BARUA YA WAZI KWA RAIS SAMIA (3)

Rais Samia Suluhu Hassan

Hii ni sehemu ya tatu ya barua hii, ikijadili muktadha mpana wa kiuchumi kwa kutazama suala la mkataba wa bandari kati ya Tanzania na Dubai. Endelea.

UCHUMI NA MAENDELEO

Mheshimiwa rais, kama ujuavyo, kwenye uchumi kama ilivyo kwenye siasa, maabara yetu kuu ni historia. Ni historia ambayo hutupatia zana za uchambuzi( economic assessment tools) kuhusu tulikokuwa, kwa nini tuko hapa tulipo na ipi mipango yetu ya baadae. Ni historia hiyo inayotusaidia kujua, kwa mfano, kwa nini wengine walikosea hata kama walitumia njia tunazokubaliana nazo kuwa ni njia za kitaalumu.

Hapa nchini kwetu, tumetafsiri misingi ya uchumi wa soko kwa njia ambayo inakinzana na misingi halisi ya soko. Tafsiri korofi zaidi tuliyoifanya, ni kubadili maana ya uchumi, mfumo wa uchumi na maendeleo.

Tumefikiri, tumepanga na kutekeleza kwa kutumia tafsiri hizo korofi. Kwetu, Maendeleo yamekuwa miundombinu ya kiuchumi na kijamii hata pale miundombinu hiyo inapokuwa haina uwezo wa kuongeza tija(total factor productivity) kupitia ukuaji wa uchumi. Na kwa msingi huo, tumenyonya uchumi na kuudhoofisha mno kwa kiwango ambacho tumefanya mfumo wa uchumi kuwa tegemezi kwenye soko la mitaji ya dunia hata kama soko hilo linatengeneza zaidi utegemezi wa uchumi wetu.

Mheshimiwa rais, kuwa na mfumo wa uchumi unaokua kwa uhalisia ni lazima uwekeze kwenye uchumi ambako watu wako wapo na upime mabadiliko ya kiuchumi kupitia viashiria hivyo kwani hiyo ndiyo sehemu kuu ya kuleta maendeleo ya nchi.

Maeneo ya uchumi ambako Watanzania wako ni kwenye kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara ndogondogo, ubunifu na sanaa .Watanzania wako kwenye ualimu, udaktari, ufundi, ushonaji na useremala kwa kutaja maeneo machache. Watanzania hawako(kiuchumi )kwenye madaraja, ndege kubwa kubwa, majengo marefu mijini, makampuni makubwa ya kuwekeza bandarini, makampuni makubwa kwenye migodi yetu ya madini au barabara na madaraja ya tozo.

Miundombinu ya kiuchumi inakuwa sehemu tu ya mzunguko wa wa maendeleo ya kiuchumi wenye kuwajali watu( virtuous cycle of economic development) ikiwa watu wako kwenye uchumi halisi wa maisha yao kwenye maeneo niliyotaja. Mzee Yoweri Kaguta Museveni aniuita uchumi huu The real economy.

Nje ya hapo, matokeo yake ni mzunguko wa umaskini kwenye uchumi( viscious cycle of poverty). Toka tulipobuni Dira 2025, tulifanya hiki ninachokisema. Dira hii inabeba mkanganyiko huu na kwenye kuutekeleza tumenyima chakula uchumi(economy) na kulisha ambacho tumekiita maendeleo (We have starved the real economy to feed the convoluted meaning of development).

Mheshimiwa rais, hizo siyo hoja tu za vitabuni. Ni hoja ambazo ni dhahiri kwenye uchumi kwa takwimu na matokeo.  Naomba nitaje mambo kadhaa muhimu ambayo yamejitokeza kuthibisha ukweli huu.

Mosi, ukuaji hafifu wa uchumi unaolipa kodi. Kati ya mwaka 1998-2021, miundombinu ya kiuchumi imechangia kati ya asilimia moja(1%) na asilimia tatu tu(3%) kwenye ukuaji wa uwiano kati ya pato ghafi(GDP) na kodi.( Tax/GDP ratio).

Ndiyo maana kwa miaka kumi na moja(11) iliyopita, pamoja na uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya kiuchumi, wastani wa kodi na pato ghafi umekuwa ni asilimia kumi na moja tu(11%) hata kama namba za ukuaji wa uchumi zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia mia moja na sitini(160%).

