Kama ilivyowasilishwa na ripota raia, BJ, leo tarehe 9 Februari 2022.
Shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka Mkaguzi wa Polisi Tumaini Swila anaendelea kuhojiwa na mawakili wa utetezi. Wakili Peter Kibatala ameuliza jumla ya maswali 107. Yaliyojibiwa ni 98. Miongoni mwa majibu hayo, majibu ya ‘NDIYO’ 15, ‘SIFAHAMU’ ni 12, ‘SAHIHI’ ni 9, ‘NAFAHAMU’ 4 na ‘SIJUI’ 1.
Jaji ameingia Mahakamani tayari kuendelea na kesi. Ni saa 4:21 asubuhi ya Februari 9, 2022.
Shauri namba 16 la mwaka 2021 la Jamuhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe linatajwa tena hapa mahakamani.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, ikupendeza mimi naitwa Robert Kidando na nipo pamoja na wakili
- Pius Hilla
- Abdallah Chavula
- Jenitreza Kitali
- Nassoro Katuga
- Esther Martin
- Ignasi Mwinuka na
- Wakili Tulimanywa Majige
Peter KIBATALA: Mheshimiwa Jaji ikupendeza mimi naitwa Peter Kibatala na nipo na wakili
- Michael Mwangasa
- Gaston Garubindi
- Evaresta Kisanga
- Maria Mushi
- John Masoud (kwa niaba ya Nashon Nkungu)
- Clinton Kipengele (kwa niaba ya John Malya)
- Fredrick Kihwelo
- Dickson Matata
(Jaji anaandika. Kisha anaita majina ya washtakiwa wote wanne na wote wanaitika kuwa wapo mahakamani).
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji shauri limekuja kwa ajili kuendelea kusikilizwa na tupo tayari kuendelea na shauri hili.
Peter KIBATALA: Nasi pia Mheshimiwa Jaji tupo tayari kuendelea.
(Shahidi anapanda kizimbani).
(Jaji anaandika).
JAJI: Shahidi nakukumbusha ulikuwa chini ya kiapo na utaendelea kuwa chini ya kiapo.
SHAHIDI: Sawa Mheshimiwa Jaji, ila kuanzia jana jioni hali yangu haikuwa nzuri lakini nitaendelea kutoa ushahidi.
KIBATALA: Good Morning Inspector!
SHAHIDI: Morning.
KIBATALA: Nafikiri unakumbuka jana tulikuwa kwenye suala la Mbowe kuanzisha ugaidi.
SHAHIDI: Sahihi.
KIBATALA: Tulijadili mpaka pale ambapo washitakiwa walikutana pale Morogoro na Luteni Dennis Urio.
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Ni sahihi kwamba upelelezi wako uligundua hivyo?
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Na aliyewaita pale alikuwa ni Luteni Dennis Urio?
KIBATALA: Na utakubaliana na mimi kuwa mpaka mshitakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu wanakutana na Dennis Urio Mbowe alikuwa hawajui na hajawahi kukutana nao?
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Ni sahihi kwamba kabla ya kukutana walikuwa wanafanya shughuli zao halali?
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Ni sahihi kwamba Luteni Dennis Urio aliwaita Morogoro kwa sababu yeye makazi yake yalikuwa Morogoro?
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Kwa namna yoyote ile Freeman Mbowe hakuwahi kuwa Morogoro kabla na baada ya hizo tarehe walizokutana Morogoro?
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Uliwahi kugundua kwa wewe kuwa pro-active au kuarifiwa na Luten Dennis Urio kwamba kabla ya Mohammed Ling’wenya kuondoka Mtwara kuja Morogoro ilibidi awasiliane na Mzee Ling’wenya kupata ruhusa?
SHAHIDI: Sikuwahi kufahamu.
