Kwa Lowassa ilikuwa zaidi ya Richmond – 009

Kuna watu wamekuwa wananitaka nijadili ufisadi na usafi wa Edward Lowassa, katika muktadha wa orodha ya mafisadi 11 iliyotolewa na Chadema, Septemba 15, 2007, katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam. Wanataka kujua kwanini, baada ya yote hayo, Chadema ile ile iliyojumuisha jina la Lowassa katika orodha hiyo, hatimaye ilimkaribisha na kumteua agombee urais mwaka 2015.

Kwa baadhi yao, nimekuwa natoa majibu mafupi. Kwanza, nawashauri wapitie upya orodha ya mafisadi, wasome na kujikumbusha tuhuma za Chadema kwa kila mtuhumiwa. Lowassa aliwekwa katika orodha hiyo kwa sababu alivunja mkataba wa kampuni ya City Water ya Dar es Salaam. Kampuni ilipeleka shauri mahakamani kudai fidia.

Chadema ilimshutumu Lowassa kwa uamuzi huo ambao, kwa macho yetu wakati ule, ulikuwa wa kibabe, na ungesababishia taifa hasara iwapo serikali ingeshindwa mahakamani. Lowassa ana bahati. Serikali ilishinda shauri hilo. Kwa mantiki hiyo, ufisadi aliotuhumiwa Mwembeyanga ulifutika wenyewe mahakamani.

Lakini alikuwa na bahati mbaya, kwamba nguvu iliyokuwa imetumika kutangaza “ufisadi” huo mwaka 2007, haikutumika tena kutangaza “ushindi wake” mahakamani. Akiwa ndani ya kikao kimojawapo cha Halmashauri Kuu ya CCM mwaka 2012, Lowassa alitumia ushindi wake huu kumkabili Rais Kikwete alipoleta hoja ya mafisadi mbele ya wajumbe.

Kwa mara ya kwanza, baada ya kukaa kimya kwa miaka minne, Lowassa alipata ujasiri wa kumweleza rais kuwa miongoni mwa waliotajwa kwa ufisadi katika orodha ile, na Kikwete alikuwemo, lakini alikuwa hajasafishwa na kikao chochote au mahakama yoyote. Ni jambo la bahati mbaya kwamba wananchi wengi wanaojadili orodha ya mafisadi, wanakosea kudhani na kusema kwamba Chadema ilimtuhumu Lowassa kwa ufisadi wa Richmond. Hapana! Ufisadi wake wa Mwembeyanga ulitokana na yeye kuvunja mkataba wa City Water.

Hata sakata la Richmond lilipoibuka mwaka 2008, likamuumiza Lowassa kisiasa na kijamii, Rais Kikwete, kwa kuwa alijua ukweli halisi, alimfariji Lowassa kuwa ile ilikuwa “ajali ya kisiasa.” Baadhi yetu tulikuwa hatujajua vema undani wa sakata la Richmond. Nasi tuliingizwa katika mkumbo ambao nitaujadili baadaye kidogo. Hata leo, wapo watu wanaodhani kwamba Richmond ilikuwa mali ya Lowassa.

Mwaka 2009, niliporejea nyumbani kutoka masomoni Uingereza, miongoni mwa watu wa kwanza niliokutana nao ni Dk. Harrison Mwakyembe, mbunge wa Kyela, ambaye pia ndiye alikuwa ameongoza kamati teule ya Bunge iliyochunguza sakata la Richmond. Katika ushirika wetu wa kupambana na ufisadi, Dk. Mwakyembe alikuwa rafiki yangu. Jioni moja, tukiwa nyumbani kwake Kunduchi, Dar es Salaam, tulizungumza mambo mengi ya kitaifa.

Dk. Mwakyembe aliniambia kuwa kilichomponza Lowassa katika Richmond si umiliki, bali akiwa waziri mkuu alishiriki katika kusimamia mchakato wa kampuni hiyo kupewa tenda. Aliniambia pia kwamba kamati teule ilipoanza uchunguzi, katika siku za awali kabisa, iligundua kuwa rais alikuwa anahusika, lakini iliogopa kumhusisha au kumtaja rais kwa kuwa wajumbe walihofia “kuuawa.”

Aliongeza pia kuwa walikwepa kumhoji waziri mkuu Lowassa makusudi, kwani walitambua kuwa kwa cheo chake na utendaji wake, angeweza kuathiri matokeo ya kazi ya kamati kabla haijawasilishwa bungeni. Lengo lao lilikuwa kumwadhibu waziri mkuu, kwa kuwa waliona “mkono” wake, hata kama hakuwa mmiliki.