Pili, kodi za umaskini(poverty tax/ penalty poverty) imeongezeka kadiri uwekezaji wa miundombinu unaodhoofisha uchumi halisi unavyoongezeka. Poverty Tax ni ile gharama ya ziada ambayo watu maskini hulipia zaidi huduma na bidhaa kuliko watu matajiri kutokana na mazingira waliyomo.

Kwa mfano gharama za nyumba, usafiri, gharama za kulipia choo, gharama za maji na mambo ya aina hiyo. Kati ya mwaka(2014-2021), watu maskini mijini wanalipa asilimia mia tatu(300%) zaidi ya watu matajiri kupata huduma ya choo. Hii inatokea hata pale ambapo miundombinu ya jumla mjini imeimarika. Kwenye kipindi hichohicho gharama za taka zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia mia moja sabini(170%) kwenye maeneo ya watu maskini ambao pia idadi yao haijapungua.

Tatu, mfumuko wa bei(silent inflation) imekuwa ikiongezeka kadiri miundombinu ya kiuchumi inavyoshamiri. Silent Inflation ni ule mfumuko wa bei ambao unapimwa kwa muda mrefu kwa kulinganisha viwango vya mfumuko wa bei na viwango vya kuongezeka mishahara.

Kati ya mwaka (2015-2022), kiwango cha mfumuko wa bei ni asilimia ishirini na nne nukta tano(24.5%), wakati ongezeko la mishahara kwenye sekta ya umma kwenye kipindi hicho, ilikuwa asilimia moja nukta saba tu (1.7%). Ni kipindi hiki ambapo hoja za kuwa hatuwezi kuongeza mishahara kwa sababu tunajenga miradi ya kimkakati zilishamiri.

Hata pale ambapo serikali yako Mh.Rais; iliposema kuwa inaongeza “allowances”, siyo watumishi wengi na hasa wa chini wamefikiwa. Ukweli ni kuwa; kwa sababu ya shughuli nyingi kwenye uchumi zinazohusu miradi ya kimkakati watumishi wa daraja la juu kati ya mwaka(2021- 2023), “allowances” zao zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia mia tatu na kumi(310%) ya mishahara yao. Hawa siyo walimu kwenye sekta ya elimu, wala wauguzi kwenye sekta ya afya.

Mifano kuhusu haya ni lukuki na inaweza kuanishwa kwa urefu zaidi.

Aidha, kuwa na uchumi ambao umeondokana na dhana hafifu za maendeleo zinazodhoofisha misingi ya uchumi, mambo makuu mnne(4) ni ya lazima;

  1. Mfumo wa uchumi unaoendeshwa kwa kutegemea ongezeko la tija badala ya ongezeko la tija kwenye makampuni ambayo siyo sehemu ya uchumi wako.

Hapa ni kusema kuwa; tija inakuwa kubwa kwenye uchumi halisi badala ya kutegemea faida kiduchu zinazotokana na kuongezeka kwa tija kwa makampuni yaliyoko kwenye uchumi ili kuimarisha tu miundombinu ya kiuchumi. Kwa mfano, uchumi wetu tija yake imekuwa hafifu lakini tija kwenye makampuni yaliyokuja kujenga miundombinu kwenye sekta za mawasiliano, usafiri, madini au ujenzi ikishamiri.

Japo hili si tatizo la Tanzania tu, lakini ni tatizo kubwa kwa nchi maskini kama Tanzania. Na sasa zipo jitihada duniani za kuzihimiza nchi kama zetu kulitazama jambo hili kwa kina kwenye mijadala ya tija kwenye uchumi.

Mh Rais, ikukupendeza watake wasaidizi wako wakuletee kitabu kipya cha Daron Acemoglu kwa jina la; Power and Progress: Our Thousand- Year Struggle Over Technology and Prosperity. Kwenye kitabu hiki, Acemoglu na Simon wanaonesha kuwa, tunawekeza kwenye miundombinu kwa hoja za kuvutia teknolojia ili tuongeze tija, zinaweza kuishia kuongeza tija kwa kampuni lakini siyo mfumo wa uchumi kwa upana wake. Na hii ni hoja yenye utafiti kwa miaka elfu moja(1000) iliyopita.

