CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema Tanzania inapoteza kiasi cha shilingi trilioni 4 kila mwaka katika madini kwasababu ya kukithiri kwa rushwa, ukwepaji kodi, magen̈do na uhamishaji haramu wa fedha za mauzo ya madini nje ya nchi, kutokana na usimamizi mbaya wa sekta hiyo.
Kwamba, upotevu huo wa mapato unachangia kuchelewesha, kukwamisha na kurudisha nyuma kasi ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma wa chama hicho, Edward Kinabo, wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Masumbwe, Katoro na Geita Mjini jana, katika mfululizo wa mikutano ya Operesheni Chaumma for Change (C4C), iliyofanyika leo mkoani Geita.
Kinabo amesema ufisadi huo unafanywa na makampuni ya madini kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi na watendaji wasio waaminifu waliopo serikalini.
Akiichambua ripoti mpya ya Shirika la kimataifa la Global Financial Integrity, lenye makao yake makuu nchini Marekani, Kinabo alisema:
“Tarehe 30 mwezi Aprili mwaka huu, Shirika la Global Financial Integrity, limetoa ripoti inayothibitisha kuwa Tanzania inapoteza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 1.5, sawa na Shilingi Trilioni 4 za Kitanzania, kwasababu ya uhamishaji haramu wa fedha za madini nje za nchi. Fedha hizi zinapigwa kwasababu ya kukithiri kwa rushwa, ukwepaji kodi na uuzaji wa madini kwa magendo.”
Mwanasiasa huyo amedai kuwa taarifa ya kile kilichoitwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika sekta ya madini, iliyotolewa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, mbele ya vyombo vya habari mwezi Mei mwaka huu, inaonyesha kuwa waziri huyo amemdanganya rais na taifa zima, kwani makusanyo ya maduhuli yenye thamani ya Shilingi bilioni 902 ni madogo sana kulinganisha na fedha nyingi zinazopotea katika sekta hiyo.
“Tunapoteza fedha nyingi kwasababu ya ufisadi halafu Waziri anamdanganya rais, anaidanganya nchi eti tumefanya vizuri,” aliongeza Kinabo.

Akizungumzia thamani na tija ya fedha hizo kama zingedhibitiwa na kuelekezwa katika miradi ya maendeleo ya wananchi, Kiongozi huyo alisema trilioni nne zingeweza kujenga zaidi ya zahanati 11,000, kwa gharama ya zahanati moja milioni 358, na hivyo kumaliza kabisa shida ya zahanati kwa vijiji na mitaa yote nchini.
“Ukichukua trilioni 4 ukaenda kujenga vituo vikubwa vya afya vya ngazi ya kata utapata vituo viwili kwa kila kata, kwa kata zote zaidi ya 3,900 zilizopo nchini. Ukichukua Trilioni 4 ukasema unaenda kujenga shule nzuri, kwa gharama ya milioni 800, utajenga zaidi ya shule 5,000 nchi nzima. Ni maskini siyo kwasababu hatuna fedha, bali kwasababu tumeweka watu wasiojali madarakani,” aliongeza.
Aliwataka wananchi wa Geita kuiunga CHAUMMA katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani ili chama hicho kiweze kudhibiti rushwa, ufisadi na uhamishaji haramu wa fedha za madini nje ya nchi.
“Tushirikiane kuing’oa CCM madarakani. Tubadilishe maisha yetu, tuifanye dhahabu yetu ikalete thamani na mabadiliko katika maisha yetu,” alihitimisha.