Majaji waishauri Chadema: Pokeeni hukumu, ongezeni moto wa katiba mpya

BAADA ya uamuzi wa Jaji Kiongozi Mustafa Siyami unaolalamikiwa katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya Freeman Mbowe na wenzake wanaotuhumiwa ugaidi, nimezungumza na viongozi kadhaa wakiwemo majaji na wanasheria wakuu wastaafu, kwa nyakati mbalimbali, na wote wanashangaa uamuzi huo, lakini wanasisitiza kuwa, hata hivyo, waliutarajia.

Wawili wametoa kauli zinazofanana ambazo nikiziweka katika maneno yangu mwenyewe zinakuwa hivi: “Chadema wasikubali lakini wapokee hukumu, na waendelee kudai katiba mpya.”

Sitataja majina yao hapa, lakini naweza kusema kwa uhakika kuwa wote wamezungumza kwa uchungu. Mmoja wao akasisitiza: “Hukumu hii ya Jaji Kiongozi katika kesi ndogo ni kielelezo kuwa madai ya katiba mpya yana uhalali na umuhimu mkubwa sasa.”

Hukumu hiyo imeibua hisia kali miongoni mwa jumuiya za wanasheria, wanaharakati, jumuiya ya kimataifa na makundi ya wanaCCM wanaopenda haki.

Mmoja wa wanasheria wakuu wastaafu amehusisha hukumu ya Jaji Siyami na uteuzi wake kuwa Jaji Kiongozi. Anasema: “Hata huko nyuma, uteuzi wa majaji umekuwa hivi lakini tulikuwa na marais waadilifu na majaji waadilifu. Marais waliteua na kuishia hapo, hawakuingilia kazi za majaji. Majaji pia walikuwa na maadili na misimamo ya kutokubali kuingiliwa. Lakini hivi sasa majaji wanaingiliwa kiasi cha kutisha.”

Mwingine, ambaye ni jaji, amesema: “Ni vema uteuaji na usimamizi wa majaji viwekwe nje ya mikono ya marais”.

Kimsingi, haingii akilini, Rais Samia Suluhu (Mwenyekiti wa CCM) kupitia DPP amkamate na kumfungulia mashtaka Mbowe
(Mwenyekiti wa CHADEMA), kisha Samia huyo huyo Mwenyekiti wa CCM amteue Jaji Siyami kuwa jaji, na jaji aende kusikiliza kesi kati ya Samia na Mbowe na utarajie Jaji Siyami atende haki.

La ajabu ni kwamba Jaji Siyami, wakati akiwa katikati ya kusikiliza kesi kati ya Samia na Mbowe, Rais Samia akamteua Siyami kuwa Jaji Kiongozi.

Na katika kumwapisha, katikati ya usikilizwaji wa kesi, Jaji Siyami akasema: “nitakuwa mtiifu kwa Rais Samia na daima nitatunza siri zote nitakazojua au kuambiwa na Rais Samia!”

Kana kwamba hiyo haitoshi, Jaji Mkuu akasimama na kumwambia Jaji Siyami mbele ya kadamnasi kuwa mahakama ni sehemu ya jamii, kwa hiyo Jaji Siyami anatakiwa awe sehemu ya jamii inayoheshimu uamuzi na matakwa ya rais. Hii ni kama kumwambia Jaji Siyami kuwa asijifanye mjuzi kusimamia kisichosimamiwa na rais aliyemteua.

Katika mazingira haya, ili Jaji Siyami aweze kutoa haki sawa katika kesi inayomhusisha Rais Samia (mteuaji) yanahitajika mambo mawili.

Kwanza, Jaji Siyami asiwe mwanadamu na asiweze kuwa Mungu kama alivyowahi kusema Askofu Benson Bagonza. Ni mateso kwake kutokuwa mwanadamu na kutokuwa Mungu.

Pili, inabidi Jaji Siyami apate mateso kuliko ya Adamoo ili akubali kuwa aliwahi kuambiwa na Rais Samia kwamba lazima amfunge Mbowe. Jaji Siyami, katika uamuzi wake, si tu kwamba amebariki mateso ya watuhumiwa bali pia ameonyesha kutoamini kuwa mateso huwa yapo.

Anafanya kosa walilofanya majaji wa Uganda kabla ya Idd Amin. Nao walikuwa kama Jaji Siyami. Walikuja kujifunza kwa tabu kupitia mateso waliyoyapata mikononi mwa Idi Amin pale walipoamua kesi kinyume na matakwa ya serikali. Jaji Kanyeihamba amesimulia mambo haya katika kitabu chake. Idi Amini aliwakamata kwa mikono yake, akawatesa na kuwaua.

Uamuzi mdogo wa kesi hii unaweka historia chafu katika utawala wa sheria Tanzania, lakini kibaya zaidi ni kwamba unazifanya hata hukumu zinazokwenda kinyume cha matakwa ya serikali zionekane ni mzaha.

Mgongano huu wa maslahi unaoukabili utawala wa sheria Tanzania unaonekana wazi sasa kwa sababu kesi nyingi ni za kisiasa. Kwa watoa haki wanaoteuliwa na wanasiasa, ni vigumu kutatua hili bila kupata katiba mpya itakayoondoa mgongano huu.

Huko nyuma, mgongano ulikuwa unavumilika kwa sababu kesi nyingi zilikuwa ni za madai au jinai ndogo ndogo. Hizi kesi za sasa ni hatari kwa sababu zinahusu maslahi ya rais na chama chake, wabunge na madiwani wake.

Kibaya zaidi, madai ya katiba mpya yanatishia hata nafasi za majaji kwa sababu wengi wa majaji tulionao yawezekana wasingepata ujaji kama wangekuwa wanapitia katika mchakato wa wazi na usio wa kisiasa.

Kimsingi, Siyami amejichafua yeye na mahakama anayoiongoza, na amechochea upya madai ya katiba mpya.

Hadi sasa, wanaodai katiba mpya ni wengi kuliko wanaoipinga. Wapo ndani ya vyama vyote vya siasa, katika makundi mbalimbali ya kijamii na hata serikalini.

Wanaotazama mbali, wanaolitakia taifa usitawi huko tuendako, wanaona umuhimu wa katiba mpya. Hii ni ajenda isiyokufa, isiyoweza kumwacha salama rais yeyote anayeipinga – labda tu kama anajifariji kwa muda.

Like
32