  1. Ajira na Vipato.

Mfumo wa uchumi unaolenga uchumi halisi ni sharti uwe unaojibu hoja ya kuongeza ajira na vipato vya watu au unaotengeneza mazingira zaidi ya ajira na vipato. Hiki hakijawa kipaumbele kwenye tafsiri yetu ya mfumo wa uchumi na maendeleo. Miundombinu ya uchumi haijaweka mazingira ya kufikia lengo hili na badala yake imekuwa ni kwa ajili ya kuweka mazingira bora ya biashara.

Kwenye kufanya hivi, tumesahau kuwa mazingira bora ya biashara ni zaidi kwa wale ambao tayari wana mmitaj (mitaji kwa maana ya kiuchumi; yaani nguzo za kuwezesha uzalishaji). Ili kufikia hapo, swali kuu ni; Watu wangu wako wapi?  na siyo; Sekta zangu ziko wapi?.

Ukijiuliza sekta, kama ambavyo tumekuwa tukifanya; utavutia uwekezaji kwenye miundombinu bila kujali kama miundombinu hiyo ina matokeo tarajiwa kwenye uchumi halisi. Aidha, utajikuta unalenga faida za kihasibu kwa wale tayari wenye mitaji, badala ya faida za kiuchumi kwenye mfumo wa uchumi na hapa kwa maana ya ajira na vipato.

Hii ndio maana uwiano kati ya mtaji unaohitajika kuzalisha ajira moja( capital/ labor) ni mkubwa na umekuwa unakua kwa kasi kuliko ilivyokuwa miaka thelathini iliyopita. Kimsingi uwiano huo umepanuka mara thelathini na tatu zaidi kwenye kipindi hicho ukilinganisha na nchi kama Vietnam, Bangladesh na hata India kwenye sekta kama ya viwanda vya nguo na mazao ya ngozi.

Ni kwa sababu hiyo, nchi yetu inaagiza zaidi ya pea milioni ishirini na tatu( 23) za viatu kwa mwaka hata kama tuna mifugo wengi zaidi ya nchi tunakoagiza viatu hivyo. Ni kwa sababu hiyo uwezo wa tija kwenye sekta ya kilimo uko chini mara thelathini na nne zaidi ya nchi kama Misri hata kama iko kwenye jangwa.

  1. Uwekezaji wa ndani(DDI’s-Domestic Direct Investment).

Lengo la kuwa na uchumi   halisi ni kuongeza uwezo  wa ndani wa uchumi kuwekeza kwenye (Domestic Direct Investment). Kufika hatua hii, lazima kuwepo uhusiano mkubwa kati ya uwekezaji kwenye miundombinu ya kiuchumi na uchumi halisi.

Nje ya uhusiano huo, uchumi wa ndani kwa maana ya “DDIs” hulazimika kuwa viambata(appendages) vya makampuni ya nje ambayo yameingia ndani ya uchumi wenu kwa sababu ya miundombinu maalumu iliyolenga kuwezesha shughuli za makampuni hayo. Hivi ndivyo mambo yamekuwa kwa muda sasa ndani ya nchi yetu.

Tanzania kwa kipimo hiki, ni moja ya nchi ambazo uwekezaji wa miundombinu ya kiuchumi umekuwa mchango mdogo kwenye “DDIs”. Kwa mujibu wa Africa Re-imagined, kwa kila dola mia moja ya kimarekani($100) iliyoingia kwenye miundombinu kiuchumi ni dola tatu( $3) pekee ambayo imechangia moja kwa moja kwenye uwekezaji wa ndani kwenye sekta ya kilimo na chini ya dola moja($1) kwenye sekta ya uvuvi.

  1. “Mabadiliko halisi ya Kiuchumi”(Economic Transformation)

Mh Rais, sina hakika sana kama Kiswahili cha Economic Transformation ni hicho nilichotumia kwenye nukta yangu ya nne kwenye eneo hili. Hata hivyo, naomba unielewe kuwa hapa nina maana ya kuufanya uchumi kuwa na mabadiliko ya kimsingi kimfumo na kimatokeo. Kwamba uchumi katika hatua hii unalenga kuwafanya watu kuwa na tija zaidi kwenye uchumi wao kwa kuimarisha sekta ya viwanda nchini.

