Lissu apanda mtumbwi kwenda Ukerewe baada ya kunyimwa pantoni

TUNDU Lissu, mgombea urais kupitia CHADEMA, jana Jumatano alilazimika kupanda mtumbwi wa wavuvi kutoka Kisorya hadi Ukerewe baada ya mamlaka kuzuia pantoni, kwa madai kuwa ni mbovu, ili ashindwe kufanya kampeni kisiwani humo.

Hii ni mara ya pili kwa Lissu kufanyiwa visa hivyo. Wiki tatu zilizopita, mamlaka ziliamuru kivuko kilichokuwa Kisorya kiondoke alfajiri mapema kabla ya muda wake, kabla yeye na msafara wake hawajafika, ili washindwe kwenda Ukerewe. Ziara yake iliahirishwa.

Jana, ilidaiwa kuwa kivuko ni kibovu, hivyo kisingeweza kwenda Ukerewe. Ndipo akapanda boti ndigo za wavuvi hadi Ukerewe na kufanya mkutano mkubwa wa hadhara.

Akiwa Ukerewe, wananchi walimweleza kuwa hizo ni hujuma zinazoongozwa na mkuu wa wilaya ya Ukerewe. Lissu alisema kuwa wakuu wa wilaya hawaruhusiwi kujihusisha na kampeni za uchaguzi, na kwamba wanapofanya hivyo wanakuwa wahalifu kama wengine, hivyo wanapaswa kushughulikiwa. Alisema hujuma za dola dhidi yake hazitafanikiwa.

Katika hali ya kushangaza tena, pantoni nyingine iliyokuwa upande wa Ukerewe nayo iliondoka muda mfupi kabla Lissu hajamaliza hotuba yake, kwa shabaha kuwa ashindwe kusafiri nayo hadi Kisorya.

Ilipofika Kisorya, ilishindwa kushusha mizigo wala abiria kwa kuwa katika njia ya mizigo na abiria kulikuwa na magari ya msafara wa Lissu, na madereva wa Lissu ndio waliokuwa na funguo za magari hayo, na walikuwa Ukerewe. Lissu alirejea Kisorya baadaye kwa mtumbwi uliompeleka.

Baada ya kutoka Ukerewe alielekea Jimbo la Rorya mkoani Mara akawambia maelfu ya wananchi waliokuwa kwenye viwanja vya Shirati kuwa uchaguzi mkuu huu ni muhimu kwa sababu ndiyo unakwenda kuamua hatima ya maisha yao. Alisema:

“Watu wa Rorya mmekuwa mkinyanyaswa na mifugo yenu, mnatozwa msururu wa kodi kuanzia zizini mpaka mnapotaka kuuza mifugo yenu. Kabla hapo hakukuwa na msururu huo wa kodi. Ni nani ana mamlaka yakutoza kodi zisizo na kichwa wala miguu? Chadema ilani yetu inasimamia uhuru, haki na maendeleo ya watu. Tutaleta haki kwa wananchi.

“Watu wa Rorya nawaomba dhamana yakuongoza nchi hii ili nikabadilishe mfumo wa uongozi, niwe raisi wa katiba mpya. Nitakuwa raisi wa katiba mpya, nitakuwa raisi ninaye fariji watu. Sitakula rambi rambi kama yule jamaa. Sasa watu wa Rorya tarehe 28 tukapige kura kwa ajili ya katiba mpya itakayorudisha mamlaka kwa wananchi.

“Chadema ikiingia madarakani itaondoa changamoto zote zinazowanyima haki watu wa Rorya. Itaondoa vitambulisho vya Magufuli, itapandisha mishahara kwa watumishi wa umma ambao miaka mitano hawajapewaa stahiki zao. Chadema itatenda haki kwa kila mwananchi.

“Chadema tukipata serikali mwaka huu itabadilisha mfumo wa elimu. Tunataka watoto na vijana watakaopata maarifa yatakayowafanya waajirike. Mfumo utawawezesha vijana kuajirika popote duniani. Na tutahakikisha tunafungua mipaka kwa wananchi kwenda mahali popote kutafuta ajira. Chadema itahakikisha vijana wanapata ujuzi ambao watautumia kuzalisha mali.

“Chadema ikichukua nchi italeta bima ya afya kwa watu wote, kila  mkazi wa Tanzania atakuwa na bima ya afya. Gharama za bima zitakuwa chini, watu watapata huduma bora za Afya. Na kutakuwa na upatikanaji wa dawa na vituo vingi vya afya. Chadema inataka taifa lenye afya; na siku zote taifa lenye afya hata uzalishaji mali unakuwa wenye tija.

“Watu wa Rorya tarehe 28 mkapige kura ya haki kuchagua viongozi wa Chadema, mkapige kura ya maisha yenu, mpige kura kwa wingi mpaka washindwe kuiba. Kura ya kwanza pigieni kura madiwani wote wa Chadema tuchukue Halmashauri; kura ya pili pigieni mbunge wenu Ezekiel Wenje na kura ya tatu ni kwangu Tundu Lissu, yule wasiyempenda kaja.

“Japo leo walinizuia kwenda Ukerewe kwa Kuzuia pantoni, nikapanda mtumbwi, huyo niko Ukerewe. Sasa Naomba mnichague nikawe raisi atakayewafariji na kuwaongoza kwenye haki na maendeleo yenu.”

Like