KIBATALA: Na pia hufahamu kwamba Luteni Dennis Urio alitoa ushahidi Mahakamani akithibitisha?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Kwa hiyo hata nikikuambia kwamba Mzee Ling’wenya ilibidi aitishe kikao cha ukoo na familia kujadili suala la mtoto wao kwenda kwa Luteni Dennis Urio?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Pia hufahamu kwamba wakati wanamtoa walimtoa kwa uangalizi kwamba wanamkabidhi kwa Luten Dennis Urio na kwa Freeman Mbowe, kwa sababu ni watu wanaoaminika?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Baada ya kuwa wa wamekutana Luteni Dennis Urio na Khalfani Bwire na Moses Lijenje na baadaye kundi la pili Adam Kasekwa, Mbowe hakuwahi kutia neno katika yale yaliyokuwa yanajadiliwa pale?
SHAHIDI: Fafanua tena.
KIBATALA: Ulikuwa unafahamu kwamba Luteni Dennis Urio alikutana na makundi mawali kwa nyakati tofauti?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Baada ya kuwa wa wamekutana Luteni Denis Urio na Khalfani Bwire na Moses Lijenje na baadaye kundi la pili Adam Kasekwa, Mbowe hakuwahi kutia neno katika ya yale yaliyokuwa yanajadiliwa pale?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Aliyewaambia Bwire na Moses Lijenje na aliyewaambia Adamoo na Ling’wenya alikuwa ni Luteni Dennis Urio. Je, ni sahihi?
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Unaposema kwamba alipowasiliana na Mbowe aliwasiliana kwa meseji, Telegram au simu?
SHAHIDI: Kwa njia ya mdomo na pia kwa njia ya mawasiliano ya jumbe za Telegram.
KIBATALA: Walipoongea Dennis Urio na Freeman Mbowe wewe ulikuwapo?
SHAHIDI: Sikuwapo.
KIBATALA: Wewe kama mpelelezi ulishawahi kusikia neno maarufu la kiupelelezi la “Your Word Against Mine”?
SHAHIDI: Sijui.
KIBATALA: Kwa kuwa wewe, Kingai na DCI hamkuwapo wakati Mbowe anaongea na Urio?
SHAHIDI: Hatukuwapo lakini tulifanya upelelezi.
KIBATALA: Watu wawili wamezungumza, na DCI hakuwapo. Kingai hakuwapo, na wewe hukuwapo. je, si lazima sasa tupime maneno ya Dennis Urio na Freeman Mbowe?
SHAHIDI: Siyo lazima. Unaweza kufanyia kazi maneno ya Dennis Urio.
KIBATALA: Wewe kama mpelelezi wakati Dennis Urio anakutajia kuwa kuna Cassa Motel, je, uliwahi kwenda hata kuthibitisha?
SHAHIDI: Sijawahi kwenda.
KIBATALA: Mgahawa ambao Dennis Urio alitaja wamekutana na Mbowe wewe kama mpelelezi uliwahi kwenda?
SHAHIDI: Sikwenda.
KIBATALA: Je, Urio aliwahi kukuambia kwamba alipanda teksi Mgulani?
SHAHIDI: Sikwenda.
KIBATALA: Je, aliwahi kukuambia kwamba alikuwa mjini alipanda bodaboda?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Je, uliwahi kufika kuona kama kuna kituo cha bodaboda?
SHAHIDI: Sikwenda.
KIBATALA: Je, uliwahi kwenda Cassa Motel kuthibitisha kama gari ya Dennis Urio lilifika pale?
SHAHIDI: Sikwenda.
KIBATALA: Uliwahi kwenda Mgulani kuthibitisha kwamba Denis Urio aliwahi kufika na kuishi pale?
SHAHIDI: Sikwenda.
KIBATALA: Nyiye kama Polisi mkipata taarifa mnairekodi au kuifanyia kazi?
SHAHIDI: Tunafanyia kazi.
KIBATALA: Je, wewe kama mpelelezi uliwahi kwenda Julai 14, 2020 kule Ngerengere 92 KJ kujua kama kweli alikuwa kazini?