Hapa viwanda sina maana tu ya miundombinu ya viwandani lakini zaidi mfumo mzima wa kiuzalishaji kwenye jamiii ambao unaunganishwa na mfumo mama wa uchumi wa taifa kiviwanda. Katika hatua hii mambo makuu matatu (3) ni muhimu kuzingatiwa; 

Mosi, mgawanyo wa mitaji (Capital DE Concentration). Hapa maana yake ni kuwa vyanzo vikuu vya uzalishaji ambavyo vinatumika kwa usawa kwenye uchumi. Mitaji hii inaweza kuwa ardhi, miundombinu, teknolojia au mifumo ya kiutawala inayotoa mazingira na fursa za kiuzalishaji kwa usawa nchini. Hii hasa ndiyo maana ya mtaji kwenye uchumi.

Pamoja na kuwa eneo hili ni muhimu katika kujenga uchumi wa kitaifa, bado uendeshaji wa uchumi wetu haujaamini kwenye dhana hii. Badala yake, tumeamini kwa matokeo ya hoja hii ambayo ni mgawanyo wa vipato. Hii ni sawa na kupanda kutokea kwenye matawi. Ni njia ya uhakika ya kuchelewa kuimarisha uchumi wa kitaifa. Kama zilivyo hoja zingine, na hii inajidhihirisha kwenye takwimu zetu na hapa nioneshe kwa uchache.

  1. Pamoja na kuwa biashara ni kama asilimia thelathini na mbili (32%) ya pato ghafi la nchi(GDP), ukweli ni kuwa, asilimia tisini na nne(94%) ya *tija* ya  sehemu hii ya biashara tunaipoteza kwa sababu ya ukosefu wa usawa wa mitaji kwenye uchumi. Au tusema, tunapata asilimia sita(6%) ya tija kwenye biashara yetu.

Hii ni chini ya wastani wa nchi za “uchumi wa kati chini” kama nchi yetu ambao ni asilimia thelathini na sita(36%). Taarifa za kiuchumi zinaonesha kuwa, changamoto hii imekuwa sababu ya nchi nyingi kukwama kwenye uchumi wa kati (middle income trap), kuwa na gharama kubwa za biashara, na kuwa katika hali ambayo *nchi inakuwa kwenye uchumi wa kati lakini ina raia wachache wenye vipato vya kati.

Mataifa yaliyochupa kwa kasi ya haraka kiuchumi kama Kusini Mashariki mwa Asia, yalikabili vizuri hatari hii. Aidha kwa mujibu wa Bank ya Dunia(1970), inaoneasha kuwa hii ilikuwa sababu kuu ya uchumi wa Marekani kufikia utajiri wa Dola za Kimarekani Trillion Moja kwa mara ya kwanza mwaka(1969) kabla ya nchi nyingine yoyote kufanya hivyo.

  1. Kuwa na soko linalofanya kazi kwa wote( A fair market system). 

Hii ina maana kuwa na mfumo wa soko ambao unawawezesha wananchi kuwa sehemu muhimu  ya uchumi wa nchi yao.Kwa lugha nyingine, ni kuwa na sera ambazo kwa makusudi, zinalenga kuwaibua wananchi kumiliki uchumi na bila ya sera hizo kwa makusudi kuwasukuma nje ya mfumo wa uchumi  kwa hoja za kutokuwa na uwezo.

Kinyume na msingi huu, uchumi wetu umejengwa kwenye dhana ya kuwa na sera ambazo kwa makusudi, zinatengeneza soko la kiuchumi ambalo ni kizingiti kwa raia wa ndani. Hapa, hoja kama ukosefu wa mitaji, teknolojia, kutaka matokeo ya haraka na rushwa hutumika. Matokeo yake tunaendelea kufungamanisha soko la uchumi wetu ambao siyo wetu kimsingi, na soko la dunia ambalo siyo kazi yake kuwafanya raia kumiliki uchumi wao. Tumefanya hivi kwenye karibu kila sekta ya uchumi wetu.

Hata pale hoja za kiitikadi zinapoibuliwa, kwa mfano, kuwa; kusema hoja ya soko sawa kwa wote ni hoja ya kijamaa, watunga sera wanaona ni sawa kutumia nchi ambazo zinapambana kila siku kujenga uchumi wa soko sawa ili zitusaidie kujenga uchumi wa soko lisilokuwa sawa. Mifano ya nchi hizi ni mingi sana, kuanzia Sweden, Switzerland, Korea Kusini au Ujerumani.

