Lissu ajibu propaganda za Magufuli na vijigazeti vyake

SIKU moja baada ya kutoka hospitalini, na baada ya kushuhudia propaganda zinazosambazwa na kikosi cha wapambe wa Rais John Magufuli kupitia vijarida vyao, wakijaribu kumsafisha rais na kashfa ya shambulizi la risasi dhidi yake Septemba 7 2017, Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki, ametoa kauli nzito kukemea propaganda hizo na kuweka kumbukumbu sahihi. Andiko lake limechapishwa hapa chini:

KAZI YA GAZETI LA HOJA SASA IMERITHIWA NA JAMVI LA HABARI, TANZANITE

Kabla ya mwaka 2005, wakati CHADEMA ilipokuwa chama kidogo na dhaifu, hakuna watu wa ‘mfumo’ waliokuwa wanahangaika nacho. Adui nambari wani wa CCM na ‘mfumo’ wakati huo alikuwa Augustine Lyatonga Mrema na NCCR-Mageuzi (1995-2000); na Profesa Ibrahim Lipumba na CUF (2000-2005). Tuhuma za ‘Uchagga’ zilikuwa za Mrema, na za Uislamu wa siasa kali zilikuwa za Lipumba. Kwa wenye umri kama wa kwangu mtamkumbuka IGP Omari Mahita na kontena la visu na majambia yaliyofungwa bendera za CUF.

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, CHADEMA mgombea Urais kwa mara ya kwanza, Mwenyekiti Freeman Mbowe. Pamoja na kushika nafasi ya tatu kwenye Uchaguzi huo, CHADEMA ilijitokeza kuwa Chama kikuu cha upinzani kwa upande wa Tanganyika, na idadi ya Wabunge wake iliongezeka kutoka watano wa mwaka 2000 hadi 11.

Mara CHADEMA ikageuzwa na ‘mfumo’ kuwa adui nambari wani wa CCM. Na tuhuma za ‘Uchagga’ zikahamishwa kutoka kwa Mrema na NCCR-Mageuzi na kuelekezwa kwa Mbowe na CHADEMA.

Baadae mwaka 2008 marehemu Chacha Zakayo Wangwe alipofariki kwenye ajali ya gari Dodoma, watu wa ‘mfumo’ wakaongeza na tuhuma ya kifo cha Chacha Wangwe dhidi ya Mbowe na CHADEMA.

Kazi kubwa ya kusambaza tuhuma hizi za uongo na upuuzi mtupu zilifanywa na kigazeti kiitwacho Hoja. Kwa miaka mitano mfululizo kati ya 2005 na 2010, hakuna story ya ‘fenti fodi’ ya kigazeti hicho ambayo haikumtaja Mwenyekiti Mbowe kwa tuhuma hii au ile, kwa uzushi huu au ule.

Kupita nyingine zote, uzushi mkubwa ulikuwa Uchagga na kifo cha marehemu Chacha Wangwe.

Wananchi wa Tanzania walijibu tuhuma na uzushi huo kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Kwenye Uchaguzi huo, CHADEMA ilipata wabunge wengi zaidi kutoka Kanda ya Ziwa kuliko Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Wachagga wa Mwenyekiti Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa.

Ukiachia Kanda ya Kusini, Kanda nyingine zote zilipata Wabunge wa majimbo wa CHADEMA.

Baada ya majibu hayo ya wapiga kura, tuhuma za ‘Uchagga’ na kifo cha Chacha Wangwe zilififia sana; na kigazeti cha Hoja kilichokuwa kinazisambaza nacho kilitoweka.

Fast forward to Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na mafanikio makubwa ya CHADEMA na UKAWA, vita dhidi ya Mbowe na CHADEMA imepamba moto tena.

Na sasa nafasi ya kigazeti cha Hoja imechukuliwa na vijigazeti vya Jamvi la Habari na Tanzanite.

Lakini anayezushiwa hajabadilika, ni Mwenyekiti Mbowe. Alikuwa ndiye aliyemuua Chacha Wangwe; sasa ndiye alimshambulia Tundu Lissu kwa risasi.

Ilikuwa Chacha aliuawa kwa sababu alikuwa anataka kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA. Sasa ni Lissu ameshambuliwa kwa risasi naye anataka kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA.

Ni uzushi mtupu. Ni upuuzi mtupu. Mimi sijawahi kutaka kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA. Sijawahi kutangaza popote au kuambia mtu yeyote kuwa nataka kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA.

Sijawahi kukutana na mbunge yeyote wa CHADEMA, iwe nyumbani kwangu, au hoteli ya African Dreams, au mahali popote pale, ili kuwaeleza kuwa nataka kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA.

Sikushambuliwa kwa risasi kwa sababu ya kutaka kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA. Ingekuwa hivyo, Magufuli na watu wake wangeshangilia sana na wasingeninyima stahiki zangu za kisheria za kutibiwa na Bunge.

Nilishambuliwa kwa sababu ya upinzani wangu kwa Rais Magufuli na matendo yake.