SHAHIDI: Sikwenda.
KIBATALA: Je, unafahamu kwamba baada tu ya kurejea kutoka Darfur alikamatwa kikosini baada ya kutajwa na Adam Kasekwa?
SHAHIDI: Sifahamu. Nilifanya uchunguzi.
KIBATALA: Kwa kuwa umechunguza, kule 92 KJ uliongea na nani?
SHAHIDI: Nimeshasema sikwenda.
KIBATALA: Kwa hiyo wewe hata 92 KJ hufahamu hata mkubwa wake ni nani?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Kwa hiyo hufahamu hata 92 KJ ipo wapi?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Unafahamu kwamba makampuni ya simu yanatunza kumbukumbu za mawasiliano?
SHAHIDI: Nafahamu.
KIBATALA: Je, yanatunza kwa muda gani?
SHAHIDI: Sikumbuki.
KIBATALA: Je, wewe kama mpelelezi uliomba taarifa za call recordings katika makampuni ya simu kati ya Freeman Mbowe na Dennis Urio?
SHAHIDI: Ndiyo. Niliomba.
KIBATALA: Kwa barua ya tarehe ngapi?
SHAHIDI: Kwa barua ya tarehe 13 Agosti 2020.
KIBATALA: Kwenda kampuni gani?
SHAHIDI: Kwenda kwenye kitengo cha uchunguzi wa makosa ya mtandao.
KIBATALA: Kwa Inspekta Ndowo?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Kwa hiyo wewe uliomba taarifa kwa Inspekta Ndowo. Je, yeye ndiye mwenye kuhifadhi?
SHAHIDI: Yeye ndiye aandike barua kwenda TiGO na Airtel.
KIBATALA: Kwa hiyo wewe pamoja na mambo yote ulimwomba na rekodi za mawasiliano ya simu?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Je, wewe uliona katika barua yake kutoka kwenu Terms of Reference suala la Call Recordings lipo?
SHAHIDI: Halipo.
KIBATALA: Kwa hiyo mliomba au hamkuomba?
SHAHIDI: Hatukuomba.
KIBATALA: Uwe sasa unasikiliza kwa makini.
KIBATALA: Haya! Unafahamu kuhusu Sheria ya EPOCA?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Kwa hiyo hufahamu kwamba Sheria hiyo inakupa mamlaka ya kuomba voice recordings?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Kwa hiyo wewe wakati DCI na Kingai wanakuteua walikuteua kwa sababu ya uwezo au sababu ya Kutengo X?
SHAHIDI: Sababu ya uwezo.
KIBATALA: Hivi una elimu gani?
SHAHIDI: Kidato cha sita.
KIBATALA: Sekondari gani?
SHAHIDI: Moshi Sekondari.
KIBATALA: Ulipata division ngapi?
SHAHIDI: Division Three ya points 13.
KIBATALA: Ulifaulu kwenda chuo?
SHAHIDI: Hapana. Nilienda CCP Moshi.
KIBATALA: OK. Sawa! Ndiyo walikuchagua sababu ya uwezo?
KIBATALA: Je, unafahamu kwamba mojawapo ya majukumu ya upelelezi kazi yako ilikuwa ku- trace kila single cent?
SHAHIDI: Hilo siyo muhimu. Cha muhimu kama alitoa pesa kufadhili ugaidi.
KIBATALA: Swali langu nasema kwamba kama mpelelezi una jukumu la ku- account for na ku- trace kila single cent.
SHAHIDI: Nishajibu kuwa siyo muhimu.
KIBATALA: Je, nani alikuwa na jukumu la kuona na kuthibitisha zile pesa?
SHAHIDI: Nafahamu.