Matokeo ya haya, uchumi wetu umekuwa na uwezo mdogo kwenye vipimo vya soko lililo sawa kwa wote ambavyo ni uwezo wa raia mmojammoja kulipa kodi( revenue per capita), pato la mtu mmojammoja (income per capita), uwezo wa serikali kutumia kwa kiwango cha mtu mmojammoja(spending per capita). Vipimo hivi huweza kusaidia ukuaji halisi wa uchumi(GDP) kwa kutumia uwiano wake.

Mh Rais, uwezo wetu kwa vipimo vyetu hapo juu, umeendelea kuwa hafifu kadiri tunavyofungamanisha uchumi wetu na soko la dunia kwa sababu nilizotaja awali. Vipimo hivi viko chini ya vipimo vya nchi kama Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiiji na Uingereza vya kati ya mwaka(1797-1820)

  1. Kupunguza ugonjwa wa (GPDism).

Mh, Rais, japo kipimo cha  afya ya uchumi wetu kama zilivyo chumi zingine kinabaki kuwa Pato Ghafi (GDP), ukweli ni kwamba; kipimo hiki ni hafifu mithili ya Daktari anayepima afya ya jumla ya mwili wa mwanadamu kwa kigezo tu cha uwezo wa kusimama.

Hata hivyo, unaweza kuwa na uwezo wa kusimama lakini usiweze kutembea. Kutoweza kutembea maana yake huwezi kukimbia. Usipoweza kufanya hayo, maana yake unayo matatizo mengine makubwa ndani ya mwili wako. Na hivyo, kushindwa kutembea au kukimbia linaweza lisiwe tatizo la msingi bali  matokeo ya tatizo kubwa zaidi ndani ya mwili. 

Kama ulivyo mwili wa binadamu, ndivyo ulivyo mfumo wa uchumi. GDP ni uwezo tu wa uchumi kuweza kusimama. Uwezo huo hauna maana uchumi utatembea; yaani kuwa na mabadiliko ya kiuchumi (Economic Transformation) na hatimaye kuweza kukimbia kwa kupunguza umaskini na kutengeneza utajiri endelevu kwa uchumi wa kitaifa. Kwa hiyo, ni muhimu kuangalia ndani ya mwili wa uchumi huo ili kupima vizuri afya yake.

Napenda pia kusema kuwa; daktari akitaka kujua afya ya binadamu huyo zaidi ya kipimo cha kusimama, hawezi kutumia viashiria ambavyo ili viashiria hivyo viwepo ni muhimu mtu huyu awe na afya njema ndani ya mwili wake. Kwa mfano, daktari hawezi akatumia kipimo cha kung’aa usoni hata kama mgonjwa amejipaka mafuta ya nazi kudai kuwa mtu huyo ana afya njema sasa. Au kutumia tabasamu la usoni kusema mtu huyu ana afya njema.

Kadhalika kwenye uchumi, GDP ambao ni uwezo wa kusimama tu, hakiwezi kuwa kipimo cha kupima afya jumla ya uchumi. Ili kujua tatizo ni sharti kuangalia ndani ya mwili wa uchumi ili kuona ni vitu gani vinafanya GDP ikue, vitu hivi ni lazima viwe ni vile vinavyoongeza tija kwenye uchumi na kuwa na uendelevu kupitia uchumi halisi kama ambavyo nimevitaja awali kuhusu mitaji, soko lililo sawa kwa wote, tija kwenye uchumi jumla badala ya makampuni tu au taasis. Na kwa hakika, kama vitu hivi havipo, huwezi kusema unapima afya ya uchumi wako kwa kutumia vitu ambavyo ili viwe halisi, lazima mfumo wa ndani wa uchumi uwe unafanya kazi.

Kwa mfano, huwezi kusema unaangalia furaha ya watu, kwa sababu, furaha ya kweli inatokana na uchumi halisi, au huwezi kusema unaangalia kipimo cha rasilimali watu hata kama rasilimali hiyo inasukumwa nje ya mfumo wa uchumi kwa sababu ya mfumo ulivyotengenezwa.

Mh Rais, mfumo wetu wa uchumi umekuwa wa kuangalia uwezo wa kusimama tu (GDP),na hata tunapotaka kuhalalisha njia hii, tunatumia vipimo ambavyo vinatakiwa kuwa matokeo ya uchumi halisi kama vile hali ya furaha ya watu au uwepo wa rasilimali watu isiyokuwa na uhusiano na uchumi wa ndani wenyewe.