Jambo jingine aliloniambia ni kwamba siku chache kabla ya kwenda Bungeni, rais alimwomba Dk. Mwakyembe ampelekee nakala ya ripoti ya kamati teule aipitie. Akasema kuwa baada ya rais kugundua kuwa jina lake halikuwa miongoni mwa watuhumiwa, alimwambia, “haya endelea.” Naye alishangaa kwamba rais alikuwa anajua, na alibariki kilichokuwa kinaendelea bungeni dhidi ya Lowassa.

Sababu kuu ya Dk. Mwakyembe na wenzake kumwadhibu waziri mkuu ni ugomvi wa madaraka bungeni kati ya Lowassa (waziri mkuu na kiongozi wa shughuli za serikali bungeni) na Samuel Sitta (spika). Nimewahi kueleza kuwa “ugomvi” wao ulisababishwa na ahadi ya Kikwete wakati anagombea urais. Aliahidi kumpa Sitta uwaziri mkuu. Vile vile, aliahidi kuwapa wengine, akiwemo Lowassa.

Baada ya uchaguzi, wakati anaanza kuunda serikali, huku Pius Msekwa akiwa ameshajiandaa kugombea uspika, Rais Kikwete alituma ujumbe wa kushtukiza kwa Sitta kumwomba agombee uspika! Maelezo ya Rais Kikwete kwa Sitta ni kwamba, kwa kuwa walikuwa wamefanikiwa kukamata serikali, lakini hawakuwa na uhakika na bunge, alihitajika mtu wanayemwamini, awasaidie kukamata bunge, ili mambo yao yaende sawa sawa.

Kikwete alimwaminisha Sitta kwamba hakukuwa na mtu mwingine aliyeaminiwa kukamata bunge. Kwa ujumbe huo pekee, Sitta alijua kuwa hakuwa tena chaguo la Kikwete katika uwaziri mkuu. Zilianza kampeni kali kumsaidia Sitta, wakisaidiwa mno na vyombo vya habari. Msekwa aliitwa “agano la kale.” Naye kwa kutojua, alimuuliza Rais Kikwete, “nasikia hunitaki?” Rais Kikwete alikanusha kuhusika na njama hizo.

Matokeo ya uchaguzi wa spika yalimpa ushindi Sitta. Lakini katika moyo na akili zake, hakuwahi kudhani kwamba Lowassa ndiye angeteuliwa kuwa waziri mkuu. Licha ya kwamba Sitta na Lowassa walikuwa kwenye kambi moja wakati wa kampeni, yeye na baadhi ya wenzake walikuwa wameanza kumzunguka Lowassa, kwa propaganda za mwaka 1995, kwamba “alikataliwa na Mwalimu Nyerere.”
Kwa hiyo, hata alipopokea barua ya uteuzi wa waziri mkuu kutoka Ikulu, Sitta alipatwa na mshtuko alipoona jina la Lowassa na kulisoma kwa wabunge ili wapige kura ya kumthibitisha.

Muda mfupi kabla ya hapo, mbunge mmoja mpya, aliyekuwa katika kambi ya Sitta, ambaye hakupenda Lowassa awe waziri mkuu, baada ya kupata tetesi kuwa Lowassa ndiye alikuwa chaguo la Kikwete, alikimbilia kwa Mzee Samwel Malecela kumwomba asaidie kuzuia uwaziri mkuu wa Lowassa.

Akamwambia Malecela: “Nasikia atamteua Lowassa. Wewe uliondolewa kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa sababu walisema Nyerere alikukataa. Nyerere huyo huyo si alimkataa na Lowassa? Tunataka utusaidie kufanya kampeni ya kupiga kura ya hapana, iwapo Lowassa atateuliwa.”

Mzee Malecela alimtazama mbunge huyo, akatabasamu, halafu akamwambia: “Sikiliza. Namjua Lowassa. Alipoteuliwa kuwa waziri kwa mara ya kwanza, aliletwa ofisini kwangu, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, akawa waziri wa nchi. Mimi ndiye nilikuwa waziri mkuu. Najua utendaji wa Lowassa. Ni mtu ambaye akiamua kufanya jambo, hataki kulala mpaka jambo hilo litekelezwe. Ni mchapakazi.

“Yote yatasemwa juu yake, lakini natambua kuwa akiwa waziri mkuu, atachapa kazi bila kupumzika. Pili, wewe naona ni mbunge mpya. Hujui watu hawa. Wameshashinda, na wameshika serikali. Utawapinga, lakini hutafaulu kuwazuia. Na ukishashindwa, ujue kuwa ubunge wako utakuwa wa tabu, kwa sababu watakuandama. Waache. Hutaweza kuzuia Lowassa kuwa waziri mkuu.”

