MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametoa michango mbalimbali ya kifedha kusaidia jamii akiwa katika ziara ya chama hicho inayoendelea kwenye mikoa ya kanda ya ziwa kwa miezi miwili sasa.
Hivi majuzi, akiwa wilayani Kishapu, mkoani Simiyu, Mbowe, aliguswa na matatizo ya Shule ya Msomagedi, iliyopo Kata ya Msomagedi, ambayo inahitaji matundu ya choo na nyumba ya mwalimu.
Kutokana na hali hiyo, Mbowe alitoa fedha taslimu, shilingi milioni moja (1,000,000), kwa ajili ya kuchangia utatuzi wa changamoto hizo.
Akiwa wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera, wiki chache zilizopita, Mbowe alishiriki ibada katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kayanga, ambapo alichangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa la usharika huo.
Vile vile alichanga shilingi milioni mbili na laki nane (2,400,000) kwa ajili ya kugharamia uandaaji wa sare za kwaya nne za usharika huo.
Akiwa wilayani Misenyi, mkoa wa Kagera, Mbowe aliguswa na tatizo la mwananchi aliyebomolewa nyumba, Mzee Terestori Ludovick, mwenye miaka 101 (pichani juu).
Ilielezwa kuwa nyumba ya mzee huyo ilivunjwa na serikali kwa madai kuwa aliijenga ndani ya ardhi iliyokuwa chini Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.
Mbali na mzee Ludovick, wananchi wengine wengi walihamishwa kwenye maeneo yao ya asili yaliyopo kwenye mji wa Mutukula, wakidaiwa ni wavamizi.
Maeneo waliyokuwa wakiyakalia sasa yamekabidhiwa kwa mwekezaji kwa ajili ya shughuli za ufugaji lakini wananchi hawakulipwa fidia yoyote.
Kutokana na mzee huyo kukosa nyumba ya kuishi, Mbowe alichangia ujenzi wa nyumba yake. Alitoa shilingi milioni mbili (2,000,000).
Baada ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu, Oparesheni ya mikutano ya hadhara na uimarishaji wa mtandao wa Chadema, leo imeingia katika mkoa wa Mara.