Mazungumzo ya rais na maaskofu Ikulu yavuja, yaibua maswali magumu sita

MAZUNGUMZO kati ya Rais John Magufuli na viongozi wa dini ya Kikristo, ambayo makanisa na Ikulu wamekuwa wanayafanya kuwa  siri, yamevuja na kuibua masuala yapatayo sita.

Rais Magufuli alikutana na viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) tarehe 7 Agosti mwaka huu, katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Baada ya vikao vyao, rais na viongozi hao walipiga picha na kutoa kauli za jumla jumla ambazo zilirekodiwa na studio za kurugenzi ya mawasiliano Ikulu, zikasambazwa katika vyombo vingine vya habari. Lakini Ikulu haijawahi kusema wala maaskofu hawajawahi kusema popote kilichozungumzwa kati yao na rais.

SAUTI KUBWA limefanikiwa kupata baadhi ya masuala hayo kutoka chanzo kilichopo karibu na ofisi ya rais, kwa sharti la kutotajwa jina. Baadhi ya mambo waliyojadili yanazua maswali.

Kwa mfano, wakati ilidaiwa kuwa maaskofu walifika Ikulu ili kujitambulisha kwa rais, baadhi ya wapambe wa rais wanasema rais ndiye aliwaita ili kuongea nao kwa kuitikia “ushauri” aliopewa na viongozi wastaafu waliomtaka asikae mbali na viongozi wa dini. Lakini Rais Magufuli mwenyewe aliweka bayana kuwa viongozi hao wa dini ndio waliomba kuonana naye.

Kwamba suala la nani aliomba kumwona mwingine linaonekana siri na lina uzito katika mawazo ya rais, ni swali ambalo kwa sehemu tu jibu lake linapatikana katika masuala mengine matano yaliyozungumzwa.

Nyaraka za kichungaji zawa “msumari wa moto”

SAUTI KUBWA linaeleza pasipo shaka kuwa miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa mwanzoni kabisa ni nyaraka za kichungaji za makanisa hayo ambazo ziliikera serikali na kusababisha misukosuko kadhaa serikalini na katika jamii tangu kipindi cha Kwaresma na Pasaka ya mwaka huu.

Rais Magufuli alitumia fursa ya vikao hivyo kueleza kwa kirefu mawazo yake na msimamo wake kuhusu anakotaka kupeleka taifa. Katika kusisitiza hilo, alieleza viongozi hao, kila kundi kwa nafasi yake, kwamba nyaraka za makanisa hayo zilimsikitisha sana.

Alisema nyaraka hizo zimekuwa “msumari wa moto” katika moyo wake. Chanzo kinasema rais alifikia mahali akawaambia maaskofu, “nilijiuliza uzalendo wa mababa hawa umeenda wapi?”

Mithili ya mtu asiyejua historia, utaratibu, na umuhimu wa nyaraka hizo kwa waamini, huku akitaka kuonyesha kwamba nyaraka za kichungaji zilimlemga yeye binafsi, rais alihoji maaskofu kwa nini waliamua kuandika nyaraka badala ya kuonana naye na kuzungumza naye.

Kwa karne nyingi, nyaraka za kichungaji zimekuwa sehemu ya jukumu la kitume la maaskofu. Hapa nchini, kwa miaka yote na katika awamu zote za utawala, makanisa yamekuwa yanatoa nyaraka hizo.

Lakini Rais Magufuli anataka ionekane kwamba yeye ndiye aliandikiwa nyaraka, kana kwamba anaagiza makanisa yasitoe tena nyaraka za kichungaji zenye ujumbe mzito wa kinabii, unaoonya dhidi ya uovu katika jamii bila kujali vyeo ya waamini.

Viongozi wa CCT, wakiongozwa na Askofu Alinikisa Cheyo wa Kanisa la Moravian, walimweleza kuwa suala la kuonana naye halihusiani na nyaraka, na kwamba walikuwa wamejitahidi sana kuomba kuonana naye, akawanyima nafasi.

