Huu ni ujumbe mbaya mbele ya watu wasiohusika

President John Magufuli - File photo

WIKI iliyoisha Jumapili 26 April 2020, Rais John Magufuli alihutubia taifa akiwa nyumbani kwake Chato kuhusu mapambano dhidi ya kuenea kwa virus vya Korona (COVID 19). 

Katika hali ya kushangaza sana, aliita wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama waende Chato ili awahutubie wakati anahutubia taifa. Walisafiri kutoka Dodoma na wengine kutoka Dar es Salaam ili kusikiliza hotuba yake wakiwa Chato. Chanzo kimoja kimeandika mahali, nami nanukuu: “Nilibahatika kusafiri na mmoja wao na nikiri wazi, sijawahi kuona kamanda aliyekata tamaa kama huyo katika maisha yangu.”

Inaonekana wazi kuwa kabla ya makamanda hao kuitwa Chato kulikuwa na kazi kubwa ya kumshawishi rais aseme kitu au afanye uamuzi mpya wa kuweka mwelekeo wa mapambano dhidi ya Korona. 

Baada ya yeye kukubali lililobakia lilikuwa ni aina ya mwelekeo mpya amabo angeweka. Ujumbe wa rais kwa taifa na makamanda ulikuwa mbaya, usiofaa na usio na matumizi. Waingereza wanasema ulikuwa “irrelevant.” 

Badala ya kupambana na kuenea kwa virusi, yeye alichagua kupambana na watu wasioonekana lakini waliokuwa wanashauri namna nyingine ya mapambano.

Aliamua kutumia fursa hiyo kukataa ushauri aliopewa na watu wake wa karibu, wakiwemo wasaidizi wake, kuhusu kufungia Jiji la Dar es Salaam kwa muda kama njia ya kudhibiti uenezaji wa maambukizi. 

Akakataa kuzuia mikusanyiko, akahimiza watu watoke wafanye kazi, akafundisha watu watumie dawa za kienyeji, akawajaza watu shaka juu ya matumizi ya barakoa za kigeni, akapingana na Benki ya Dunia na kusisitiza kuwa nchi maskini zinahitaji msamaha wa madeni kuliko misaada au mikopo mipya, na akahoji takwimu zinazotolewa na serikali yake mwenyewe kuhusu maambukizi ya virusi vya Korona. 

Ujumbe huu haufai na haukupaswa kutolewa na mkuu wa nchi wakati huu. Ujumbe kama huo ulipaswa kuwa mhadhara wa kisomi katika kongamano la wataalam, na katika si hotuba ya mkuu wa nchi kwa taifa. Aliwageuza watanzania kuwa wanafunzi darasani na yeye akawa mwalimu.

Kasoro kubwa ya pili ni kitendo cha yeye kuhutubia makamanda wa vyombo vya ulinzi. Sijui nani alimshauri au ni tatizo lake yeye binafsi la kupenda kila wakati kuonekana amezungukwa na vyombo hivi? 

Chaguo hili linafunika hata ujumbe aliolenga kuutoa kwa wasikilizaji. Unawezaje kutoa ujumbe wa afya kwa kutumia hadhara ya askari? Ili waufanyie nini? Kitendo hiki cha kujizungushia majeshi kilifunua udhaifu mwingine ndani yake ambao utajadiliwa siku nyingine.

Katika awamu ya tano, matumizi ya vyombo hivi yamezidi mipaka. Yaonekana Magufuli ama anapambana na adui asiyeonekana au anatibu kidonda cha moyoni kwa kutumia makamanda. Kwa jinsi anavyowatumia na wao wakakubali kutumika, amesababisha matatizo makubwa ndani ya vyombo hivyo hata kama hayasemwi hadharani.

Kwanza, amerejesha taswira ya majeshi ya kikoloni ambayo yalitumika kumlinda mkoloni na kukandamiza wananchi. Vyombo vyetu hivi sasa ni nyenzo za kukandamiza haki na uhuru wa raia. Tuliona hata siku hiyo anaviagiza kuwasaka na kuwashughulikia watu wenye maoni tofauti mitandaoni.

Pili, rais amevigawa vyombo ndani yake. Makamanda wanapewa amri zisizotekelezeka na wanapoenda kuwaambia wenzao wanachekwa kama watoto wadogo. Ufa unajengeka taratibu kati ya makamanda na askari wenzao katika majeshi yote. Hii si afya kwa nchi.

Lakini pia kitu kilichoonekana wazi kupitia hotuba ile ni ufa uliopo katika ya rais na wasaidizi wake. Mpaka mtu unajiuliza, ni nani mshauri wa rais ikiwa hata takwimu alizo nazo waziri mkuu ni tofauti na alizo nazo rais kuhusu wagonjwa wa Korona? 

Kabla ya tukio hili la hotuba ya rais, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa ametoa takwimu akasema wagonjwa waliopona ni 11. Rais akasema takwimu alizonazo yeye ni zaidi ya wagonjwa 100! 

Maana yake nini? Kati yao kuna mmoja ana takwimu zisizo sahihi au wote wawili wana takwimu zisizo sahihi. Na kama kuna uwezekano kwamba mmoja wao ana takwimu za uwongo na mwingine za kweli kuhusu waliopona, kwanini jamii isiaminii kuwa hata takwimu kuhusu idadi ya wagonja au waliokufa ambayo wanatangaziwa kila mara si ya kweli?

Yaani, kama hadi siku ile waziri mkuu nawaziri wa afya walisema kulikuwa na wagonjwa jumla ya 284 huku, waliopona wakiwa 11; na baadaye rais akasema waliopona ni 100, inawezekanaje idadi ya wagonjwa ikabaki 284?

Matokeo yake sasa, tangu rais agongane na wasaidizi wake, kumekuwa na ombwe la kutoa taarifa kutoka kwa waziri wa afya kama tulivyozoea. Na pale zinapotolewa, takwimu za wagonjwa wanaopona zimeanza kubadilika haraka mno ili rais aonekane ndiye alikuwa sahihi. 

Kimsingi, kama alivyiwahi kutamka Tundu Lissu mwanzoni mwa utawala wa Magufuli, tuna rais wa ajabu. Na sasa anatufanya tuwe nawaziri mkuu wa ajabu!

Like
4

Leave a Comment

Your email address will not be published.