AKIHUTUBIA maelfu ya wananchi katika mikutano sita aliyoifanya jana 26.08.2023 kwenye majimbo ya Ushetu na Kahama, mkoani Shinyanga, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amekutana na vilio vya wananchi kuhusu zao la Pamba, Tumbaku na Madini katika majimbo hayo.
Kuhusu tumbaku, imeelezwa kuwa asilimia 80 ya wakulima wa zao hilo katika jimbo la Ushetu wamekopwa tumbaku yao, bila kulipwa na makampuni yaliyopaswa kununua tumbaku hiyo kupitia vyama vya msingi.
Kampuni zinazotuhumiwa zaidi ni Vodsel na Mkwawa, zikidaiwa kukopa tumbaku ya wakulima wengi tangu mwezi Mei mwaka huu na kushindwa kulipa mpaka sasa.
Akizungumzia malalamiko hayo, Mbowe, mbali na kutaka walipwe stahiki zao, amewaomba wakulima wote wa tumbaku nchini kuachana kabisa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwani serikali ya chama hicho ndiyo iliyohusika kuleta kampuni hizo zillizoshindwa kuwalipa mpaka sasa.
“Nawaomba mjiunge kwa wingi Chadema, muachane na CCM, hilo ndiyo jibu la msingi la kukomesha utapeli huu dhidi ya tumbaku yenu,” alisema Mbowe.
Imeelezwa kuwa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Tumbaku ndiyo waliyohusika katika kuyapitisha makampuni hayo ya ununuzi wa tumbaku yanayolalamikiwa na wakulima.
Mbali na kuongeza makali ya umaskini wa kipato, kuendelea kutolipwa tumbaku yao kunasababisha wakulima hao kuingia hasara kubwa kwani walikopa mkopo wa pembejeo benki na riba ya mkopo huo inazidi kuongezeka.
Mbali na tumbaku, wakulima wa pamba katika majimbo ya Ushetu, Kahama na maeneo mengi ya mkoa wa Shinyanga wanalalamikia kuporomoka vibaya kwa bei ya pamba kutoka shilingi 2040 hadi 1060 kwa kilo, huku wabunge wa CCM kwenye ukanda huo wakidaiwa kuwa ndiyo wanunuzi wakuu wa pamba hiyo kupitia makampuni yao.
Wananchi wanahoji ikiwa wabunge ndiyo wanunuzi wa pamba wanaofaidika na bei ndogo inayomnyonya mkulima, watawezaje kuwatetea wananchi ili bei ya kuuzia pamba ipande?.
Mbunge wa Ushetu, Emmanuel Cherehani, ametajwa katika tuhuma hizo.
Akiwa Kahama mjini Mbowe alizungumzia zaidi madini, akisema uongozi mbaya wa serikali za CCM umesababisha nchi kuingia mikataba mibaya na wawekezaji kwenye sekta ya madini, gesi alisia na mafuta, huku wananchi wakibaki kwenye umaskini kwasababu ya mikataba hiyo kuwanufaisha zaidi wawekezaji kuliko nchi.
“Kahama mna dhahabu, mkoa wa Shinyanga una almasi….almasi ndiyo madini ghali zaidi duniani. Pamoja na utajiri wote huo, Kahama hamna maji safi na salama, huduma za afya ni duni, elimu inayotolewa si bora, na vigogo wa serikali na Watanzania wenye pesa wanasomesha watoto wao Kenya, Uganda na nchi nyingine kwasababu elimu ya Tanzania si bora.
“Nawaomba Watanzania wa Kahama, kioneni chama hiki (Chadema) kuwa ndiyo suluhisho na kimbilio la matatizo yenu. Chama hiki si cha Mbowe, ni chenu, kipokeeni, kitumieni kujikomboa,” alisema Mbowe.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa mbunge wa Kahama, James Lembeli, naye ameibukia kwenye mkutano wa Chadema uliofanyika kwenye kata ya Bulungwa uliohutubiwa na Mbowe.
Akisalimia wananchi wa kata hiyo, Lembeli, aliyewahi kujitoa CCM na kuhamia Chadema kabla kurejea tena CCM wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, alisema CCM na serikali yake wamezidi kukumbatia rushwa na kwamba yeye hapendi rushwa wala uuzaji holela wa raslimali za nchi, hivyo ataeleza msimamo na mwelekeo wake wa kisiasa hivi karibuni.