Kwanini ‘Jaji wa Kimkakati’ Elinaza Luvanda anasikiliza kesi ya Mbowe?

JUZI Jaji Elinaza Luvanda alitupilia mbali pingamizi la awali ambalo lilikuwa limewekwa na mawakili wa upande wa utetezi katika kesi inayomkabili Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema.

Uamuzi wa Jaji Luvanda umesababisha baadhi ya watu kutaka kumjua yeye ni nani, na imekuwaje akawa msimamizi wa Mahakama Kuu Division ya Uhujumu Uchumi na Rushwa. SAUTI KUBWAi imefuatilia na inayo machache ya kueleza kuhusu wasifu wa Jaji Luvanda katika kesi za aina hii – “kesi za kimkakati” zinazofunguliwa na dola.

Kwa kifupi, huyu ndiye Jaji Elinaza Luvanda:

  1. Mwaka 2017, Elinaza Luvanda alikuwa katibu wa Kaimu Jaji Mkuu, Jaji Ferdinand Wambari.
  2. Mwaka 2018, aliteuliwa kuwa mjumbe kwenye Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania hadi Rais John Magufuli alipomteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
  3. Mwaka 2021, Jaji Luvanda aliwahukumu kifungo cha maisha Shamim Mwasha na mkewe kwa makosa ya mihadarati.
  4. Mwaka 2020, alikuwa miongoni mwa jopo la majaji watatu ambao walikuwa na kesi ya Addo Shaibu dhidi ya Jamhuri kuhusu kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adelardus Kilangi.
  5. Mwaka 2021, alikuwa miongoni mwa jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi ya Peter Msigwa na Joseph Mbilinyi (Sugu) – kesi ya kikatiba dhidi ya Kamishina Jenerali wa Magereza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
  6. Mwaka 2019, alikuwa miongoni mwa jopo la majaji watatu katika kesi ya Zitto Kabwe dhidi ya Spika Job Ndugai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali – kesi ya sakata la CAG Assad kuhojiwa na Kamati ya maadili ya Bunge.
  7. Mwaka 2019, kesi ya madai ya sh.bilioni 10 ya Bernard Membe dhidi ya Musiba, ilianzia kwa Jaji Luvanda kabla hajahamishiwa Mahakama ya Ardhi na hivyo kesi ikapangwa Jaji De Melo.
  8. Mwaka 2020, Jaji Luvanda aliwahukumu Anitha Oswald (mfanyakazi wa PPF Moshi) na Frank Moshi (dereva wa teksi) kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la mihadarati.
  9. Mwaka 2020, Jaji Luvanda alitoa uamuzi wa kutaifisha Tsh.16.7 bilioni kuwa mali ya Serikali baada ya DPP Biswalo Mganga kuwasilisha ombi mahakamani kuwa washitakiwa waliokuwa na kosa la upatu hawakuwahi kufika mahakamani tangu kesi ilipoanza. Washitakiwa walikuwa ni kampuni ya IMS Marketing Tanzania.

Ukiunganisha matukio haya na hukumu ambazo Jaji Luvanda ametoa, hatua kwa hatua, unaweza kuona kuwa huyu ni “jaji wa kimkakati” ambaye amekuwa anapewa kusikiliza kesi za kimkakati. Sasa anasikiliza kesi nyingine ya kimkakati inayomkabili Mbowe na wenzake watatu.

Wachambuzi na wachunguzi wetu wanaendelea kumulika mwenendo wa kesi hii na Jaji Luvanda.

Like
23