KIBATALA: Na hilo jukumu uliteleleza kikamilifu la ku- trace hizo pesa?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Na tayari kwamba Dennis Urio alituambia kuwa watuhumiwa walisafiri kutoka walipokuwa kuja Morogoro. Je, unafahamu kwamba walikuwa refunded?
SHAHIDI: Nafahamu.
KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji nani alitoa pesa kuwa- refund (kuwarejeshea).
SHAHIDI: Luteni Dennis Urio.
KIBATALA: Na kwamba unafahamu kwamba hawa walikuwa wanajua kuwa walikuwa wanapewa pesa kurejeshewa nauli zao.
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Unafahamu kwamba ni shilingi ngapi Moses Lijenje alirejeshewa?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Lini wewe ulifahamu kuwa unakuja kutoa ushahidi?
SHAHIDI: Alhamisi.
KIBATALA: Hiyo taarifa ulipewa na watu serious au uliwachukuliwa poa?
SHAHIDI: Nilichukua serious.
KIBATALA: Hii kesi ni kubwa au nyepesi?
SHAHIDI: Kubwa.
KIBATALA: Wewe kama mpelelezi ni nani atakuja kutueleza kuhusu mabadilishano ya pesa kati ya Moses Lijenje na Khalfani Bwire kutoka kwa Dennis Urio?
SHAHIDI: Ni mimi.
KIBATALA: Shahidi anaitwa Gladys Fimbari kutoka Airtel alileta taarifa ya miamala. Je, ulisoma na kuelewa?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Je, pesa ambayo walibadilishana mikono kati ya Adam Kasekwa na Denis Urio ilikuwa shilingi ngapi?
SHAHIDI: Sikumbuki.
KIBATALA: Pesa ambayo ilibadilishana mikono katika ya Mohammed Ling’wenya na Dennis Urio ni shilingi ngapi?
SHAHIDI: Sikumbuki.
KIBATALA: Ni wewe ulimhoji Dennis Urio?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Alikueleza?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Ilikuwa shilingi ngapi?
SHAHIDI: Sikumbuki.
KIBATALA: Pesa iliyobadilishana mikono kati ya Moses Lijenje na Khalfani Bwire ilikuwa shilingi ngapi?
SHAHIDI: Sikumbuki.
KIBATALA: Unafahamu ni pesa kiasi gani ambacho alipewa Mohammed Ling’wenya nauli ya kwenda Moshi?
SHAHIDI: Sikumbuki.
KIBATALA: Wakati washitakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu wanakwenda Moshi kama wanavyosema watuhumiwa, je, walikuwa wanafahamu wanaenda kufanya nini huko?
SHAHIDI: Walikuwa hawafahamu.
KIBATALA: Nikumbushe kozi uliyosema kwamba ulisomea masuala ya ugaidi Botswana.
SHAHIDI: Post Blast Scene Investigation.
KIBATALA: Ni sahihi kuwa kozi hiyo inahusu uchunguzi baada ya milipuko?
SHAHIDI: Sahihi.
KIBATALA: Umesoma Sheria yetu ya ugaidi hapa Tanzania?
SHAHIDI: Nimesoma kidogo.
KIBATALA: Umesoma kuhusu vifungu vinavyohusika na ufadhili wa ugaidi?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Unafahamu vipengele vinavyohusika katika ufadhili wa ugaidi?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Taja.
SHAHIDI: 1. Anayetuma lazima awe anafahamu malengo ya fedha, 2. siyo lazima awepo eneo la tukio, 3. siyo lazima matumizi ya pesa yajulikane.
KIBATALA: Kwa hiyo hata uchunguzi wako ulifuata hicho ulichoelewa wewe?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Na conclusion yako ilijikita katika tafsiri hiyo?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Je, unafahamu kwamba uwepo wa pesa yenyewe ni sehemu ya shitaka?
SHAHIDI: Nafahamu.
KIBATALA: JE, nikitaka kutuma pesa kufadhili kitengo cha ugaidi Mtwara, je, ikiwa pesa ile imeenda kutumika kwenye kilimo cha mpunga Ifakara nitakuwa nimefadhili ugaidi?
