CCM waanza kununua vitambulisho vya wapiga kura

KATIKA maeneo mbalimbali nchini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeingiwa na hofu ya kushindwa, na sasa kimebuni mbinu ya kujinusuru kwa kununua vitambulisho vya kupigia kura.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, baadhi ya majimbo yamethibitika kuwa magumu kwa chama tawala.

Wimbi la upinzani, hasa kutoka kwa Chadema (Tanzania Bara) na ACT-Wazalendo (Zanzibar), limekuwa kubwa kadiri mgombea urais Tundu Lissu anavyozidi kutembelea mikoa mbalimbali na kuvuta maelfu ya mashabiki huku akitoa hotuba zenye mguso kwa wananchi. Awali, CCM waliamini kuwa kazi ya kampeni ingekuwa rahisi kwani walijiaminisha kuwa manyanyaso, ukatili, vitisho na mapigo mazito mfululizo dhidi ya wapinzani kwa miaka mitano vingetisha na hata kuua upinzani kabla ya 2020. Hali imekuwa tofauti.

Taarifa za matukio ya ununuzi wa vitambulisho vya wapiga kura zineripotiwa katika majimbo mengi nchini. Kazi hiyo inafanywa usiku ikisimamiwa na watendaji wa kata na viongozi wa CCM wa maeneo husika wakishirikiana na wagombea.

Kwa mfano, katika Jimbo la Kawe, Dar es Salaam, kuna kikundi kinajiita “timu ya ushindi” ya mgombea ubunge wa CCM, Josephat Gwajima, ambacho tangu mwanzo wa wiki hii kimekuwa kinapita mitaa kadhaa (mchana) na kukutana na wananchi, hasa vijana wanaodaiwa kuwa ni mashabiki au wanachama wa vyama vya upinzani.

Kila wanapokutana na vijana hao wanawashawishi kwa fedha ili wawauzie vitambulisho hivyo kwa lengo la kupunguza nguvu ya ushindi kwa mgombea mwenye nguvu katika jimbo hilo, Halima Mdee wa Chadema.

Kila kitambulisho kimewekwa bei ya Sh. 50,000. Wengine wanaviuza, kwa sababu ya dhiki, wengine wanagoma.

Katika mzunguko wao huo, wanaongozana na mtu moja ambaye hutumia simu yake ya mkononi kuwatumia fedha wale wote wanaokubali kuuza vitambulisho vyao.Katika Jimbo la Kawe, mchuano wa ubunge ni mkali zaidi kulio majimbo mengine ya Dar es Salaam, baada ya kuwa na upekee wa kuwakutanisha wagombea maarufu zaidi – Gwajima wa CCM na na Halima wa Chadema.

Mbinu nyingine inayotumiwa na Gwajima ni kuwaomba na kuwapa fedha maaskofu wapatao 70 wa makanisa ya “kiroho” Dar es Salaam ili wamsaidie kumnadi makanisani mbeya waamini wao.

Maaskofu hao, wa mara ya kwanza walikutana Alhamisi iliyopita katika Hoteli ya Piccolo, iliyoko Kawe jijini Dar es Salaam.

Taarifa zinaeleza kuwa lengo la mkutano huo lilikuwa kuomba viongozi hao wa kiimani kupitia makanisa yao kusaidia Gwajima apate kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu.

Kikao hicho kilichoanza saa 5.12 asubuhi, kilianza kwa sala na baadaye wasaidizi wa Gwajima waliendelea na ratiba. Gwajima alifika hotelini hapo saa 4.49 na kwenda moja wa moja kwenye mkutano huo ambao awali ulipewa jina la “mkutano wa kuombea amani na Uchaguzi 2020.”

Akishuka katika gari lenye rangi ya kijani aina ya Toyota Prado ambalo lilikuwa limefunikwa namba za usajili kwa bendera ya CCM, alisalimia waliompokea na kupelekwa ukumbini.

Baada ya mkutano huo, viongozi hao wa kiroho walipewa bahasha za khaki zilizofungwa. Hata hivyo, Gwajima amekanusha taarifa za ununuzi wa vitambulisho akidai kuwa hawezi kufanya hivyo kwa kuwa yeye tayari ni mshindi. Anasema “mtumishi wa Mungu ana hofu ya Mungu, hivyo anaamini tayari ameshinda.

Haki hiyo imeripotiwa pia katika majimbo ya Kalenga, Ubungo, Moshi Vijijini, Vunjo, na Kigamboni. Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wamelalamika kuwa wanabughudhiwa usiku kwa kutembelewa na viongozi wa serikali na kuombwa wakabidhi vitambulisho vyao ili “vihakikiwe.”

Mkoani Songwe, chama tawala kimemtumia waziri wa kilimo ambaye kwa kutumia maofisa wake anagawa mbolewa kwa wananchi baada ya kukusanya vitambulisho vyao vya kupigia kura. Kampuni ijulikanayo kama YARA ndiyo inatumika, na tukio la hivi karibuni lilikuwa la tarehe 26 Septemba. Ili upewe mbolea sharti utoe kitambulisho cha mpiga kura, jambo ambalo tayari linabeba taswira ya rushwa.

Mahali pengine, wanagawa chandarua bure kwa wale tu wanaowapatia shahada za kupigia kura.

Wachambuzi wa masuala ya siasa, ambao hawakutaka majina yao yatajwe wamesema kuwa CCM kinatoa rushwa ya wazi, na kwamba kinatumia watendaji wa serikali kufanya ufisadi huo.

Mmoja wa makada wa CCM aliyezungumza na SAUTI KUBWA amekiri: “Unashangaa bure, kwani hii si mara yetu ya kwanza kufanya hivi. Bila hivi ushindi kwetu ni mgumu kwa kuwa tunatambua nguvu ya upinzani. Wao wana nguvu ya umma, sisi tuna nguvu ya serikali. Lazima tutitumie.”

Like