Magufuli aondoka na watu 45 Dar es Salaam

MAOMBOLEZO ya msiba wa Rais Dk. John Pombe Magufuli yameua watu 45 ambao walikanyagwa na umati, huku wengine wakikosa pumzi wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo.

Tukio hilo la aina yake limetokea jana, Machi 21, 2021 siku ya pili ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Magufuli, katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya maandishi iliyovuja kutoka Ofisi ya Upelelezi (RCO) wa Mkoa wa Kipolisi Temeke asubuhi leo Machi 22, 2021 ilisema vifo hivyo vilitokana na msongamano, kukanyagana na kukandamizana wakati umati mkubwa wa watu ulipokuwa unakwenda kuaga mwili wa hayati Rais Magufuli.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa katika idadi hiyo wamo wanaume 11 na miongoni mwao, watu wazima ni 6 na watoto 5. Baadhi yao tumechapisha picha zao hapa.

Ilisema vifo vya wanawake ni 34 na kati yao watoto ni 2 na watu wazima 32.

Aidha taarifa hiyo ya RCO kwenda kwa uongozi wa juu wa polisi ilisema majeruhi 32 wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke na 6 kati yao hali zao ni mbaya na wamepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

“Tutoe angalizo kwa mikoa ya Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Geita ambako mwili wa hayati Rais Magufuli utapita wachukue tahadhali mapema kwani watu ni wengi na wanalazimisha kutaka kuaga mwili,” ilisema taarifa hiyo ya RCO wa Temeke.

Familia moja yapoteza watu 5

Kwa mshtuko mkubwa familia ya Mbasa Mtuwa ya Kimara Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam imepoteza watu 5 wakiwemo watoto kutokana na kukanyagwa vibaya wakati wakiaga mwili wa hayati Magufuli.

Mmoja wa marafiki wa familia hiyo ambaye hakufahamika jina lake alisikika akisema, “Mbasa Mtuwa amepoteza mtoto wake, mtoto wa kaka yake, watoto 3 wa mdogo wake pamoja na mke wa mdogo wake…hii familia inahitaji maombi na faraja,” alisema.

Mwingine aliandika: “Hawa ni watoto wa shemeji yangu na wadogo zangu Alan na Harry Mtua. Ni kweli tumefiwa na watu 5 katika familia yetu, Kimara! Mtoto moja wa shemeji yangu, watoto wawili wa mdogo take Alan poja na mke wake na mtoto moja wa Alan (Aliyevaa uniform) walienda na mama yao Uwanja wa Taifa kuanga mwili wa Hayati Rais Dkt. JPM hawakurudi! Tumepokea taarifa hizo jioni saa 9 hivi. Tumefanikiwa kutambua wote kasoro dada wa kazi ambaye alikuwa pamoja nao. So far Gari imepatikana ilikuwa bado ipo kwenye parking za uwanja wa Taifa. Kesho tutaendelea kumtafuta dada wa kazi.”

Taarifa zilizosambaa mitandaoni kuanzia jioni jana, zilimtaja Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Mgeule Kata ya Buyuni, wilayani Ilala Dar es Salaam, Jeni Mgonde, ni miongoni mwa waliofariki duniani kutokana na msongamano wa watu wakati wa kuaga mwili wa hayati Rais Magufuli.

Mabadiliko kuaga mwili Dodoma

Kufuatia vifo vilivyotokea Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, leo Machi 22, 2021 amesema ratiba ya kuaga mwili imebadilishwa.

Amesema katika Uwanja wa Jamhuri watu wachache wataruhusiwa kuaga mwili, kisha mwili huo utatolewa na kupitishwa kwenye mitaa mbalimbali jijini humo ili kutoa fursa kwa watu wengi kushiriki msiba huo.

Like
2