Maneno ya rais yalimlenga zaidi Askofu Frederick Shoo wa KKKT, kwani rais alieleza bayana kusikitishwa na waraka wa kanisa lake. Kuhusu suala la kuonana naye, Askofu Shoo naye alimweleza rais kuwa kanisa lake limekuwa linajitahidi kukutana naye tangu aingie madarakani lakini hakuwahi kulipa nafasi hiyo.

Rais anyanyapaa wapinzani katika maridhiano ya kitaifa

Katika mjadala huo, Askofu Shoo, bila kupepesa macho, alimsisitizia rais juu ya umuhimu wa maridhiano ya kitaifa.

Alimwambia kuwa amani ya nchi ni tete, na uhusiano kati ya serikali na vyama vingine vya siasa ni mbaya sana; na kwamba njia ya kuondoa hali hiyo ni rais kufanya jitihada za kuonana nao ili kuweka maridhiano ya kitaifa.

Akijibu hoja ya Askofu Shoo, Rais Magufuli alisema yupo tayari kuonana na viongozi wa vyama vya siasa lakini hayupo tayari kuwaita.

Alishauri viongozi wa siasa ndio waombe kuonana naye au viongozi wa makanisa waitishe mkutano wa kuwakutanisha, na yeye atakuwa tayari kukutana nao.

Aomba ushirikiano na TEC “mpya”

Katika mazungumzo ya rais na viongozi wa TEC, rais aliwapongeza viongozi wapya. Aliwaomba wampe ushirikiano wa kueleza Watanzania umuhimu wa kudumisha amani ya nchi.

SAUTI KUBWA halikupata kujua iwapo viongozi hao wa TEC walimweleza rais juu ya umuhimu wa serikali kuzingatia haki kwa wananchi ili kujenga msingi huo wa amani.

Askofu Gervase Nyaisonga aliyekuwa kiongozi wa msafara, naye alimwambia rais umuhimu wa kufungua milango ya maridhiano na makundi mbalimbali ya kijamii kwa sababu ndiyo “wadau wakuu wa amani.

Waislamu wametengwa katika amani

Wakati rais akijibu hoja kuhusu wadau wa amani, alisisitiza bila aibu kuwa yupo tayari kukutana na makundi mbalimbali, hayupo tayari kukutana na makundi ya kidini yenye mlengo wa kigaidi. .

Katika hali isiyotarajiwa, rais alisema hata Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limepoteza mwelekeo wa kuongoza Waislam, na kwamba haoni haja ya kukutana nao.

Chanzo kinamnukuu rais akisema: “Mkiomba kukutana nami kama viongozi wa dini, msiwalete BAKWATA.” Rais hakujadili lolote kuhusu Shura ya Maimamu ambayo ndiyo taasisi kubwa inayoongoza waislamu wengi nchini.

Hisia za rais dhidi ya Waislamu zinarejesha kumbukumbu za mvutano uliomgonganisha rais na Mwigulu Nchemba, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, katika suala la idara ya uhamiaji kuzuia wahubiri wa Kiislamu waliokuwa wamenyimwa kibali cha kufanya kazi yao nchini kwa kisigizio cha ugaidi.

Katika barua ya kutengua zuio la uhamiaji, Nchemba aliandika kwamba “ucha Mungu si ugaidi.” Ndani ya siku tatu rais alimfukuza kazi.

Akihitimisha mazungumzo yake, Rais Magufuli aliwaahidi ushirikiano viongozi hao, kuwa serikali yake itaendelea kushughulikia matatizo yanayokabili mashirikika ya dini ili yaendelee kutoa mchango wake kwa jamii ya Watanzania.

Vyuo, shule na hospitali za kanisa

Maaskofu walitumia fursa hiyo pia kumweleza rais kuwa serikali inaumiza mno taasisi za kidini hasa vyuo vikuu, shule na hospitali za makanisa.

Like
35

Leave a Comment

Your email address will not be published.