WANASIASA machachari wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Edward Kinabo na Yeriko Nyerere, kesho wanatarajiwa kuchuana vikali na wazungumzaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na ACT-Wazalendo katika mdahalo maalumu ulioandaliwa na vyombo vya habari katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.

Washiriki kutoka CCM wanaotarajiwa kushiriki mdahalo huo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo, na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Ally Hapi. Taarifa ambazo SAUTI KUBWA imezipata ni kuwa ACT-Wazalendo itawakilishwa na Sheikh Ponda Issa Ponda anayegombea ubunge Jimbo la Temeke.

Mdahalo huo uitwao Cafe Talk unalenga kufanya tathmini ya kwa kiasi gani serikali ya awamu ya sita imegusa mahitaji ya “Watanzania wanyonge.”

Kinabo ni Katibu wa Sekretariati na Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma wa CHAUMMA Taifa, na ni mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba kupitia CHAUMMA. Yeriko Nyerere ni mgombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni kupitia CHAUMMA.

Prof Kitila pia ni mgombea anayetetea ubunge wake katika Jimbo la Ubungo kupitia CCM.