SHAHIDI: Inategemea.
KIBATALA: Inategemea na nini?
SHAHIDI: Kama pesa imekwenda.
KIBATALA: Narudia swali. Je, nikitaka kutuma pesa kufadhili kitengo cha ugaidi Mtwara, ikiwa pesa ile imeenda kutumika kwenye kilimo cha mpunga Ifakara nitakuwa nimefadhili ugaidi?
SHAHIDI: Ndiyo. Unakuwa umefadhili ugaidi.
KIBATALA: Je, una ushahidi wowote kwamba ile 199,000 ilitumika kule Moshi walipokuwa wamefika?
SHAHIDI: Hilo sifahamu. Najua tu kuwa walifadhili.
KIBATALA: Katika maelezo ya Luteni Dennis Urio anasema alitumiwa kiasi cha shilingi 500,000 katika simu yake ya 0787-555 200, je alikuambia?
SHAHIDI: Aliniambia.
KIBATALA: Hiyo 500,000/- kwa mujibu wa Dennis Urio, Mbowe alituma kwa sababu gani?
SHAHIDI: Kwa sababu ya kufadhili vitendo vya kigaidi.
KIBATALA: Ambavyo ni vitendo vipi?
SHAHIDI: Kulipua vituo vya mafuta, kukata miti barabarani, kudhuru viongozi wa Serikali…
KIBATALA: Unafahamu kwamba Luteni Dennis Urio anasema katika maelezo yake kwamba aliwapa Khalfani Bwire na Moses Lijenje aliwapa kuwa- refund kama nauli?
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji naomba afafanue. Je, ana- refer katika maelezo au ushahidi?
KIBATALA: Katika statement yake Dennis Urio anasema alitoa shilingi 300,000 akawapa Moses Lijenje na Khalfani Bwire. Na katika ushahidi wake Dennis Urio anasema kuwa aliwapa shilingi 150,000 kila mmoja kuwarejeshea nauli huko alipotaka.
KIBATALA: Je, unafahamu?
SHAHIDI: Sifahamu.
KIBATALA: Kati yako wewe na Dennis Urio nani yupo katika nafasi nzuri ya kufahamu jinsi pesa Ilivyogawiwa na kutumika?
SHAHIDI: Ni Luten Dennis Urio.
KIBATALA: Je, shahidi ulisoma maelezo ya onyo ya Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya?
SHAHIDI: Nilisoma ila sikumbuki kiwango.
KIBATALA: Ungependa kujikumbusha au isingependa?
SHAHIDI: Ningependa kujikumbusha.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji naomba kielelezo namba 1 na kielelezo namba 13.
KIBATALA: Tuanze na maelezo ya Adam Kasekwa. Tafuta sehemu ambapo anasema tarehe 24 Julai 2020 nilikutana na Mohammed Ling’wenya.
(Shahidi anaangalia kama vile haoni sawasawa).
SHAHIDI: “Tarehe 24 Julai 2020 nilikutana na Mohammed Ling’wenya kasisitiza twende Morogoro tukakutane na Luteni Urio. Tuliondoka siku hiyo hiyo na kukutana na Luteni Dennis Urio. Akasema maelezo tutayakuta huko huko. Akatupa shilingi 87,000 kila mtu nauli ya kwenda Moshi.”
(Shahidi anaonyesha amemaliza kusoma).
KIBATALA: Shilingi ngapi umesoma?
SHAHIDI: Ni shilingi 87,000 kila mmoja.
KIBATALA: Ulilinganisha maelezo ya Mohammed Ling’wenya ni shilingi ngapi kapewa dhidi ya maelezo ya Luten Denis Urio?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Kama mpelelezi makini kabisa?
SHAHIDI: Ndiyo.
KIBATALA: Je, Luteni Dennis Urio alikuambia aliwapa shilingi ngapi?
