Maaskofu wamuasa Rais Samia kuhusu haki na ustawi

MAASKOFU wa makanisa mbalimbali Tanzania wamempa ushauri Rais Samia Suluhu Hassan juu ya namna nzuri ya kuongoza nchi kwa haki na ustawi.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam wa Kanisa Katiloki, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa’ichi, Jumamosi iliyopita alisema kazi ya urais si ndogo, ni jukumu zito ambalo linambebesha wajibu wa kuwahudumia kwa usawa raia wote.

“Najua kuwa Mama Samia alishirikiana kwa karibu na Magufuli wakati akiwa makamu wake wa rais, hivyo hatuna wasiwasi kuwa anaielewa nchi, anaifahamu na anajua vipaumbele vyake hivyo ataviendeleza kwa juhudi,  yale yote mema ambayo yalikuwa yakishughulikiwa na Magufuli.”

“Lakini kwa sababu nimesema jukumu la kuongoza nchi ni jukumu zito, nawaalikeni wote tumuweke katika sala, tumpe ushirikiano na kushikamana naye katika kutafuta ustawi na maendeleo ya kila raia wa nchi hii,” alisema Ruwa’ichi.

Samia aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania kufuatia kifo cha John Magufuli, aliyekuwa mtangulizi wake. Alifariki Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama, Dar es Salaam.

(Askofu Bagonza)

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza, amemshauri Samia kuiogopa na kutetemekea nafasi hiyo “kama sisi raia tunavyomuogopa na kumtetemekea mtu aitwaye rais.”

“Rais asiyeuogopa urais ni hatari kwa nchi na kwake mwenyewe binafsi. Rais asiyeuogopa urais lakini anataka aogopwe, ni hatari na msiba usiokwisha kwa Taifa lolote,” alisema askofu huyo.

Askofu Bagonza alimshauri Rais Samia “kuwapumzisha kazi” wote wenye hulka na rekodi ya kukanyaga sheria na katiba kwa kisingizio cha uzalendo.

“Hawa watu ni hatari kwa rais kuliko walivyo hatari kwa nchi. Rais wetu aimbe wimbo wa haki tu ili kuondoa kila chembe ya ubaguzi,” aliongeza Askofu Bagonza.

Aliwashauri wasaidizi wa Rais Samia kumsaidia kufanya kazi zake salama na kwa mamlaka ambayo hayaonei mtu yeyote.

Askofu Emmaus Mwamakula, Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania na Afrika Mashariki ,amemshauri Rais Samia kusikiliza maoni ya makundi mbalimbali nchini yanayodai Katiba mpya na kujenga mazingira ya kuanza upya kwa mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya ili Uchaguzi Mkuu ujao ufanyike kwa haki na salama.

Mwamakula ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani, amemshauri Rais Samia kuacha vyombo vya habari kufanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na vyombo vya dola.

Askofu huyo anasema ni vyema uongozi wa Rais Samia uangalie namna ya kurekebisha mazingira ya wafanyabiashara ili wasinyanyaswe wala kutishwa na maofisa wa serikali.

“Tunashauri utawala mpya ufungue majadiliano na maridhiano na viongozi wa vyama vya upinzani kuhusu malalamiko yao na kuwapa nafasi ya kufanya kazi zao za siasa kwa uhuru,” aliongeza askofu huyo.

Askofu Mwamakula
Like
2