Anna Mghwira ajiingiza katika mgogoro na Kanisa Katoliki akitaka lipindishe taratibu za mazishi

MKUU wa Mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira (62), amejiingiza katika mgogoro wa kiimani na Kanisa Katoliki baada ya kuingilia taratibu za mazishi, akitumia mamlaka ya kisiasa kuamuru kanisa lipinde kanuni na misingi ya uendeshaji wa huduma zake.

Mgogoro huo ulidhihiri wiki moja iliyopita – Jumanne, Desemba 29, 2020 – katika Kitongoji cha Kisomboko, Uru Mawella, Moshi Vijijini, wakati wa maziko ya familia ya watu wanne – baba, mama na watoto wao wawili – waliofariki baada ya ajali ya moto iliyotokea siku moja baada ya  Sikukuu ya Krismas, katika Mtaa wa Sahare Majengo Mapya, Kata ya Mzingani jijini Tanga.

Waliofariki ni baba wa familia, Sigfrid Kimbi (44), mkewe Aurelia Shayo na watoto wao, Samweli Kimbi (9) na Ezra Kimbi (7). Miili yao ilisafirishwa hadi Moshi, nyumbani kwa Kimbi kwa ajili ya mazishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda, alisema ajali hiyo ilitokea wa saa 11 alfajiri na kwamba chanzo chake kinaelezwa kuwa ni hitilafu ya umeme.

Alisema mke na watoto hao walifariki papo hapo wakati baba wa familia hiyo alifariki katika baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Bombo wakati akipatiwa matibabu. Alisema vyomo husika vinaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.

Katika eneo la makaburi ya familia ya Kimbi, taratibu za Kanisa Katoliki za shughuli za mazishi ziliongozwa na Paroko wa Mawella, Padri Chrispine Jumanne, ambaye alisema kanisa litahusika zaidi kwa mazishi ya watoto wa Kimbi, na kwamba baba na mama wa watoto hao hawatapata misa takatifu kamili kwa kuwa hawakuwa wamefunga ndoa.

Nyumba iliyoteketea

“Taratibu na sheria za kanisa letu ziko wazi na zinaeleweka kwa kila muumini kwamba kama hutatimiza baadhi ya matakwa muhimu, basi kuna vitu utavikosa, uwe hai au vinginevyo, hivyo ni pamoja na ndoa takatifu,” alisema Paroko huyo.

SAUTI KUBWA imepewa taarifa kwamba Kimbi na mkewe, hadi mauti yanawakuta, hawajawahi kufunga ndoa takatifu kama inavyotakiwa na Kanisa Katoliki.

Kutokana na mazingira hayo, Padri Chrispine aliendelea shughuli za misa takatifu ya mazishi kwa watoto wawili. Baadaye, Kimbi na mkewe walizikwa na viongozi wengine wa kanisa hilo.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa mkoa, Mghwira, aliongoza umati wa waombolezaji katika mazishi hayo na alipopewa nafasi kutoa salamu za serikali alichafua “hali ya hewa” baada ya kushutumu Kanisa Katoliki, huku akidai kwamba Kimbi na familia yake “wamehukumiwa na binadamu na si Mungu,” na kwamba wazazi wa watoto waliozikwa kwa misa takatifu hawakupewa hadhi ya kuzikwa kwa staha na ubinadamu.

Kiongozi mmoja aliyesindikiza miili ya marehemu kutoka Tanga, ambaye jina wala dhamana yake katika serikali haikufahamika mara moja, ingawa ilielezwa kuwa alimwakilisha Meya wa Jiji la Tanga, aliunga mkono kauli ya mkuu wa mkoa, huku akipayuka, “Paroko anachukua mamlaka ya Mungu kuhukumu wenzake.”

Padri Chrispine alisema, “Katoliki lina taratibu zake, na wala si zangu, mimi nafanya yanayonipasa.”

Padri mwingine katika parokia hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema kiongozi mwenye hadhi ya mkuu wa mkoa, hapaswi kuonyesha kuingilia taratibu na sheria za kanisa lolote, kwani kwa kufanya hivyo ni kuingilia imani za dini za watu, jambo ambalo halipaswi kutokea.

“Huyu ni kiongozi mkubwa, anapingana na kanisa kwenye kadamnasi. Sasa sijui ana maana gani au anataka kupeleka ujumbe gani kwa wananchi ambao hakika wanapaswa kufuata taratibu na sheria kwa imani zao. Nadhani hafanyi vyema,” aliongeza padre huyo.

Sheria ya Kanisa Katoliki (namba 1177 – 1185) inasema kuwa ni haki ya kila muumini mkatoliki kufanyiwa ibada ya mazishi ya Kikristo isipokuwa kama amepoteza haki hiyo kwa ukaidi wake mwenyewe.

Haki hiyo inaambatana na wajibu wa mkristo husika kwa mamlaka ya Kanisa na jumuia nzima ya Kikristo. Wajibu wa mamlaka ya kanisa ni kuhakikisha kuwa wajibu wa mkristo unatimizwa.

Sheria hiyo inaeleza kuwa wakristo waliojitahidi kuishi vizuri maisha yao ya Kikristo wanapaswa kupatiwa huduma ya mazishi ya Kikristo katika parokia yao, na mazishi hayo yanapaswa kuongozwa na paroko au paroko msaidizi au padri yeyote au katekista au muumini mwingine aliyeidhinishwa na paroko kutekeleza wajibu huo.

Sheria hiyo inaeleza kuwa wanaonyimwa misa ya wafu ni pamoja na wale wasiofunga ndoa, wenye ndoa za mitala na wale wanaobainika kufanya dhambi za wazi, ikiwamo machukizo kadhaa dhidi ya Ukristo.

Msimamo huo wa mkuu wa mkoa umezusha mijadala katika mitandao ya kijamii huku mitazamo tofauti ikitolewa. Wapo wanaoshutumu na wengine wakiunga mkono kauli ya Mghwira.

Mery Shayo katika ukurasa wake wa Facebook anaandika: “Mungu akubariki sana Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, maana hizi dini zinazosema mtu asizikwe kama haendi kanisani, hiyo si sawa maana wakati mtu anakufa pengine alitubu makosa yake yote kwa Mungu wake, sasa binadamu hapaswi kuhukumu. Hiyo kazi aachiwe Mungu mweyewe.”

Sultani Tego anaandika katika ukurasa wa Facebook: “Kwanza nawapa poleni sana wafiwa na pia kiongozi (mkuu wa mkoa) umeongea kitu cha maana sana. Binadamu hapaswi kumhukumu binadamu mwenzake. Mtu akifa azikwe, Mungu ndio atakayehukumu.”

 Anania Nnko anaandika katika ukurasa wake wa Facebook, “poleni sana wapendwa, utaratibu wa kanisa ubaki hivyoh ivyo. Kitu cha msingi, Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro ahamasishe Wakristo kutengeneza maisha yao, kwa sababu huo ndo utaratibu wa kanisa letu na uheshimiwe.”

Theo Kilasi katika ukurasa wake wa Facebook anaadika: “Aliyekataa kushiriki imani akiwa hai ya nini kumshirikisha akiwa mfu? Katika kuishi tuna uhuru wa kuchagua. Hivyo, kila mtu akamilishwe kulingana na chaguo lake. Tuache kulaumu kusiko na maana. Hii iwe fundisho kwa wengine walio na ushupavu wa shingo wasiotaka kuishi kiimani.”

Like
3