SHAHIDI: Sikumbuki.
KIBATALA: Ungependa ujikumbushe?
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji naomba kielelezo namba D4.
KIBATALA: Hiki ni kielelezo cha upande wa utetezi. Naomba niruhusiwe kuendelea bila kuwapa nafasi ya kuficha ushahidi.
WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Mheshimiwa Jaji nimemsikia Kibatala ambaye wenzetu waliomba kielelezo hiki kwa matumizi yao, na waliomba kwa kutumia kifungu cha 154 cha Sheria ya Ushahidi Sura ya Sita. Dhumuni ni kum- contradict shahidi ambaye alikuwa ni Dennis Urio. Leo hii anaposimama na…
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji anachokifanya wakili Abdallah Chavula kuhusu kutaja vifungu …
WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Mheshimiwa Jaji, samahani…
KIBATALA: Mheshimiwa huyu anasimama kama nani mwenye hoja? (Wakili wa Serikali kakaa).
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, Wakili Pius Hilla anafanya vurugu.
WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Mheshimiwa Jaji, anachokifanya Wakili Peter Kibatala siyo sahihi. Harusiwi kutumia hayo maelezo kwa sababu yalikuwa kwa kazi ile tu.
JAJI: Ulisimama Wakili Kibatala.
JAJI: Wakili Peter Kibatala kaa kwanza tumsikilize.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, nimesimama na mwenye hoja akakaa chini kwa sababu ni educated. Kumbukumbu zitaonyesha nani alifanya vurugu.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji! Mheshimiwa Jaji! Hoja yangu ni kwamba sijaleta neno jipya. Kuhusu rejoinder ni kujibu yale aliyoyajibu yeye. Hilo siyo lengo letu.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, kwa kuwa mwenzangu ametaja vifungu na mambo mapya, naomba sasa nipewe nafasi ya ku- respond (kujibu) kuhusu vifungu.
JAJI: Nimuache kuhusu kujibu vifungu?
WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Mheshimiwa Jaji, mwache aseme kuhusu vifungu kwa sababu Sheria haina kificho.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, wakati Wakili Robert Kidando anataja hoja yake hakutaja kuhusu vifungu vya sheria.
JAJI: Lakini sasa Wakili Chavula alikuwa hajamaliza.
WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Mheshimiwa Jaji nilikuwa naeleza kwamba kifungu walichokitumia wenzetu kilikuwa ni kifungu cha 164, na kuhusu kupokelewa mahakamani, Mahakama ilitumia kifungu cha 154. Kwa sheria ambayo niliyokuwa nayo mimi inaonekana katika mstari wa tatu wa 154 ambayo haina subsections.
(Sasa Wakili wa Serikali anasoma kifungu).
WAKILI WA SERIKALI: Sisi tuntilia mkazo katika “intended to contradict” na “for the purpose of contradict”. Kama shahidi ni maker wa ile nyaraka, then sawa. Hata ile dhana ya fairness haipo, ndiyo maana wanasheria waka- limit kwa ile tu, kwa dhana hiyo. Mwenzetu hana uwezo wa kuitumia.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, kwanza maneno “maker” ni maneno binafsi wala si kwenye sheria. Sheria inasema kwamba kama ameshiriki, ku- reduce into writing. Hata katika hiyo 164 haikuweka ukuta wala zuio. Kifungu cha 164 ni kifungu kinachozungumzia kuingizia. 164(c) inasema By proof of former statement. Hakuna ukuta au zuio. Huyu tunamuuliza kwa sababu ndiye mpelelezi kwamba atanyimwa haki ya kuzungumza wakati kuna re examination. Shahidi ame- own suala la hayo maelezo. Na ikumbukwe Mheshimiwa Jaji, Shahidi ameshajibu tayari kuhusu hiyo statement. Vipi ukimikataza sasa hivi na yale majibu ya awali? Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.
