Dar hadi Chato kupitia Roma: Magufuli ataka Kanisa Katoliki limuundie jimbo lake

WAHAYA na Wanyambo wana usemi kwamba “mtoto atukanaye wazee hatukani mtu mmoja.”

Usemi huu, ambao pia hutumiwa naWasubi na Wazinza (waishio katika maeneo ya Wilaya za Biharamulo na Chato) kwenye mkoa mpya ambao bado haujatangazwa, unaelekea kufafanua uhusiano mpya wenye shaka kati ya Rais Magufuli na Kanisa Katoliki, hasa pale anapojikuta anazozana na askofu mmojawapo kwa sababu zozote zile.

Hadi sasa Biharamulo ni sehemu ya Mkoa Kagera. Lakini katika siku kadhaa zijazo inaweza kutangazwa kuwa sehemu ya mkoa unaoandaliwa, utakaoitwa CHATO au Rubondo.

Lakini taarifa zilizopo zinasema kuwa uundaji wa mkoa huo haukamiliki bila kugusa mamlaka za Kanisa Katoliki.

Na hii inatokana na hulka ya kibabe ya Rais John Magufuli ambayo katika siku za hivi karibuni imetumika katika uamuzi wa kuvipa majina vituo mbalimbali vya umma majina ya rafiki zake, badala ya kuyaunda kupitia mifumo ya utawala.

Wanaojua wanatambua kuwa hulka hiyo sasa imemfikisha katika mgongano wa kimya kimya na itifaki za Kanisa Katoliki.

Vyanzo vyetu kadhaa kutoka Dar es Salaam, Chato, Bukoba na Vatican Roma vinatujulisha kuwa Rais Magufuli amekuwa anaomba (kwa kushinikiza) Kanisa limuundie Jimbo Katoliki la Chato.

Anataka uundaji wa jimbo hilo uende sambamba na uundwaji wa “mkoa wake” mpya kiserikali.

Sababu kuu ya shinikizo hilo ni yeye kutotaka kuendelea kuwa chini ya Jimbo la Rulenga-Ngara linaloongozwa na Askofu Severine Niwemugizi. Ana chuki ya kihistoria dhidi ya Askofu Niwemugizi, na amekuwa na mikwaruzano ya wazi naye tangu mwaka 2016 askofu huyo aliposhauri umuhimu wa katiba mpya, na mwaka jana alipohamasisha waamini wa jimbo lake kujikinga dhidi ya Corona wakati Rais Magufuli akisisitiza “hakuna Corona.”

Kwa sababu hiyo, hata katika ibada nyingi ambazo Magufuli alishiriki akiwa nyumbani kwao Chato, na kutumia mimbari kutangazia kanisa kuwa “hakuna Corona,” alitumia zaidi makanisa yasiyo ya Katoliki.

Kwa muda mrefu sasa, Magufuli amekuwa anakejeli maaskofu – hasa awapo na rafiki zake – akiwaita “miungu watu.” Na amekuwa anatumia urais wake kuagiza taasisi za serikali ziwashikishe adabu baadhi yao.

Halafu wanapokuwa matatani, yeye huwapigia simu binafsi za “kuwapa pole.” Anauma na kupuliza.

Hata masimango yake Jumapili iliyopita dhidi ya Askofu Mkuu Yuda Thadei Ruwa’ichi akiwa katika Kanisa la Mt. Petro, Dar es Salaam, ni sehemu ya “fujo zake za kimkakati” dhidi ya maaskofu.

Kwa miaka kadhaa amekuwa na chuki dhidi ya Kanisa Katoliki, jambo lililomfanya ahamehame makanisa. Akiwa waziri alijenga kanisa huko Chato na akalitoa kama zawadi kwa “madhehebu yote” ili walitumie kwa ibada zao, kwa kupishana.

Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara lilikataa kutumia kanisa hilo kwa sababu za kiteolojia. Lakini yeye alibeba uamuzi huo kwa chuki dhidi ya Askofu Niwemugizi.

Haikushangaza wanaojua pale Askofu Severine Niwemugizi aliponyang’anywa pasipoti na kuhojiwa uraia ndani ya mwaka wa kwanza wa kipindi cha kwanza cha urais wa Magufuli.

Hata aliporejeshewa pasipoti yake, baada ya kelele nyingi kupigwa, alitakiwa asiongee na vyombo vya habari kuhusu suala hilo.

Kufuatia waraka wa Kwaresima uliokemea ukiukwaji mkubwa wa haki za raia, uliotolewa na TEC mwaka 2018, Magufuli alidai (kwa watu wake) kuwa ulichochewa na kuandikwa na Askofu Niwemugizi. Na alidhamiria kuwakomesha hadi watambue kuwa “hakuna cha rais wa TEC,” bali yeye ndiye rais.