Mbunge huyo aliondoka akiwa ameinamisha kichwa. Mbunge huyo, akiwa swahiba wa Sitta, alikuwa miongoni mwa wabunge machachari waliokuwa wanasumbua serikali bungeni. Zaidi ya hayo, alishiriki hata kuandika upya kanuni za bunge ili kuwezesha bunge libane serikali.

Kwake, serikali ilikuwa Lowassa, si Kikwete. Na lilipozuka suala la Richmond, kampuni iliyoingizwa nchini na Sitta akiwa mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania, mbunge huyo aliteuliwa kuwa mjumbe katika kamati teule ya Bunge iliyochunguza sakata hilo.
Jambo ambalo halikujulikana mapema ni kwamba Dk. Mwakyembe naye alikuwa na kampuni ya kuzalisha umeme, ikishindana na Richmond. Kwa hiyo, hakustahili kuwa mwenyekiti wa kamati teule, kwa kuwa na maslahi ya moja kwa moja. Ilikuwa lazima Lowassa “asulibiwe.” Kwao, ilikuwa zaidi ya Richmond.

Ilijulikana baadaye kwamba Lowassa hakujua kwamba Rais Kikwete alikuwa ameamua kujivua lawama katika sakata la Richmond. Mara baada ya Bunge kuahirishwa mchana, Lowassa alikwenda moja kwa moja kwa rais. Wakateta kuhusu suala hilo, na jinsi bunge lilivyochafuka.

Rais akamshauri Lowassa ajiuzulu bungeni, lakini kwa ahadi kwamba angekataa barua yake ya kujiuzulu – ilimradi ameshaonesha moyo wa uwajibikaji. Vyanzo vya kuaminika vinasema Lowassa aliomba karatasi pale pale, akaandika na kumpa karani aichape, baadaye akaisaini na kumkabidhi rais.

Mara tu alipoondoka Ikulu kuelekea Bungeni, ujumbe wa wabunge wa CCM ukaingia Ikulu wa rais na kumweleza kuwa kwa jinsi ilivyo, rais akimng’ang’ania Lowassa naye atanguka. Muda mfupi baadaye ukaja ujumbe kutoka idara ya usalama wa taifa, ukiwa na hoja hiyo hiyo, kwamba asipoondoka Lowassa wabunge wanaweza kupoteza imani na rais. Bahati mbaya, Lowassa alipokuwa amejiuzulu, Rais Kikwete hakumwite tena kumpa mrejesho wa taarifa mpya alizonazo.

Laiti Lowassa angejua kinachoendelea, angetumia fursa hiyo kujenga hoja na kujitetea bungeni. Alipokuwa kujua, alikuwa ameshachelewa. Ndivyo alivyopatikana Mizengo Pinda, na ndivyo Rais Kikwete alivyopata ujasiri wa kumpa pole Lowassa kwa kile alichoita “ajali ya kisiasa.”

Pamoja na hayo, Lowassa aliendelea kumfichia rais siri. Aliendelea kumwamini na kumlinda kwa kukaa kimya hata aliposhambuliwa. Alivunja ukimya mwaka 2012 ndani ya kikao cha NEC alipotaka rais aeleze wajumbe ukweli kuhusu Richmond. Upepo ulichafuka kwa muda, lakini baadaye kikao kiliendelea bila rais kutoa ufafanuzi.

Kwa Lowassa, huo ulikuwa ushindi mkubwa uliompatia ushujaa wa ghafla ndani ya NEC. Waliokuwa hawajui wakapata fursa ya kujua kwamba katika sakata la Richmond, yeye alipotea ili wengine wanusurike.

Hadi sasa sakata la Richmond limebaki kuwa la kisiasa. Serikali ya awamu ya tano imeanzisha mahakama ya mafisadi, lakini hakuna anayetaka Richmond ifikishwe mahakamani. Kwanini? Wanaogopa kusiibuke mambo mazito ambayo yalifichwa kwa miaka mingi.

Samuel Sitta alipofariki dunia mwaka 2016, niliandika tanzia nikirejea historia ya mapambano kati ya Sitta na serikali, na matokeo mema ya ushujaa aliopata kutokana na ugomvi wake na Lowassa. Kwa ajili ya kutunza kumbukumbu, katika andiko lijalo nitaweka hapa tanzia hiyo iliyochapishwa katika gazeti MwanaHALISI.

Like
10

Leave a Comment

Your email address will not be published.