CCM INATAJIRISHA WACHINA – MBOWE

Ataja kampuni zao 10 zilizochuma Trilioni 11 za miradi ya barabara, huku Watanzania wakiambulia Bilioni 633 tu.

Alia na rushwa, aongoza maandamano makubwa Bukoba

Na Edward Kinabo, Mwana wa Gombera

FREEMAN MBOWE, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ameibua kashifa nzito dhidi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), akisema imekuwa ikizipa kampuni za China kazi nyingi za ujenzi wa barabara, zenye thamani kubwa, huku ikiziminya kampuni za Kitanzania, licha ya kuwa na uwezo wa kutekeleza kazi hizo.

Amesema kampuni zote za Kitanzania, zilizojenga barabara ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita, kuanzia mwaka 2014 hadi 2024, ziliambulia kupewa miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 633 pekee, wakati kampuni za Kichina zilipewa miradi yenye thamani ya Shilingi trilioni 11, ikiwa ni mara 17 zaidi ya thamani ya miradi iliyotolewa kwa kampuni za ndani.

Mbowe, ameyasema hayo leo, wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Bukoba, mkoani Kagera, katika mkutano wa hadhara, uliotanguliwa na uzinduzi wa awamu ya pili ya maandamano ya chama hicho.

“Na sifa kubwa ya Wachina kwenye kupewa kandarasi huwa ni rushwa. Na Wachina wanajenga barabara ambazo ni chini ya viwango. Shauri ya kutoa rushwa kwa viongozi wetu, baada ya miaka mitatu, minne, unakuta barabara ina matundu, ina mashimo. Hakuna barabara imejengwa Tanzania kwa kipindi cha 10 iliyopita, ikakaa zaidi ya miaka miwili bila kuanza kufanyiwa repair (ukarabati)….kwasababu Wachina wana sifa ya kutoa rushwa kwa viongozi wa serikali ya Chama cha Mapinduzi,” aliongeza.

Miongoni mwa kampuni 10 za Kichina alizotaja ni pamoja na kampuni ya China Civil Engeneering Construction Corporation (CCECC), ambayo ndani ya miaka 10, imepewa zabuni za kujenga barabara, zenye thamani ya shilingi trilioni 5.6.

“Kampuni moja ya Mchina imepewa trilioni 5.6 lakini kampuni za Kitanzania zote, hata trilioni moja haijafika,” alisema Mbowe.

Aliongeza kuwa kampuni hizo za kigeni zinapokuja nchini huwa hazileti mtaji bali hupata fedha za ujenzi hapa hapa nchini na huchota fedha za kupeleka kwao.

Alisema, serikali yenye akili, angalau ingezitaka kampuni za kigeni kuingia ubia na kampuni za Kitanzania, ili kujenga uwezo na uzoefu wa kampuni za ndani badala ya kuwapa wageni karibu kazi zote wageni.

“Angalau wagawane hisa ya 60% kwa 40% ili baadhi ya faida zibaki kwenye kampuni zetu, baada ya miaka 10 tuseme hatutumii tena kampuni za nje, tunatumia kampuni za watoto wetu kwasababu tayari wamepata uzoefu,” alisema Mbowe na kushangiliwa na maelfu ya wakazi wa Bukoba.

Akitumia maneno ya “watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa, Mbowe alisema, Serikali ya CCM, inaangamiza Watanzania kwa kushindwa kulinda maslahi yao na kuigeuza nchi yao kuwa shamba la wageni.

“Taifa lolote linalojitambua, wajibu wake wa kwanza ni kunyanyua watu wake. Ukinyanyua kampuni ya kijana wa Kihaya, fedha inakuja Bukoba, watoto wanasoma, mababu na mashangazi wananeemeka. Lakini ukimpa Mchina, Mturuki, Mwarabu, fedha watapeleka kwao, itasaidia watu wao,” alisema.

Kwasababu hiyo, alihitimisha kuwa Serikali ya Chadema, ikiingia madarakani, itasitisha mara moja kile alichokiita ujinga wa kutoa kandarasi kwa kampuni za kigeni na kuacha kampuni za Kitanzania zikifa njaa.

Kwamba, Serikali ya Chadema itakomesha utaratibu huo, kwani una madhara makubwa kwa uchumi wa nchi na ustawi wa watu, ikiwa ni pamoja na kusababisha mitaji kuhamishwa kutoka nchini kwenda kwenye mataifa ya watu wengine.

Mkutano huo, ulihutubiwa pia na Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekia Wenje, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA), John Pambalu, Katibu wa Sekretarieti, Julius Mwita, Kada wa Chadema, Sheikhe Ally Kadogoo, Mwenyekiti Mpya wa Chadema Mkoa wa Kagera, Gratian Mukoba, Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Kagera, Magreth Mugyabuso na viongozi wengine wa chama hicho.

Like