SERIKALI imetumia ajali ya kivuko Mv Nyerere kama kisingizio cha Rais John Magufuli kutohudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika Marekani siku chache zilizopita, lakini rais mwenyewe amejisahau na kutibua mambo.
Rais alimtuma Balozi Augustine Mahiga amwakilishe katika mkutano huo ukiohudhuriwa na wakuu wa nchi duniani. Mahiga ni waziri anayehusika na mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, lakini huu ni mkutano wa marais, si wa mawaziri.
Akihutubia mkutano huo kwa niaba ya rais, kwa hotuba iliyoandikwa, Balozi Mahiga alisema kuwa Rais Magufuli alishindwa kujumuika na marais wenzake katika mkutano huo muhimu kwa sababu ya ajali ya kivuko cha Mv Nyerere kilichoua watu zaidi ya 200 katika Ziwa Victoria.
Hadi leo Oktoba 2, 2018, Rais Magufuli hajawahi kwenda Ukerewe au Ukara kuhani msiba huo. Hata siku ya mazishi kitaifa ya miili ambayo haikutambuliwa na ndugu, tarehe 23 Septemba 2018, rais alikuwa Ikulu akinywa chai na maofisa wa polisi wa barabarani, jambo lililozua minong’ono na mshangao katika jamii.
Jioni yake muda wa saa 10 msafara wa rais ulionekana ukielekea maeneo ya Salasala, Tegeta, Dar es Salaam katika kile kinachoonekana yalikuwa matembezi binafsi.
Wakati Balozi Mahiga anaiambia dunia kuwa ajali hiyo ndiyo ilisababisha rais asiende Marekani, rais mwenyewe amesema hadharani kuwa hakwenda ili kuokoa pesa ya safari.
Anakiri kwamba katika ziara hiyo alimtuma Balozi Mahiga na msaidizi wake tu, na kwamba iwapo angeenda yeye kungekuwa na msafara mkubwa sana.
USHAHIDI: Katika video hii, kuna kauli mbili zinazopingana – ya Balozi Mahiga na ya Rais Magufuli.
Inapatikana pia katika https://youtu.be/qpI-A-duI60
Hii si mara ya kwanza Rais Magufuli kukwepa vikao vya kimataifa vinavyomhusu.
Kwa miaka mitatu sasa tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa anatafuta visingizio vya kutohudhuria mikutano hii, huku akituma wawakilishi. Mara kadhaa amekuwa anamtuma makamu wa rais – jambo linaloua hoja yake ya kuokoa fedha.
SAUTI KUBWA haina kumbukumbu ya mikutano ya kimataifa ambayo Rais Magufuli ameshiriki tangu alipoingia madarakani.
Mwaka 2017, rais alikwepa kikao cha Umoja wa Afrika kilichofanyika Zambia akisingizia tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.
Hata hivyo, rais hakwenda Bukoba kufariji wafiwa na manusura wa tetemeko, hadi baada ya miezi minne kupita.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia hawakubaliani na sababu za rais kukwepa vikao hivyo.
Ingawa yeye anatumia kigezo cha “kuokoa fedha” kama kinga, wataalamu hawa wanasema hoja hiyo ingekuwa na nguvu iwapo zingekuwa ziara binafsi za rais.
“Hivi ni vikao vya lazima kwa rais kushiriki. Ni fursa adhimu ya rais kukutana na marais wenzake, kubadilisha maoni na uzoefu, kujitambulisha na kusaka fursa nyingine za kimaendeleo kwa ajili ya nchi yake. Visingizio anavyotoa, havina mashiko,” alisema mtaalamu wa siasa za kimataifa anayefanya kazi serikali.
Mchambuzi mwingine ameiambia SAUTI KUBWA kuwa sababu zinazotolewa na rais na wasaidizi wake zinaakisi udhaifu mwingine.
“Kuna tatizo, si bure. Rais wetu hajiamini katika nyanja za kimataifa. Anajua haya mambo ya kiswahili swahili ya kufoka foka. Kule nje anakosa confidence (hajiamini); na sasa ana hofu na aibu kwa sababu ya baadhi ya matukio mabaya yanayogubika utawala wake kwa miaka mitatu mfululizo.
“Anaogopa akienda nje atakutana na waandishi wa habari wa kimataifa watakaomhoji kuhusu mauaji, ukatili wa serikali yake dhidi ya wakosoaji, wapinzani, wanaharakati na waandishi wa habari.
“Hana uwezo wa kujieleza vizuri kwa Kiingereza, lakini pia anajua dunia itamzomea, kwani hata wawekezaji wa nje wananyanyaswa, na hizi sheria mbovu ambazo serikali yake inatunga hadi wahisani na wakopeshaji wetu wanaanza kushtuka ni baadhi ya mambo ambayo yanamnyima amani ya kusafiri nje. Haya maelezo mengine ni kudanganyana kama watoto,” alisema mchambuzi huyo kwa sharti la kutotajwa jina.