MAKUMI ya wanachama na viongozi wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Kata ya Didia, Jimbo la Solwa, mkoa wa Shinyanga, ni miongoni mwa wananchi waliopiga kura ya wazi leo kupinga Mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai, kuhusu uendelezaji wa bandari na maeneo mengine ya kiuchumi.
Awali, UWT, waliokuwa wametangaza kufanya mkutano wao kwenye eneo la Tambukareli, waliamua ghafla kuhamishia mkutano wao jirani na mkutano wa Chadema, kwa nia ya kuvuruga mkutano wa Chadema, uliopangwa kuhutubiwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe alipowasili kwa helcopter, maelfu ya wananchi wa Didia waliukimbilia mkutano wa Chadema, wakiwemo wanachama na viongozi wa UWT walioamua kuukimbia mkutano wao.
Mkutano wa UWT ulipangwa kuhutubiwa na Mwenyekiti wao, Mary Chatanda.
Akiongoza kura ya wazi, Mbowe aliwaomba wananchi wote wanaokubaliana na msimamo wa CCM kuwa mkataba wa bandari ni mzuri na una manufaa kwa Taifa wanyooshe mikono yao juu, lakini hakuna hata mwananchi mmoja aliyenyoosha mkono wake juu kuunga mkono CCM na mkataba huo, licha ya kuwepo UWT uwanjani hapo.
Hata hivyo, alipouliza wananchi wote wanaounga mkono msimamo wa Chadema wa kupinga mkataba wa bandari, wanyooshe mikono yao juu, uwanja mzima ulinyoosha mikono juu kuashiria kupinga mkataba huo.
Miongoni mwa walio nyoosha mikono yao juu kupinga mkataba huo ni wanachama na viongozi wa UWT.
“Nashakuru akina mama wa CCM, nao wamenyoosha mikono yao juu kupinga mkataba huu. Ahsanteni sana. Mungu awabariki saba,” alisema Mbowe.
Mbali na Kata ya Didia, Mbowe anafanya jumla ya mikutano sita kwa siku nzima ya leo ndani ya jimbo la Solwa, akitumia usafiri wa helcopter.