Finland yakumbwa na shamrshamra za mkesha wa Mei Mosi

Image by yle.fi

BAADA ya saa 12 kamili jioni tarehe 30 Aprili, mambo mitaani yamebadilika katika Jiji la Helsinki, Finland.

Shamrashamra za Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambayo huadhimishwa Mei Mosi kila mwaka, zimeanza.

Vijana kwa wazee, wakiwa wamevaa nguo za rangi mbalimbali, wengine wakiwa na kofia maalumu vichwani, wamejaza mitaa ya Helsinki katika mikusanyiko mikubwa, hasa maeneo ya wazi ya Hakaniemi Market Square.

Wengine wanakunywa bia, wengine wanakula pizza, wengine wanavuta sigara, wengine wanafurahia masimulizi ya wenzao.

Ni kama vile sherehe za Mei Mosi 2018 zimeanza. Wale ambao hawakuweza au hawakupenda kukusanyika maeneo hayo, wamejipangia sehemu za kukutana na rafiki zao kwa ajili ya mapochopocho.

Katika mikusanyiko mikubwa ya maeneo ya wazi, polisi wanakadiria kuwa leo kumekuwa na umati wa watu wapatao 80,000. Mwaka jana walikadiriwa kuwa na mkusanyiko wa watu 40,000.

Hata hivyo, haya ni maandalizi tu. Maadhimisho rasmi ni kesho tarehe 1 Mei 2018.

Yatakuwa maadhimisho yenye ladha ya kisiasa, yakianza na maandamano ya wananchi kutoka Hakaniemi hadi Kituo Kikuu cha Reli, katikati ya jiji. Ni mwendo wa kilomita zipatazo 2.3.

Viongozi kadhaa wa vyama vya wafanyakazi na vyama vya siasa wanatarajiwa kuhutubia waandamanaji hao.

Miongoni mwa viongozi hao ni Li Andersson, dada mwenye mvuto ambaye ni mwenyekiti wa Left Alliance, chama cha siasa cha mrengo wa kushoto. Vile vile, Li ni mbunge anayetokana na chama hicho.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa na wananchi wa kawaida wa hapa Finland wanasema Li anaweza kuwa waziri mkuu wa nchi hii katika miaka michache ijayo, maana nyota yake inawaka.

Like
4

Leave a Comment

Your email address will not be published.