FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Tundu Lissu, Makamu mwenyekiti, leo wameendelea na mikutano ya kuimarisha Chama hicho katika mikoa ya kanda ya ziwa, huku hotuba zao zikijadili zaidi hali mbaya ya uchumi wa pamba, dhahabu na kupanda kwa bei za mafuta ya petrol na diesel nchini.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika mikutano nane aliyoifanya leo kwenye kata mbalimbali za majimbo ya Geita Vijijini, Nyagh’wale na Geita Mjini, Mbowe amesema sera mbovu na.ufisadi ndani ya serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), vimesababisha Geita kubaki maskini, licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa dhahabu na pamba.
Amesisitiza kuwa siasa ni maisha na kwamba gharama ya kupuuza siasa ni wananchi kuzidi kutawaliwa na viongozi mafisadi na wasio na maarifa yoyote ya kuliletea maendeleo Taifa.
“Ukipuuza siasa utakutana nayo kwenye bei ya Petrol na Diesel zilizopanda hivi sasa…utakutana nayo kwenye kilo ya Unga na kwenye umaskini wenu,” alisema Mbowe.
“Hata sisi tuna watoto na wake zetu ambao tungependa kukaa na kufurahi nao majumbani mwetu, lakini tumeamua kuifanya kazi hii ili kuikwamua nchi yetu. Vyama vingi vilitishwa na Magufuli vikajifia, vingine vimefunga ndoa na CCM. Leo siasa ya Tanzania imebaki kuwa ni mbio za Farasi wawili… ni kati ya CCM inayowapeleka gizani na Chadema tunaotaka kuwapeleka kwenye nuru. Tumekuja tujadili hali mbaya ya maisha yenu, tukiwasihi tuungane pamoja kuikomboa nchi yetu,” alisema Mbowe.
Akizungumzia uchumi wa Pamba, Mbowe alisema bei ya zao hilo imezidi kuporomoka hadi kufikia Shilingi 1,060 kwa kilo.
Aliongeza kuwa sababu ni kuwepo kwa genge la vigogo wa CCM na serikali yake walioamua kuhodhi soko la Pamba na kujipa mamlaka ya kupanga bei ndogo ili kuwanyonya wakulima.
Taarifa zinaonesha kuwa Pamba imewahi kuuzwa kwa zaidi ya Shilingi 2,040 kwa kilo moja kabla ya kuporomoka hadi kufikia bei ya sasa ya Shilingi 1,060 kwa kilo.
Mbali na bei ndogo, tija ndogo katika kilimo cha Pamba, imechangia kuangusha uchumi wa Pamba na kumnyima mkulima fursa ya kutengeneza kipato kikubwa.
Aidha, kwasababu ya kukosa pembejeo, huduma bora za ugani na zana za kisasa za kilimo, wakulima wa Pamba katika mkoa wa Geita na mikoa mingine, wamekuwa wakivuna wastani wa Kilo 200 kwa ekari moja, wakati katika nchi zenye kilimo cha kisasa cha Pamba, kama Brazil, mkulima hupata mpaka kilo 3,000 za Pamba kwa ekari moja, tija ambayo ni zaidi ya mara kumi ya Tanzania.
Kwa upande wake, Lissu, akihutubia wananchi wa Geita mjini, alisema mikataba mibovu ya uwekezaji kwenye madini iliyoingiwa na serikali ya CCM, leo imesababisha nchi kukosa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni na hivyo kushindwa kuagiza mafuta ya Petrol na diesel kwa wingi na matokeo yake ni kupanda kwa bei za mafuta hayo pamoja na kupanda kwa gharama za maisha.
“Leo hapa Geita nimeuziwa mafuta lita moja Shilingi 3, 280. Waziri wa Nishati na Madini, January Makamba amesema bei za mafuta zimependa kwasababu nchi yetu haina dola za kutosha za Kimarekani. Sasa tujiulize, dola zimekwenda wapi wakati tuna migodi ya dhahabu inayopaswa kutuingizia pesa nyingi za kigeni,” alihoji Lissu.
Akifanya uchambuzi wa kitakwimu, Lissu alisema thamani ya dhahabu yote iliyochimba nchini na kuuzwa nchi za nje kwa mwaka wa fedha 2021/22 ni Dola za Marekani Bilioni 3.6, sawa na Shilingi za Kitanzania Trilioni 8.6, lakini nchi yetu ilipata mapato ya Dola milioni 85.6 tu kama kodi, sawa na Shilingi Bilioni Moja na Milioni 732 za Kitanzania.
“Mapato hayo tuliyopewa ni sawa na asilimia 0.86 tu ya fedha zote walizochota wawekezaji kutoka katika madini yetu, ” alisema Lissu na kuongeza.
“Geita, inakotoka dhahabu yenye thamani ya Dola Bilioni Moja za Kimarekani, sawa na Shilingi Bilioni 210 za Kitanzania kwa mwaka, iligawiwa mapato ya Dola 700,000 tu, sawa na Shilingi Bilioni Moja na Milioni 732. Mapato hayo mliyopewa Geita ni zaidi ya asilimia sifuri ya kile alichochota mwekezaji
“Kwa hiyo, leo nchi haina dola za kutosha za Kimarekani kwaajili ya kuagiza mafuta, kwasababu ya mikataba hii ya hovyo ya madini iliyoingiwa kichwa kichwa na serikali za CCM kuanzia serikali ya Hayati Rais Benjamin Mkapa. Mikataba mingine ni ya vitalu vya mafuta na gesi asilia iliyoingiwa na rais mstaafu Jakaya Kikwete. Ndiyo maana tunampinga huyu Mama na mkataba wake wa bandari na Waarabu, kwasababu tuna uzoefu na mikataba hii mibaya inayonyonya nchi,” alisema Lissu.
Lissu aliwataka wananchi wa Geita kujiunga Chadema kwa wingi ili kuing’oa CCM madarakani na kulijenga upya Taifa letu.
Akiwasili katika mkutano wa Geita Mjini dakika za mwisho mwisho baada ya kuchelewa kutoka kwenye mikutano mingi aliyoifanya siku ya leo, Mbowe aliendesha kura ya wazi, ambapo maelfu ya wananchi waliunga mkono msimamo wa Chadema unaopinga mkataba wa uendelezaji bandari na maeneo mengine ya kiuchumi, ulioingiwa na serikali ya Tanzania na Dubai.