KATIKATI ya wiki hii, tumeshuhudia Lionel Messi akinyakua tuzo ya Ballon D’or (mchezaji bora wa soka duniani) kwa mara ya saba katika sherehe kabambe za tuzo hiyo zilizofanyika jijini Paris, Ufaransa.
Kwa ushindi huo, Messi ameongeza idadi ya tuzo hiyo mara mbili zaidi ya mpinzani wake wa jadi, Cristiano Ronaldo, aliyeshinda tuzo hizo mara tano tu.
Licha ya sherehe hizo kupamba moto, zilighubikwa pia na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau juu ya uhalali wa Messi kutwaa tuzo hiyo, wakidai kuwa Robert Lewandowski, mshambuliaji mahiri wa Bayern Munich ameonyesha kiwango bora na amekuwa na rekodi nzuri mfululizo ya kutupia mabao mengi kuliko mchezaji mwingine yeyote barani Ulaya tangu mwanzo wa mwaka 2021.
Hata hivyo, tofauti na Messi ambaye amesaidia timu yake ya taifa Argentina kubeba Copa America (kombe la mataifa ya Marekani Kusini), Lewandowski hakufanikiwa kuipa heshima nchi yake Poland katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya.
Messi amefanya mahojiano maalumu na France Football, jarida ambalo linahusika na tuzo za Ballon D’or. Mahojiano hayo yamegusia mada mbalimbali.
Si kawaida ya Messi kuwa na mahojiano marefu na ya kina na vyombo vya habari. Hivyo, mashabiki wengi wa soka wametaka kufahamu alichokisema kuhusu masuala mbalimbali aliyoulizwa.
Sakata la kukataa jezi namba 10 aliyozawadiwa na swahiba wake Neymar Jr klabuni PSG
“Jezi namba 10 ni yake. Binafsi, nimekuja PSG kusaidia kutwaa mataji, na lilikuwa jambo la kiungwana sana na sikushangaa kwani namjua vyema Neymar. Ni rafiki yangu mkubwa na tulicheza pamoja klabuni Barcelona, na binafsi niliona ni vema zaidi kama atabaki na jezi hiyo, na ndiyo maana nilichukua jezi nyingine ambayo ni chaguo langu.”
Kuhusu yeye kulala chini ya ukuta wa PSG kwenye ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Manchester City
“Kwa wakati huo lilikuwa ni jambo sahihi kufanya, kwani tulikuwa tunaelekea kupata ushindi na hakukuwa na mtu mwingine aliyejitokeza kulala chini ya ukuta, hivyo nikaamua nifanye hivyo. Halikuwa jambo kubwa, sote tulitaka kupata ushindi, na kila mmoja wetu alitaka kuchangia chochote, na huo ndio ulikuwa mchango wangu kwa timu.”
Maoni yake juu ya kutajwa kwake kama mchezaji bora zaidi wa soka kuwahi kutokea
“Sijawahi kusema kuwa mimi ni mchezaji wa soka bora zaidi wa zama zote, huwa najaribu kushindana na mimi mwenyewe ili niimarike zaidi. Kutajwa kama mchezaji wa soka bora zaidi kuwahi kutokea ni kitu ambacho kinanipa hamasa kubwa, lakini ni kitu ambacho binafsi sikuwahi kukifikiria kwani hakina maana sana kwangu, hakiniongezei wala kunipunguzia lolote kiuwezo, na sijawahi kutamani niwe hivyo.”
Kuhusu yeye kuwa mfano wa kuigwa kwa wengine
“Sifahamu kama nachukuliwa kama mfano wa kuigwa na watu, sikuwahi kupenda kuwa hivyo, au hata kutoa ushauri kwa watu. Nilipigania matamanio yangu; mwanzoni ilikuwa ni kucheza soka la kulipwa, na baada ya kulifanikisha hilo nilipambana kujiboresha zaidi ili nifikie malengo ninayoyaweka kila mwaka. Kwa kipindi chote hicho, namshukuru sana Mungu kwani yeye ndiye aliyeamua niipate bahati hiyo ya kufanikisha malengo yangu.”
Kuhusu yeye kumpita Cristiano Ronaldo kwa idadi ya Ballon d’Or
“Siku zote nimekuwa nikipambana na nafsi yangu mwenyewe, huwa siangalii wachezaji wenzangu wanafanya nini. Mimi na Cristiano tumeendeleza ushindani wetu katika La Liga kwa miaka kadhaa.
“Hali hii imetusaidia sana kukua na kuendeleza kazi zetu lakini bila kufuatiliana. Nimekuwa nikishindana na nafsi yangu, kuimarika zaidi na si kwa ajili ya kuwa bora zaidi ya mchezaji mwingine yeyote.”
Mtazamo wake juu ya yeye kufananishwa na Diego Maradona
“Sijawahi kujilinganisha na Maradona, sijawahi pia kufuatilia mijadala inayonifananisha na Diego hata siku moja, ingawa kukosolewa kuliniumiza sana kipindi cha nyuma. Nilikuwa na wakati mgumu sana na timu ya Taifa lakini si kwa sababu hiyo.
“Mara kadhaa nimekuwa nikikasirishwa na ukosoaji dhidi yangu lakini hasira hiyo inabaki kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, hatimaye hili ni jambo binafsi. Ni upendo unaofanya timu kuwa imara zaidi. Kukwazana na kukasirikiana ni katika jitihada za kuwa bora zaidi. Hii haitokei kwangu tu bali kwa kila mtu.”