Mbowe, Lissu wamshika pabaya Samia

– Chadema, Mikataba ya Uwekezaji vyaiweka pabaya CCM

HALI ya kisiasa ya Rais Samia Suluhu Hassan inazidi kuwa mbaya, akionekana kuathiriwa zaidi na mikataba tata ya uwekezaji iliyoingiwa na serikali yake, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikijiimarisha na kupata uungwaji mkono katika maeneo mbalimbali nchini, SAUTI KUBWA linathibitisha.

Tangu kufanyika kwa ziara za mikutano ya hadhara na uimarishaji mtandao wa Chadema, iliyopewa jina la *Operesheni +255*, katika kanda zake za kichama, ikianzia Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora, ikafuatia kanda ya Ziwa Victoria ya mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza, na sasa ikiingia kanda ya Serengeti yenye mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara, chama hicho kimeonekana kupata uungwaji mkono mkubwa si tu kwa mahudhurio bali pia kwa wimbi kubwa la wananchi wanaolipia ada ya uanachama na kujisajili kwenye kanzidata ya kidigitali ya wanachama wa Chama hicho.

Katika mikoa yote takribani sita iliyofikiwa mpaka sasa, Chadema imefanya mikutano mikubwa zaidi ya 240, ikifikia majimbo yote, tarafa zote na kata nyingi, huku ikiwa imetawanya pia timu nyingi zinazofanya uhamasishaji wa mtu kwa mtu wa kupata wanachama na kuimarisha safu za uongozi za chama hicho.

Mikutano ya Chadema imerejesha shauku ya wananchi kushiriki, kufuatilia, na kujadili siasa baada ya zuio la mikutano ya hadhara lililokuwa limedumu kwa takribani miaka saba.

Wakati Chadema ikizidi kuchanja mbuga, hali si shwari kwa rais Samia Suluhu Hassan na chama chake (CCM), kwani wamekuwa wakihaha kujibu tuhuma za kile kinachoitwa “kuuza nchi” kupitia mkataba tata wa ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na Dubai, ambao umechambuliwa kuwa unakibidhi sehemu kubwa ya uendeshaji wa shughuli za bandari na maeneo mengine ya kiuchumi kwa kampuni ya Dubai ya DP World.

Hata hivyo, jitihada za CCM kufanya mikutano ya hadhara ya kikanda kwenye baadhi ya miji mikubwa kama Mbeya, Dar es Salaam na Mwanza, wakijaribu kufanya kile walichokiita kuelimisha wananchi kuhusu mkataba wa bandari, bado hakijaonekana kuzaa matunda. Mjadala wa bandari umeendelea kuwa moto.

Hata baada ya mikutano hiyo ya CCM, bado wadau wengi wameendelea kuupinga vikali mkataba huo wa bandari unaopigiwa chapuo na serikali ya rais Samia na chama chake (CCM). Miongoni mwao ni Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki ambao limetoa Waraka uliosainiwa na Maaskofu 37 wa kanisa hilo wakiweka wazi msimamo wao wa kuupinga mkataba huo na kuishauri serikali ya rais Samia iachane nao.

Waraka wa TEC unaelezewa kuwa ni pigo jingine kubwa dhidi ya serikali ya rais Samia, kwani Kanisa Katoliki linafahamika kuwa moja ya taasisi kubwa za dini zenye waumini wengi.

Wakati sakata la “Mkataba wa Bandari” Chadema, kimemtumbukiza tena Rais Samia, kwenye kashifa nyingine kubwa, kikidai amevunja sheria za nchi na kugawa kimya kimya maliasili za misitu, maeneo ya hifadhi za taifa na mbuga kwa wawekezaji wa kigeni, bila Bunge kushirikishwa wala kuridhia mikataba ya uwekezaji huo.

Rais Samia anatuhumiwa kugawa kiholela jumla ya hekta milioni nane za misitu ya Tanzania kwa wawekezaji wa Kiarabu kutoka Dubai kwa mkataba ambao umesainiwa bila kuwekwa wazi na kupata ridhaa ya Bunge.

Anatuhumiwa pia kuhamisha wananchi wa jamii ya Kimasai na kugawa maeneo ya hifadhi za Ngorongoro na Loliondo kwa wawekezaji wa Kiarabu, kinyume cha sheria kwani mikataba hiyo haijapata ridhaa ya Bunge.

Aidha, anahusishwa pia na ugawaji wa ekari milioni sita za mbuga ya wanyama kwa kampuni ya Mwiba Holdings inayodaiwa kumilikiwa na Bilionea wa Kimarekani, Dan Friedkin, bila bunge kushirikishwa kwenye kupitia na kuridhia mkataba wa uwekezaji huo.

Kutokana na kile alichokiita “kukithiri kwa ugawaji na uuzaji wa maliasili na raslimali za nchi”, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, amewaomba Watanzania kote nchini kuzidi kuamka na kujiunga kwa wingi na chama hicho ili kuokoa urithi wa raslimali za watoto wa Kitanzania, alizodai zimezidi kugawiwa kiholela kwa wageni, hata chini ya serikali ya sasa ya rais Samia Suluhu Hassan.

