na hatutapaswa kumwamini. Magufuli aliamini hatustahili kuishi. Hata hivyo hatuamini katika kisasi. Hakika kisasi ni cha Mungu.
“Wote tumejifunza, serikali ikiharibikiwa, nchi yote inaingia simanzi. Hii haina maana sisi wa CHADEMA tumegeuka waimba mapambio wa Rais Mama Samia. Inatupa sisi changamoto ya kuongeza juhudi za kuboresha sera zetu na kuongeza ushindani wa hoja.
“Wanachadema wote,hatutakuwa tayari kwa gharama yeyote kuiona nchi yetu na Chama chetu kikirejeshwa wakati wowote kwenye dhambi na ubatili unaofanana na utawala wa Hayati Magufuli. NEVER AND NEVER AGAIN!! Maana yake salaam hii inapaswa kutupa nguvu mpya na mwelekeo mpya.
“Siku zote nimesema safari ya ukombozi wa kifikra ni nyenzo muhimu katika kujenga Taifa linalojitambua. Hakuna njia ya mkato katika kuipata Tanzania yenyehaki na furaha, isipokuwa kwa kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi na Serikali yake.
“Ni mvinyo ule ule kwenye chupa mpya. Hadi hapo azma yetu itakapotimia, hatuna budi kubanana kwa ku-coexist ili kuupata mfumo rafiki wa demokrasia ya kweli.
“Kama nilivyodokeza kwenye hotuba yangu ya Januari, chama chetu kinajiandaa kwa mikakati mingi mipya ili kuimarisha azma yetu kwa vitendo.
“Muda si mrefu, chama chetu kitaanza rasmi Operation Maalum yenye lengo la kukihuisha na kuuandaa umma wa Watanzania kujua hatma ya nchi yao iko mikononi mwao.
“Wajibu huu, tutauzindua karibuni na utatufikisha nchi nzima.Kwa sababu za kimkakati na kiusalama, itoshe kuishia hapo na kuwaomba wapenzi,wanachama na wote wanaokitakia mema chama chetu popote walipo wajiandae.Taarifa rasmi zitatolewa na mifumo yetu ya uongozi na utawala.
“Watanzania wenzangu, tunakubaliana nchi hii ni yetu sote. Tumefika hapa tulipo kwani wengi wetu tumejiaminisha kuwa jukumu la kuitetea na kuilinda nchi yetu ni la wanasiasa wa Upinzani pekee. Tunalalamika bila kuchukua hatua.
“Tumefika hapa kwa sababu tumekuwa legelege! Tumefika hapa kwa sababu Katiba tuliyonayo inatoa nafasi ya Udikteta na Urais wa Kifalme. Wote tumeshuhudia namna Magufuli, Chama Chake na Serikali yake walivyovunja hata hii katiba tunayolilia kuibadilisha.
“Uhitaji wa Katiba Mpya haupaswi kuwa utashi binafsi wa Rais au Chama chake. Hapapaswi kuwepo mjadala kama tunaihitaji ama la! Mjadala unapaswa kuwa, tunajiwekea utaratibu gani na ratiba gani ya kuipata Katiba iliyo bora na yenye maridhiano.
“Lazima tuwe na Katiba itakayoweza kujenga Taasisi imara zinazoweza kuthibiti viongozi wetu na yeyote mwenye dhamana anapojaribu dhambi ya kuivunja Katiba. Msingi huu, ndiyo utakaotupa kesho yetu iliyo endelevu na yenye majibu ya maswali na mikwamo mingi ya kimfumo!
“Mabadiliko ya Katiba yatakuwa na tija zaidi iwapo Watanzania watabadilisha fikra zao, mtazamo wao na ushiriki wao katika harakati za kudai uwajibikaji wa viongozi na taasisi za umma.
“Naomba mtuamini. Tutaendelea kukijenga Chama chetu kwa uaminifu na wivu mkubwa huku tukipigania maslahi ya Taifa bila kuchoka wala kukatishwa tamaa. Tumepita pagumu sana lakini Mungu wetu alisimama nasi. Siku zote tunaanza naye na hapa nahitimisha naye.”