WAKATI Tanzania ikidai kuwa haina ugonjwa wa Corona, imegundulika kuwa wananchi wa mikoa ya Kagera na Dar es Salaam ni miongoni mwa wengi walio hatarini kuambukizana ugonjwa huo iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa, kwani hadi sasa tayari kuna watu wengi wameathirika, na wengi wao hawajui kuwa wana virusi vya Corona.
Taarifa za uhakika kutoka katika Hospitali ya Mkoa Kagera iliyopo mjini Bukoba, zinasema kuwa hadi Alhamisi tarehe 24 Desemba 2020 hospitali hiyo ilikuwa wagonjwa 26 waliothibitika kuwa na Corona.
SAUTI KUBWA inafahamu kuwa mganga mkuu wa mkoa ametoa taarifa hiyo kwa mamlaka iliyo juu yake, na tayari hatua ya kwanza imechukuliwa, kwa agizo la Katibu Mkuu Wizara ya Afya, kupeleka kikosi kazi Kagera ili kufanya uchunguzi katika hospitali kadhaa za mkoa huo.
Vyanzo vyetu katika hospitali hiyo, vikiwa ni pamoja na madaktari, wauguzi na baadhi ya ndugu wa wagonjwa hao, vimethibitisha hatari inayolikumba taifa katika mazingira ambayo yanazuia wagonjwa, wahudumu na ndugu kusema ukweli juu ya Corona.
“Leo tunao wagonjwa 26 ambao baada ya vipimo wamethibitika kuwa na Corona. Tukiendelea kukaa kimya, wataugua wengine wengi na watakufa kimya kimya. Nadhani utaratibu huu unapaswa ukomeshwe ili watu wawe na taarifa, wajihadhari, na watibiwe kwa uhuru na uwazi kama wagonjwa wengine,” alisema daktari mmoja kwa sharti la kutotajwa jina.
“Tunaogopa. Hii nakueleza kwa kuwa nakuamini, na kelele hizi zinaweza kusaidia wakubwa na watu wengine kubadili mwenendo na kunusuru taifa, lakini kwetu sisi ni siri kubwa, haturuhusiwi kusema, maana itaonekana tunapingana na rais. Lakini tatizo lipo, watu wanaugua, wengine wanapona na wengine wanakufa kizembe tu kwa sababu ya matamko ya kisiasa,” alisema muuguzi mmoja katika hospitali ya Bukoba, naye kwa sharti la kuhifadhiwa jina lake.
Mkoa wa Kagera unapakana na nchi za Uganda na Rwanda ambazo katika siku za hivi karibuni zimekuwa na ongezeko la wagonjwa wa Corona.
Kutokana na kauli ya Rais John Magufuli, kwamba “Tanzania haina Corona,” na agizo lake kwa wizara kuacha kutoa takwimu, mamlaka za afya zimekuwa zinagoma kutoa kauli ya wazi kuhusu maambukizo haya, jambo ambalo ni hatari kwa afya za watu.
Taarifa zinaeleza kuwa wagonjwa wenye dalili za Corona wapo wengi katika hospitali kadhaa nchini, wanapatiwa matibabu kimya kimya. Wengine wanafariki dunia. Taarifa za wagonjwa hao zinabaki kwa ndugu na madaktari kwa sababu ya hofu ya kuchukuliwa hatua na vyombo vya dola.
Siku chache zilizopita, SAUTI KUBWA iliripoti kuwa wagonjwa wengi wa Corona katika jiji la Dar es Salaam wanalazwa katika hospitali za Aga Khan, Hindu Mandal na Rabinisia, lakini madaktari na ndugu wanaogopa kutoa taarifa za wazi.
Wakati hali ikiwa hivyo, huku taarifa za wataalamu wa afya duniani zikizungumzia ugunduzi wa chanjo ya Corona ambayo imeanza kusambazwa katika nchi mbalimbali, serikali ya Tanzania imesema haina mpango wa kuagiza chanjo hiyo kwa maelezo kuwa “hakuna ugonjwa wa Corona nchini.”
Msimamo huo wa awali umetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alipoulizwa endapo serikali ina mpango wa kuagiza chanjo hiyo. Alijibu kwa kifupi, “hapana!”
Kutokana na msimamo huo, zaidi ya Sh. Bilioni 432, hazitatumika kuagiza chanjo ya ugonjwa huo unaoendelea kuisumbua dunia kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kugundulika huko Wuhan, China, na kusambaa maeneo mengi.
Chanjo ya ugonjwa huo iliyothibitishwa na mataifa makubwa na kuanza kutumika, inagharimu kati ya Sh.12,000 hadi 90,000 kutegemea na ubora wake na kiwanda kinachozalisha.
Nchi zilzoanza kutoa chanjo hiyo kwa watu wake ikiwamo Marekani, imekadiria kuchanja asilimia 60 ya watu wake, kiwango ambacho kinaaminika kutumiwa na nch zote. Tanzania ina watu karibu milioni 60, hivyo asilimia 60 ni watu milioni 36, idadi ambayo ingepangwa kupata chanjo hiyo.
Tayari Kenya, Uganda na nchi zingine za Afika, zimeagiza chanjo ya ugonjwa huo kutoka Marekani ili kutoa chanjo hiyo kuzuia maambukizi zaidi. Kenya imetangaza kuagiza dozi milioni 24 ambazo zitaigharimu nchi hiyo zaidi ya Sh. bilioni 200 za nchi hiyo.
Umoja wa Ulaya (EU), Marekani na mataifa makubwa na tajiri, zimepitisha na kuanza kutumia chanjo iliyotengenezwa na viwanda vikubwa vya dawa vilivyoungana kuibua chanjo hiyo. Viwanda hivyo ni Pfizer ya Marekani na BioNTech ya Ujerumani.
Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli imetangaza kwamba Tanzania hivi sasa haina maambukizi ya Covid-19 baada ya kuondolewa kwa nguvu za maombi kwa Mwenyezi Mungu. Watanzania walifunga na kuomba kwa siku tatu mfululizo Juni, mwaka hu una baada ya hapo ilitangazwa kuwa nchi hiyo ya Afrika mashariki haina tena ugonjwa huo.
Tanzania ilizuia kutanganzwa kwa takwimu za maambukizi, kupima n ahata vifo vya ugonjwa bila kueleza sababu zozote za msingi, ingawa wachambuzi na wachunguzi wa masuala ya afya na uchumi anadai ilitokana na sababu za uchumi hasa, kwani kuendlea kutangaza kungeogopesha watalii na kusababisha biashara ningi kusimama.
Hadi zuio hilo linaanza kutekelezwa Aprili 29, maka huu, tayari kulikuwa na taarifa za serikali kwamba watu 21 walifariki kwa ugonjwa huo na kwamba maambukizi yalikuwa 509 tu, idadi ambayo imekuwa ikipingwa na watu na taasisi nyingi zinazfuatilia masuala ya ugonjwa huo.