Mbowe ameyasema hayo leo mjini Shinyanga wakati akifunga mkutano wa uzinduzi wa Operesheni +255 kwenye kanda ya kichama ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.

Operesheni hiyo yenye ujumbe wa *”Katiba Mpya:Okoa Bandari Zetu”*, inalenga kuibua kero na matatizo ya wananchi, ikinadi sera za Chadema na kujenga mtandao imara wa chama hicho nchi nzima.

Akiwasili dakika za mwisho na kuzungumza kwa ufupi, baada ya kuchelewa kwenye mkutano huo kwasababu za kiufundi, Mbowe alisema:

“Miaka 62 ya uhuru, serikali za CCM wamethibitisha kwamba hawana uwezo hata kidogo wa kuwaondoa Watanzania kwenye umaskini mkubwa unaowakabili. Uwezo pekee waliobakia nao ni wa kugawa na kuuza raslimali zetu

“Nawaomba Watanzania wote, kote nchini tuzidi kuamka na kukipokea Chama hiki, tukikumbatie chama hiki, mjiunge kwa wingi, kwa pamoja tupiganie na kuokoa urithi wa raslimali za nchi yetu ambazo zimezidi kugawiwa na kuuzwa kiholela,” alisema Mbowe.

Kwamba, kwa mwenendo huo, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake, wamekuwa si viongozi wa nchi, bali ni kikundi cha madalali tu kinachofanya kazi ya kunadi, kugawa na kuuza kila raslimali za nchi kiholela, kwa maslahi yao binafsi.

Awali, akichambua tuhuma hizo za ugawaji wa maliasili za nchi, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, alisema, rais Samia amevunja Sheria ya Enzi kuu ya Nchi inayoipa nchi Mamlaka ya Kulinda Umiliki wa Maliasili, “The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignity) Act”, ya mwaka 2017, iliyopitishwa wakati wa utawala wa hayati rais John Pombe Magufuli.

Kwamba, wakati Sheria hiyo inataka mikataba yote ya uwekezaji katika maliasili kuidhinishwa na Bunge, rais Samia, ameingia mikataba yote hiyo ya uwekezaji bila Bunge kushirikishwa katika kupitia au kuridhia mikataba hiyo kama sheria inavyotaka.

Lissu, ambaye pia ni Wakili, aliongeza kuwa sheria nyingine iliyovunjwa na rais Samia ni Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Katika Mikataba ya Maliasili za Nchi, “The Natural Wealth and Resorces Contracts (Review and Re-negotiations of Unconscionable Terms) Act”, nayo ya mwaka 2017.

Kwamba, wakati Sheria hiyo inalipa Bunge nguvu ya kupitia upya mikataba yote inayokwishaingiwa na serikali kuhusiana na maliasili za Tanzania, rais Samia hajalipa Bunge haki na wajibu wa kupitia mikataba hiyo ya uwekezaji iliyoingiwa na serikali yake mpaka sasa, hali inayoibua shaka kuhusu maslahi ya Taifa kuhatarishwa ndani ya mikataba hiyo.

“Huyu anayesambaza mabango ya picha zake nchi nzima, akijiita ni Mnyenyekevu, ni Mzalendo, sijui nini….kama kweli yeye ni Mzalendo basi tunataka aoneshe uzalendo wake kwa kuweka wazi mikataba yote ya uwekezaji waliyosaini na kuwagawia wawekezaji maliasili zetu,” alisema Lissu.

Aliongeza kuwa hayati Rais Benjamin Mkapa alibinafsisha kiholela mashirika ya umma 450, pamoja na migodi yote ya madini, kisha akafuatiwa na rais Kikwete aliyedai kuwa aliwapa wageni vitalu vya gesi asilia na mafuta na kwamba sasa ugawaji na uuzaji holela wa raslimali za nchi unaendelezwa kwa kasi kubwa zaidi na rais Samia.

“Magufuli, yeye alijaribu kurejesha raslimali za nchi, lakini alikwama kwasababu alifanya kama mtu ambaye hakwenda darasani, hakuwa na uelewa wala maarifa ya kushughulika na mikataba ya uwekezaji, akaishia kuitia nchi hasara kubwa kwa kushitakiwa na wawekezaji,” alisema Lissu, na kuongeza

“Sasa amekuja huyu anayeitwa “Nani kama Mama”. Ndani ya mwaka mmoja tu, tayari keshagawa bandari zetu zote kwa Waarabu, kahamisha wananchi kule kwenye hifadhi za Ngorongoro na Loliondo kwaajili ya kuwapa Waarabu, kagawa hekta milioni 6 za maliasili za misitu kwa Waarabu hao hao wa Dubai. Na kuna taarifa kuwa wamegawa ekari milioni 6 za mbuga ya wanyama kule Meatu kwa bilionea wa Kimarekani anayeitwa Dan Friedkin.

“Tuna kazi moja tu ya kufanya, nayo ni kuungana Watanzania wote ili tupiganie urithi huu wa watoto zetu unaogawiwa kwa wageni.”

Tathmini fupi iliyofanywa na SAUTI KUBWA kwenye mikoa ya kanda ya ziwa Victoria, ya Kagera, Geita na Mwanza, imebaini kuwa Chadema imefanikiwa kufufua na kuimarisha ngome zake.

Like