CHADEMA WAUNGANA NA CCM KIBAMBA KUMKABILI KINABO WA CHAUMMA

WAKATI kukiwa na kila dalili kuwa Edward Kinabo atawania ubunge wa Jimbo la Kibamba kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) katika uchaguzi mkuu mwaka huu, hujuma dhidi yake zimeanza, zikiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Hujuma hizo zinaratibiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA katika jimbo, Ernest Mgawe, ambaye amesikika akisema heri mgombea wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) ashinde kuliko Edward Kinabo wa CHAUMMA. Baadhi ya watu wake wa karibu wanadai tayari anasaidia CCM dhidi ya CHAUMMA.

Edwa Kinabo akihutubia katika mkutano mmojawapo wa CHAUMMA

Kinabo, ambaye ni Katibu wa Sekretariati ya CHAUMMA Taifa na pia ni Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma wa chama hicho, hajatangaza rasmi, lakini amekuwa katika mizunguko na vikao vingi vya kimkakati ndani ya jimbo la Kibamba, vyenye mwelekeo wa kuandaa wagombea udiwani na wananchi kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Mmoja wa watu wa karibu na Mgawe, ambaye pia ni mfuasi wa Kinabo katika harakati hizi, amemnukuu mwenyekiti huyo wa CHADEMA akisema:

“Ni kheri CCM ishinde kuliko kuacha Kinabo achukue jimbo letu.”

SAUTI KUBWA imeona mawasiliano ya Kiongozi huyo wa CHADEMA katika kundi sogozi la chama, akiandika:

Habari ninazo toka jana, kwamba kuna kikundi cha wahuni, kikiwa na mgombea msaka tonge, Kinabo, pamoja na takataka zao zingine, wamekuwa wakipita kwenye kata zetu. Lengo lao ni kuandaa wagombea. Jana walikutana na Magessa. Tusikubali achukue jimbo letu.

Baadhi ya viongozi na makada mbalimbali wa CHAUMMA na CHADEMA wanaomuunga mkono Kinabo, wanasema Mgawe amekuwa anawapigia simu na kuwashawishi wamsaliti Kinabo na kuhakikisha anashindwa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Mmoja wao,  Mapendano George, ambaye ni kada wa siku nyingi wa CHADEMA, amesema:

“Siwezi kumsaliti Kinabo. Ni kiongozi mwenye akili kubwa na dhamira ya kweli ya kusaidia wananchi. Ni mkazi wa jimbo hili anayezijua vema kero za wananchi na mwenye ufumbuzi wà uhakika. Jimbo la Kibamba linahitaji mtu wa sampuli ya Kinabo, mjenzi mahiri wa hoja, mbunifu, mchambuzi na mfuatiliaji makini wa maendeleo.

Kiongozi mwingine wa CHADEMA ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema:

Mimi nauguliwa na mzazi wangu na anajua lakini hatujawahi kuzungumzia suala hilo, lakini Mgawe aliposikia Kinabo amefanya kikao na mimi, ndiyo ameanza kunipigia masimu na kuahidi kunisaidia pesa za matibabu.”

Duru za kisiasa zinadai kuwa Mgawe, aliyegombea ubunge wa Kibamba 2020 na kushindwa, anahofia kuwa Kinabo anaweza kushinda ubunge wa jimbo hilo, hali itakayompa wakati mgumu wa kugombea ubunge hapo baadaye katika jimbo hilo lenye rekodi ya muda mrefu ya kuwa na wapiga kura wengi wa vyama vya upinzani.

SAUTI KUBWA inatambua kuwa miaka ya nyuma, Kinabo ndiye aliyekuwa meneja wa kampeni na mwanamikakati wa John Mnyika katika uchaguzi wa 2005, 2010 na 2015. Ni mtu mwenye uzoefu pia wa kuhudumu katika Ofisi ya Kambi ya Upinzani Bungeni, akiwa ameshiriki kuchambua sera, bajeti na mipango ya nchi na kuandaa hoja na hotuba za wabunge wa Kambi ya Upinzani bungeni.

Katika kusisitiza hili, mmoja wa wafuasi wake hapo jimboni, amesema:

“Kinabo ni mtu mwenye uwezo mkubwa, lakini kwa muda mrefu amekubali kutumika kama daraja la kuvusha na kusaidia wengine kwa maslahi ya wananchi. Sasa ni zamu yake.”

Kiongozi mwingine wa CHADEMA wa Kata ya Msigani, kwa sharti la kutotajwa jina, amesema: “Mgawe anaujua uwezo huo mkubwa wa kisiasa alionao Kinabo, ambao ulichangia katika kumwezesha yeye pia kuwa diwani. Kinabo anazijua vema siasa za jimbo hili na hicho ndiyo haswa anachohofia Mgawe.

Akaongeza:

Mgawe anadhani yeye ndiye mwanasiasa wa upinzani mwenye hati miliki na jimbo hili. No Reforms, No Elections, haina maana ya kusaidia CCM, lakini yeye anasaidia CCM kwa maslahi yake binafsi, yaani anataka eti CCM wauchukue huo ubunge halafu wamtunzie aje auchukue yeye baadaye bila kujali kuwa wananchi wanataabika kwa kukosa mbunge mahiri. Mimi ni Chadema damu, lakini siungi mkono huo ujinga.“,

Inaonekana hata wanachadema wenyewe tayari wamegawanyika kuhusu jambo hili.

Edward Kinabo akiwa na baadhi ya viongozi wa CHAUMMA wa Jimbo la Kibamba katikati ya wiki juma hili

SAUTI KUBWA imemtafuta Mgawe ili kupata maoni yake. Hadi tunaenda mitamboni alikuwa hajapatikana.

Kinabo alizungumza na mwandishi wetu akathibitisha kusikia tetesi za hujuma dhidi yake, lakini akasita kutoa kauli kama anagombea ubunge katika Jimbo la Kibamba.

Amesema: “Na mimi nimesikia tu. Nimeshangaa kusikia kuna binadamu mwenzangu ana roho mbaya kama nyoka wa mdimu. Unajua…Nyoka wa mdimu hali ndimu, lakini ukienda kuchuma ndimu, kama yupo lazima akugonge akuue. Sasa kama kuna mtu chama chake hakishiriki uchaguzi, lakini yeye hataki mwenzake anayegombea ashinde, huyo si ana roho mbaya sana kama nyoka wa mdimu. Imagine…

Alipoulizwa kama anagombea ubunge, Kinabo alicheka, halafu akasema, “nitasema baadaye.”

Hata hivyo, SAUTI KUBWA linafuatilia harakati za kisiasa katika jimbo hilo, na linafahamu kuwa Kinabo amekuwa anafanya vikao vya maandalizi ya kugombea ubunge.

Like