JAJI: Hoja iliyojitokeza ni hoja ilianza kwa Mr Kidando kwamba upande wa utetezi hawana haki ya kutumia kielelezo husika, ambapo akasimama Wakili Abdallah Chavula kwa kutaja vifungu vya sheria, kwamba statement hiyo inatumika kwa kum- contradict_ shahidi namba 12 na siyo vinginevyo. Hoja hiyo ilipingwa na upande wa utetezi kwamba vifungu haviweki katazo. Mahakama kwa kuzingatia hoja zote kwa kina, inafahamu kwamba upande wa utetezi kwa shahidi aliyepo Mahakamani lao ni kutengeneza misingi. Shahidi aliyepo mahakamani ni mpelelezi wa shauri hili. Wakati anaulizwa na mawakili wengine alisema kwamba alitumia nyaraka zote katika upelelezi kufikia katika hitimisho. Kwa maana hiyo anaulizwa kuhusu kitu alichofanya nacho kazi. Ndiye aliyemwandika maelezo ya Luteni Dennis. Kama hawezi kujibu atatuambia kuwa hawezi. Kwa sababu hiyo hatuoni sehemu ambayo ina udhibiti wa kuendelea kujibu. Kwa maana hiyo mahakama inaruhusu kutumika kwa kielelezo hicho.
(Mawakili wa pande zote mbili wanakubaliana na uamuzi wa Jaji kwa kusimama na kuinama kidogo).
KIBATALA: Shahidi tulikubaliana kuwa moja ya investigative tools … ni hii statement ya pesa na maelezo haya.
SHAHIDI: Ni sahihi.
KIBATALA: Soma pale “…baada ya kupokea pesa hizo nilizitoa…”
SHAHIDI: “Tarehe 22 Julai 2020, baada ya kupokea pesa hizo nilizitoa, na kuwapatia Mohammed Ling’wenya na Adam Kasekwa kama nauli…”
KIBATALA: Sasa mwambie Mheshimiwa Jaji kwamba ile shilingi 87,000 anayosema Adam Kasekwa kila mmoja, je, wewe kama mpelelezi unaona shilingi 87,000 ya Adamoo na Ling’wenya inaendana na taarifa ya mtoa taarifa wenu?
SHAHIDI: Hilo linahitaji maelezo. Wote wanaelezea suala la pesa. Luteni Dennis Urio anasema aliwapa shilingi 190,000.
KIBATALA: Shilingi 190,000 iko wapi?
SHAHIDI: Vyote vinaendana maelezo ya Denis Urio na akina Adam Kasekwa.
KIBATALA: Sawasawa. Wacha jibu lako liingie.
KIBATALA: Kama walipewa kila mmoja shilingi 87,000, Jumla ni shilingi ngapi?
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji samahani. Ukisoma statement ya mshitakiwa wa pili (kielelezo namba moja) kwamba alitupa nauli shilingi 87,000 kila mtu, huku alipomrejesha katika shilingi 199,000 aliyowapa Adamoo na Ling’wenya.
KIBATALA: Hakuna hoja hapo.
SHAHIDI: Samahani Mheshimiwa Jaji sijisikii vizuri!
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, sisi tunaamini kuwa ahirisho linaombwa kwa sababu nyingine na siyo sababu ya ugonjwa.
JAJI: Kabla ya hapo, hoja yao ni kwamba kila utakapotaja shilingi 199,000 usiseme nauli.
KIBATALA: Kwenye hiyo Mheshimiwa Jaji, haina shida. Nitarudi nyuma na kujenga upya misingi kurahisisha.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) (Anamfuata shahidi na kutetea naye jambo).
(Wakati shahidi anaongea na Wakili wa Serikali Robert Kidando anaonekana akitingisha kichwa).
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji nimeongea na shahidi anasema hajisikiivizuri, na kapata na tatizo ghafla. Mheshimiwa Jaji naomba tuweze kupatiwa na ahirisho.