Nilikuwa kiongozi wa kwanza, mwezi December 2015 na January 2016 kusema hadharani kwenye Mlimani TV na Channel Ten kwamba Magufuli ni tishio kubwa kwa haki za binadamu, utawala wa sheria na demokrasia.

Mtakumbuka nilimwita Magufuli kuwa ni muunganiko katika mwili mmoja wa Lyatonga Mrema na marehemu Edward Sokoine. Hizo clip zipo mtandaoni hadi sasa.

Baada ya hapo mwaka 2016 karibu wote niliutumia kwenye Kituo cha Polisi cha Central na mahakamani Kisutu, nikikamatwa kwa kauli hii au ile kuhusu Magufuli na utawala wake.

Mwaka 2017 ulianza kwa ugomvi wa Urais wa TLS. Mnayakumbuka maneno ya Magufuli mbele ya majaji na mawakili Siku ya Sheria, February 2017. Mnakumbuka wa Waziri wa Katiba na Sheria Dr. Mwakyembe baada ya mimi kujitokeza kugombea Urais wa TLS.

Magufuli alipokamata makinikia nilijitokeza hadharani na kutamka anadanganya Watanzania kwa makinikia kwa 95% ya dhahabu inakwenda kwa kupitia viwanja vya ndege vilivyoko migodini.

Maprofesa wa Magufuli, Mruma na Osoro, walipotoa ile ‘professorial rubbish’ ya shilingi trilioni 495 nilikuwa wa kwanza kusimama Bungeni na kuiita hivyo: professorial rubbish!!!

Nilipotangaza hadharani kwamba Bombardier ya Magufuli imekamatwa nchini Canada kutokana na madeni ya kesi iliyosababishwa na Magufuli, hazikupita wiki tatu nikamiminiwa risasi nyumbani kwangu Dodoma.

Walinzi wote, hata askari polisi anayelinda kwa Naibu Spika Tulia, waliondolewa kwenye maeneo yote ya Area D. Hawakuondolewa na Mbowe, waliondolewa na watu waliotumwa na Magufuli na watu wake kuja kuniua.

Na nimeambiwa na watu wa humo humo ndani ya ‘mfumo’ kwamba Magufuli aliwaagiza Mawaziri Mwigulu Nchemba na Augustine Mahiga wakanushe kuhusika kwa Serikali yake.

Na nimeambiwa na watu hao hao kwamba maagizo ya Magufuli yalikuwa nikifariki dunia nikimbizwe Ikungi kuzikwa kwa haraka na kusiwepo shughuli yoyote ya kibunge kuuaga mwili wangu Bungeni Dodoma au Karimjee Hall Dar kama zilivyo taratibu za Bunge.

Sikufa na mipango ya waovu hawa haikuwezekana. Mwenyekiti Mbowe alisisitiza nipelekwe Nairobi Hospital badala ya Muhimbili.

Viongozi waliokuwepo – Spika Ndugai, Naibu Spika Tulia, Katibu wa Bunge Tom Kashililah, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Ulisubisya Mpoki, Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba, n.k., walipokubaliana na hilo ndio nikapakiwa kwenye ndege saa sita usiku na kupelekwa Nairobi.

Nilisindikizwa na daktari kutoka Dodoma General Hospital hadi Nairobi Hospital. Mwenyekiti Mbowe alikaa Nairobi zaidi ya mwezi mmoja wakati natibiwa.

Nilitembelewa na viongozi wa kisiasa na kidini wa Kenya na Tanzania; mabalozi wa nchi za nje; wabunge wa vyama vya upinzani na maelfu ya wananchi wa Tanzania na nje ya Tanzania. Hata Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi alikuja kuniona hospitalini.

Ukiachia Makamu wa Rais Mama Samia Suluh Hassan aliyekuja hospital akitokea kwenye sherehe za kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta, hakuna mbunge wa CCM au kiongozi wa Serikali ya Magufuli aliyekuja kunitembelea au hata kunitumia salamu za pole. Wanasema walikatazwa na Magufuli na watu wake.

Walipojua sitakufa kwa risasi zao, wakaamua kuninyima stahili zangu za matibabu. Spika Ndugai ametangaza mwenyewe ndani ya Ukumbi wa Bunge kwamba Bunge halijanitibu kwa sababu Rais Magufuli amekataa kuidhinisha malipo ya matibabu yangu. Hakuna hata ile aibu tu ya kufunika funika ili ubaya wao usionekane hadharani.

Sasa, kwa kutumia vijigazeti vyao Jamvi la Habari na Tanzanite, wanajaribu kufanya kile kilichowashinda kwa kutumia kijigazeti cha Hoja: kumchafua Mwenyekiti Mbowe kwa uzushi huu wa kijinga. Watanzania wanajua na wanawaona. Dunia inajua na inawaangalia.

Mwanafasihi Shafi Adam Shafi alisema katika kitabu chake cha ‘Kuli’: “Yana mwisho haya”!!!! Haya ya Magufuli na watu wake na vijigazeti vyao vya sasa yatakuwa na mwisho. Ukweli utaanikwa hadharani siku moja. Na haki itapatikana.

Like
12

Leave a Comment

Your email address will not be published.