Vipimo viko vingi vya ndani ya uchumi vinavyotakiwa kuangaliwa ili kujua afya halisi ya uchumi ili kuifanya GDP kuwa na maana. Lakini, naomba nitaje vichache na muhimu zaidi.

  1. Kiwango cha ukuaji wa uchumi kinachotokana na deni (public debt- financed growth) kupungua kila baada ya miaka mitano (5). Hii haina maana serikali inaacha kukopa, bali mambo makuu mawili yanatokea.

Moja, kiwango cha uchumi unaolipa kodi (tax paying economy unaongezeka). Kwa hiyo, uwiano wa kodi na Pato Ghafi (Tax/GDP ratio) unaongezeka. Maana yake kunakuwa na uhusiano mkubwa wa kati ya kuongeza deni na ongezeko la shughuli za kiuchumi za kuvuna kodi zaidi. 

Pili, kiwango cha ubora wa ukuaji (Growth with equity) unaongezeka. Hii maana yake uchumi unakuwa kwenye sekta ambazo watu wako.

Uchumi hauna taarifa nzuri kwenye eneo hili. Kati ya mwaka (2010-2020), kiasi cha ukuaji wa uchumi kinachochangiwa na deni la taifa ni asilimia sabini na moja (71%) na kwa kipindi hicho chote,  wastani wa uwiano wa kodi ni asilimia kumi na moja tu(11%). Hii ni sawa na kusema; kwa kila shilling mia moja(100) ya GDP, shilling sabini na moja ni ya deni la taifa na wakati huohuo, kati ya shilingi miamoja ya GDP, ni shilingi kumi na moja tu ya kodi.

  1. Uzalishaji na siyo Mapato.

Uimara wa uchumi kuacha kupimwa kwa kuangalia mapato(Revenues) kama msingi wa kuendesha uchumi bali Uzalishaji. Hii inaweza kutokea kama hoja (a) imefanyiwa kazi. Hii inapunguza changamoto kuu mbili kwenye uchumi.

Mosi, kupunguza viwango vya kodi zinazolemea watu maskini kwa kuwa kiwango cha deni kitakuwa kinapungua lakini shughuli zinaongezeka.

Pili, kupungua kwa miradi ya kiuchumi ambayo inaingiwa kwa hoja za “revenues” kuongezeka lakini bila umakini au kwa sababu ya mifumo korofi wa biashara duniani.

Mh, Rais, mkataba kati ya Tanzania na Dubai unathibitisha changamoto tajwa kwenye hoja ya uchumi na maendeleo. Ziko hoja nyingi zinazotumika kuonesha kuwa hili ni suala kuhusu maendeleo yetu, ni jambo la kimkakati na kwa hiyo litatufanya tupige hatua kubwa na ya haraka kimaendeleo.

Hoja hizo zinasaidiki ugonjwa wetu wa muda mrefu wa kulisha tunachokiita maendeleo na kudhoofisha uchumi halisi. Naomba kutaja maeneo kadhaa kwenye mkataba yanayoithibati hoja yangu.

Moja, exclusivity rights (Haki za kipekee anazopewa DP World kwenye kuendeleza, kusimamia na kuendesha gati moja mpaka saba. Kipengele hiki, kinaleta ugumu wa kufanya mambo ambayo yangekuwa na maana kwenye uchumi wetu kama ajira, kuwa na soko linalofanya kazi kwa wote, uwezo wa serikali kuwa na kauli juu ya maslahi ya nchi na hata lile pendekezo la kuundwa kampuni ya ndani ya ubia, linabaki kuwa na maana kwenye makaratasi kuliko uhalisia.

Pili, kwa mkataba kuwa bila ukomo, unaipa Dubai fursa za muda mrefu za kimkakati- kiuchumi (long-term strategic economic interests) kama nilivyozieleza hapo juu, na Tanzania kubaki na fursa hafifu za kibiashara (Short-term parochial business interests).

Tatu, mkataba huu unaifanya Tanzania kuwa kwenye nafasi dhalili kwenye hatua za mikataba inayofuata.  Mkataba huu kama ulivyo, umeamua ni jinsi gani mikataba ijayo ya kimiradi itavyokuwa. Haielezeki vizuri, ni kwa jinsi gani mikataba inayotarajiwa kuwa ni matokeo ya mkataba huu, itakuwa na maudhui tofauti ya kiuchumi kwa Dubai na kibiashara kwa Tanzania.

Itaendelea kesho kwa sehemu ya nne na ya mwisho.

Like
1