Corona sugu yatishia wasafiri kutoka Tanzania

WAKATI dunia ikisubiri kwa hamu kujua msimamo wa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya ugonjwa wa Corona, wasafiri kutoka Tanzania huenda wakatengwa zaidi baada ya kugundulika kwa virusi vya Corona vyenye “usugu.”

Kutokana na hali hiyo, wanasayansi wanaochunguza vimelea na virusi vya magonjwa ya mlipuko, wameshauri Shirika la Afya Duniani (WHO) kufuatilia zaidi na ikiwezekana kuweka zuio kwa wasafiri wanaotoka au kupitia Tanzania kuingia nchi zingine.

Ripoti iliyowasilishwa kwa WHO wiki iliyopita inaonyesha kuwa baadhi ya wasafiri kutoka ama waliopita Tanzania, wamegundulika na virusi vya Corona ambavyo ni “hatari zaidi na vyenye uwezo wa kukataa hata chanjo zinazotolewa.”

Kwamba virusi hivyo vinaonyesha usugu mara 10 zaidi ya virusi vilivogundulika kuwepo Afrika Kusini.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Krisp inaoshirikiana na WHO kufanya utafiri juu ya virusi, Profesa Tulio de Oliveira, amesema wamegundua baadhi ya wagonjwa kutoka Tanzania kuwa na virusi hivyo. Krisp ndiyo iliyogundua kuwepo kwa virusi vyenye usugu kutoka Afrika Kusini mwaka jana.

Inadaiwa na taasisi hiyo ya Afrika Kusini kuwa wasafiri watatu kutoka Tanzania ndio waliogundulika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo vya Corona. Walitoka Tanzania kupitia Angola.

Tanzania kwa muda mrefu, wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli, ilikataa kuwepo kwa virusi vya Corona, vinavyosababisha ugonjwa huo pia ukiitwa COVID-19. Magufuli alifariki Machi 17 na kuzikwa jana kijijini kwake Chato, mkoani Geita.

Mrithi wa Magufuli, Rais Samia, bado msimamo wake kuhusu Corona haujawa wazi, ingawa, kama ilivyokwa kwa mtangulizi wake, hajavaa barakoa kwenye mikusanyiko yote ya mchakato wa msiba wa Magufuli.

Rais Magufuli alikuwa na shaka na usalama wa barakoa, hasa kutoka nje ya Tanzania na alizuia nchi yake kujiandaa kwa chanjo. Alihimiza matumizi ya mitishamba na kujifukiza, huku akilazimisha maombi kwa Mungu, msimamo alioushikilia hadi anakutwa na mauti, huku kukiwapo madai ya kufariki kwa ugonjwa wa COVID-19.

Like
1