WAKILI WA SERIKALI: Lakini Mwenzetu kusema shahidi aendelee sababu fulani fulani nafikiri Mheshimiwa Jaji si vyema kusema hivyo. Baada ya kusema hayo naomba ahirisho.
JAJI: Je, ahirisho la masaa m[aka saa 7 au ahirisho la siku au nini?
(Wakili wa Serikali Robert Kidando anamfuata tena shahidi kuteta naye).
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji anaomba ahirisho mpaka kesho. Hatuwezi kujua itakuwaje.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, sisi tuna wasiwasi sana na sababu zilizotolewa na shahidi kama ni sababu njema. Sisi tunapinga ahirisho mpaka kesho. Ikupendeze uahirishe mpaka saa tisa alasiri tuje tuone progress kwa sababu ahirisho linaloombwa linaathiri haki za wateja wetu. Na tutakaporejea tunaomba shahidi aje na uthibitisho kwamba alikwenda hospitali na alitibiwa.
KIBATALA: Ilishawahi kutokea mara kadhaa, Inspekta Jumanne Malangahe alisema hivyo hatukuona uthibitisho, Inspekta Ndowo alifanya hivyo hivyo hakuketa uthibitisho na sasa ni huyu. Hii ni Mahakama. Wateja wangu wanayo haki ya kufahamu au kuona japo kuna haki na kweli inatendeka.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji anasema ana wasiwasi na Mheshimiwa Jaji hatuwezi kucheza na haki za watu.
WAKILI WA SERIKALI: Ninachokumbuka shahidi aliongea asubuhi kuwa leo hajisikii vizuri. Hizi proceedings serious hatuwezi kuleta mzaha. Naomba ahirisho mpaka kesho ijulikane itakuwaje baada ya shahidi kupata matibabu.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji naomba kurudisha vielelezo.
(Mahakama iko kimya kiasi kwamba hata ukidondosha sindano utasikia mlio).
(Jaji bado anaandika. Mahakama bado iko kimya sana).
JAJI: Kufuatia maombi yaliyotolewa na shahidi, kwamba hajisikii vizuri na maombi hayo yaliungwa mkono na mawakili wa Serikali, shahidi ameomba nafasi ya kwenda kupata matibabu. Maombi haya yamepigwa na upande wa utetezi kupitia Wakili Peter Kibatala, na kwamba kuna mifano kadhaa ya mashahidi waliopita, na kwamba Mahakama itoe ahirisho mpaka saa tisa alasiri. Kwa kuzingatia maombi ya pande zote mbili na shahidi mwenyewe, ukizingatia shahidi alisema asubuhi kwamba hajisikii vizuri, katika utoaji haki wa Mahakama zetu shahidi lazima awe na uwezo wa kusimama au kukaa. Shahidi ameshasema hajisikii vizuri. Kwa hiyo Mahakama haiwezi kwenda tofauti na utaratibu huo. Mahakama inaona suala la shahidi kusema hajisikii vizuri ni suala la kutoa ahirisho. Na suala linalobakia ni ahirisho mpaka muda gani. Mahakama inaona kwamba suala la ugongwa siyo suala la kununua spea na kurudisha. Ni suala la afya. Mahakama haiwezi kumpangia muda wa kupata matibabu. Kwa sababu hiyo Mahakama inatoa ahirisho mpaka kesho. Suala la hoja ya utetezi wa kwamba shahidi alikuwa anaumwa ni suala muhimu hata kama uthibitisho huo hautakuwa into details. Lengo ni kulinda privacy. Shahidi nakuonya kuwa utatakiwa kuwa kizimbani kesho saa tatu asubuhi. Washitakiwa wataendelea kuwa rumande chini ya Magereza mpaka kesho asubuhi saa tatu kamili.
Jaji anaondoka mahakamani. Ni saa 6:45 mchana.