Mahakama zaamuru Musiba awalipe Prof. Tibaijuka, Fatma Karume bilioni 8 kwa kuwakashifu.

MAHAKAMA nchini Tanzania zimemuamuru Cyprian Musiba, ambaye amekuwa anajiita “mwanaharakati huru,” kulipa fidia ya Shilingi bilioni 7.58 baada ya kumkuta na hatia ya kukashfu, kudhalilisha na kusema uongo dhidi ya watu akitumia “gazeti lake.”

Waliomshtaki na kupewa ushindi na mahakama dhidi yake ni Prof. Anna Tibaijuka, waziri wa zamani wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, na Fatma Karume, rais mstaafu wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).

Musiba mwenyewe amenukuliwa akiwa analialia kuwa anaumwa, bila kueleza nini kinamsumbua, akisema – “sina hata shilingi mia, na wakitaka wanaweza kunifanya lolote, siogopi, mimi nilifanya kazi kuitumikia Tanzania nchi yangu ninayoipenda sana na nilikuwa naipigania dhidi ya mabeberu.”

Kiasi hicho cha fedha kinatosha kujenga barabara kilomita nane kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa kilomita moja ni Sh. bilioni moja.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ilimuamuru Musiba kulipa Sh. milioni 80 kwa Prof. Tibaijuka baada ya kuridhika kwamba alikashfiwa na kudhalilishwa na mshitakiwa kupitia gazeti lake la Tanzanite. Nakala ya hukumu hiyo ilitolewa Julai 16, 2021.

Gazeti hilo toleo namba 30 la Oktoba 30, 2017, lililowasilishwa mahakamani kama ushahidi, liliandika “Pigo jingine kwa Prof. Tibaijuka,” likimuhusisha na kashfa kadhaa ambazo mlalamikaji alisema ni za uongo na kuthibitishwa na mahakama, hivyo kamuamuru mshitakiwa kulipa fidia ya Sh. milioni 80.

Gazeti hilo lilimhusisha Prof. Tibaijuka na madai mengine ya kampuni ya bima ya Milembe, inayomilikiwa na mtoto wake, Muganyizi Karumuna Tibaijuka – kwamba ilishindwa kumlipa fidia mmoja wa wateja wake wa madai ya bima, tuhuma ambazo mahakama ilithibitisha kuwa ni uongo.

Mahakama hiyo pia iliamuru gazeti la Tanzanite kutoandika lolote linalomuhusu Prof. Tibaijuka, mtoto wake – Muganyizi na kampuni ya bima ya Milembe.

Sambamba na hukumu hiyo, Mahakama Kuu Zanzibar, iliyoko eneo la Vuga jana iliamuru Musiba kumlipa Fatma Karume jumla ya Sh. bilioni 7.5.

Mahakama Kuu Zanzibar ilijiridhisha kwamba Musiba kupitia gazeti lake la Tanzanite, alimkashfu Fatma Karume kwa kuandika uongo juu yake.

Gazeti lake la Tanzanite, liliandika “Fatma Karume apewa mimba na muuza unga,” habari ambayo mahakama ilithibitisha kwamba haikuwa kweli na kukubaliana na mshtaki kuwa ilikuwa na lengo la kumkashfu na kumdhalilisha.

Kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2019, iliyoitwa mara a kwanza Oktoba 3, 2019, iliendeshwa bila Musiba kufika mahakamani – bila maelezo wala taarifa kwa Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Baada ya hukumu hiyo, wakili Fatma Karume aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akiutaarifu umma juu ya uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Zanzibar na kuhimiza watu “kumtafuta alipo Musiba kumwambia kuhusu hatua hiyo ya chombo hicho cha haki.

Kuhusu namna atakavyotumia fedha hizo za fidia akilipwa na Musiba, Fatma Karume alisema akizipata atazitumia kwa manufaa ya umma.

“Hata nikipata shilingi milioni moja nitatumia kuanzisha Mfuko wa Shangazi (Shangazi Fund) ili kusomesha watoto waliopewa mimba na baadaye kufukuzwa shule kutokana na sera zenye uonevu na ubaguzi za aliyekuwa kiongozi wa Tanzania, Rais John Magufuli a serikal yake dhalimu,”aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter leo.

Profesa Tibaijuka alijibu kwa kifupi, “sina la kusema.”

SAUTI KUBWA ilimtafuta Musiba kujua ni lini atalipa fedha hizo baada ya mahakama kuamuru afanye hivyo kwa Fatma Karume na Prof. Tibaijuka, alisema “mimi sina pesa, wakitaka waniue.”

Musiba na gazeti lake la Tanzanite, alikuwa akijitanabaisha kuwa mtetezi wa Rais John Magufuli na aliwahi kutamka kwamba yuko tayari kufa ili “kumlinda.”

Huku akijiita “mwanaharakati  huru,” Musiba alifanya kazi kubwa ya “kuchafua” watu wengi – hasa waliokuwa wakipingana na sera na aina ya uongozi wa Rais Magufuli, akawapachika majina na sifa za hovyo; ikiwamo ugaidi, uhaini, usagaji na ushoga, ubakaji, na kadhalika, madai ambayo hajaweza kuthibitisha popote hadi sasa.

Pamoja na Musiba kuandika uongo, kudhalilisha na kukashifu wengine, serikali kupitia Idara ya Habari – MAELEZO, vyombo vya ulinzi na usalama, ilimkingia kifua. Hakuchukuliwa hatua yoyote kama ambavyo ilikuwa ikifanywa na vyombo hivyo kwa magazeti mengine.

Pamoja na hukumu mbili hizo, Musiba na gazeti lake la Tanzanite, anasubiri hukumu nyingine kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo anashitakiwa na Bernard Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwa kumkashifu.

Naye Erick Kabendera, mwandishi wa habari wa kujitegemea, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa atamfungulia kesi Musiba kwa kumkashifu. Orodha ya watu waathirika wa kashfa za Musiba ni ndefu.

Like