Sasa anataka atumie urais wake kujitenga rasmi na jimbo la Niwemugizi kwa kuundiwa jimbo lake la Chato.

SAUTI KUBWA inafahamu kuwa Magufuli alifikisha ombi lake kwa askofu mkuu mmoja aliye karibu naye. Chanzo chetu kutoka kanisani kinasema hata Balozi wa Vatican nchini alipoelezwa suala hilo alisema, “uundwaji wa jimbo hautokani na maombi ya rais bali utaratibu rasmi wa Kanisa.”

Mmoja wa viongozi waandamizi katika Baraza la Maaskofu Tanzania amesema, “bado hatujapokea rasmi ombi hilo.”

Lakini alisisitiza kuwa “tumesikia miong’ono kwamba JPM anataka jimbo lake. Canon Law inasema mamlaka ya kuanzisha jimbo yapo kwa Baba Mtakatifu. Anaweza kuanzisha, kuunganisha, kubadili, au kufuta majimbo.”

Hata hivyo, ili Baba Mtakatifu aamue, anategemea pendekezo lipelekwe kwake na baraza la maaskofu husika. Na baraza linapokea pendekezo kutoka kwa askofu anayetaka kuunda jimbo.

Kwa mantiki hiyo, ili Magufuli apate jimbo la Chato, lazima Askofu Niwemugizi awe amehusishwa, na aone sababu za kuwepo jimbo hilo, na apendekeze kwa Barazaa Maaskofu Tanzania.

Askofu mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema: “Si jambo la kawaida kiongozi wa serikali kuomba jimbo. Hawezi kiongozi wa serikali kulifanya kanisa ni mali ya mtu.”

Askofu Niwemugizi amethibitisha kuwa hajapelekewa pendekezo hilo.

SAUTI KUBWA inafahamu pia kwamba katika hali ya kutokubali kushindwa, Rais Magufuli alimtafuta askofu mwingine rafiki yake mwenye ukaribu mno na Vatican na kumsihi amsaidie.

Katika hali ya kushangaza, Rais Magufuli amesikika mara kadhaa akikejeli na kutishia kuhamia madhehebu mengine endapo ombi lake halitashughulikiwa atakavyo.

Chanzo chetu kimoja kutoka Chato kimesema: “Wakati wa Krismasi alimwalika askofu mmoja Mprotestanti na mkewe ili waje Chato kufanya ibada nyumbani kwake kwa sababu alikuwa hataki kwenda misa ya Katoliki. Tiketi ya ndege iliandaliwa na John Kijazi (sasa marehemu) kuwaleta askofu huyo na mkewe. Awali, alianza kwa kuwapa zawadi ya kiwanja huko Chamwino, Dodoma. Bahati mbaya safari ilikatishwa na Corona.”

Ili kuendana na mpango wa kupata jimbo jipya la Chato, Rais Magufuli amekamilisha mipango ya kuunda mkoa mpya wa Chato ambao unapendekezwa uitwe Rubondo, na makao yake makuu yatakuwa mjini Chato.

Mkoa huo utaundwa na wilaya mpya za Nyakanazi, Runzewe, Busanda, Muleba na Ngara. Anapendekeza Wilaya ya Biharamulo ya sasa iende mkoa mpya utakaokuwa mkubwa kuliko mikoa iliyouzaa.

Watafiti na washauri wa rais walimsihi acheleweshe kuutangaza kutokana na hali ya kisiasa nchini, hasa kwa kuwa watu wamekuwa wanalalamikia miradi mingi mikubwa inayoelekezwa Chato.

Awali ulikuwa utangazwe Januari 21, 2021. Manung’uniko juu ya upendeleo wa wazi kwa Chato yameongezeka siku za karibuni.

Mwakilishi wa SAUTI KUBWA aliyeko Dar es Salaam ameripoti kuwa hata mkakati wa juzi wa kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuiunda ndani ya Ilala ni mkakati wa kuwaandaa Watanzania kisaikolojia kuhusu anachotaka kufanya huko Chato.

Kuna orodha ya vitu vitakavyovunjwa na kuundwa, kupewa majina mapya na kufuta baadhi katika wiki chache zijazo ili kuonyesha kuwa uundwaji wa Chato ni sehemu ya mpango mkubwa. SAUTI KUBWA imebahatika kuona orodha hiyo kwa sharti la kutoichapisha kwa sasa.

Zipo taarifa pia kuwa ubabe na uthubutu wake wa kuiingilia Kanisa Katoliki, umeligawa kanisa hilo na kutokeza mivutano ya chini. Wapo maaskofu wanaomuunga mkono Magufuli kwa sababu za kimaslahi kuliko za kimaadili.

Na wapo wanaosimamia utume, maadili na miiko ya utumishi wao. Hawa wanasisitiza mipaka ya madaraka ya serikali katika mambo ya imani. Mjadala unaendelea.

Like
15