SERIKALI ILINDE SIRI ZAKE, ISITEGEMEE VITISHO

Je, unajua kuwa ukiwa na chombo cha kukusanya, kuchakata na kusambaza maudhui, unakatazwa kisheria kutoa siri za serikali hata kama hujui siri hizo na hata jinsi ya kuzifikia?

Kama ulikuwa hujui; au umekuwa ukipuuza kujua, basi vijana wa siku hizi watakwambia, “itakula kwako.” Wanaojali nifuateni niwapeleke kwenye katazo hili la kisheria.

Kwanza, serikali zote duniani zina siri – nyaraka, misimbo, michoro, mipango mkakati, modeli, au dondoo zilizoainishwa kuwa ni Nyarakasiri.

Kufikia siri hizi zinazolindwa na sheria, sharti uwe unahusika au umeidhinishwa kisheria. Serikali ya Tanzania, nayo ina siri.

Leo nimekumbuka sehemu ya kiapo cha wanaokabidhiwa madaraka nchini. Hapa tunajadili hasa wale ambao huapa kwa kusema, pamoja na mengine, “…sitatoa siri za Baraza la Mawaziri…”

Waapaji ngazi hiyo, ndio watungasiri. Wajadilisiri. Wenyesiri. Walindasiri za Baraza la Mawaziri.

Ndani ya kikao: watakabidhiana siri. Wataahidi kutovujisha siri. Wengine watapewa vyeo/madaraka. Watakuja kuapa hadharani; kuambia dunia kuwa wana siri; na kuapa kweupe: kutovujisha siri hizo.

Kumbuka. Hizo ni siri zao. Wao. Ambazo hawataki zijulikane kwa wananchi; na wananchi “ndio msingi wa mamlaka yote” – Ibara ya 8(1)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).

Sasa kuna hili. Kama waundasiri, watunzasiri na watumiasiri wameishaapa kulinda siri zao; kwanini asiye mwenzao aulizwe au atuhumiwe kuvujisha siri za Baraza la Mawaziri; au siri zozote zile za serikali?

Hebu njoo huku. Tusome pamoja Sehemu ya Pili, Kifungu: 7(3)(d) cha THE MEDIA SERVICES ACT – Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Maudhui (Habari?) ya mwaka 2016).

Katika “lugha yao,” Kifungu kinasema hivi: “A media house shall, in the execution of its obligations, ensure that information issued does not disclose the proceedings of the Cabinet…”

Kabla ya kwenda mbali, tuzingatie maneno: “media house.” Sheria inatoa fasiri ya maneno hayo mawili, kwamba ni aliyesajiliwa na kupata idhini ya kutoa huduma za maudhui.”

Kwa hiyo, yeyote aliyechukua leseni kutoka ofisi ya msajili wa vyombo vya maudhui – katika nafasi yake yoyote ya kusaka, kukusanya, kuchakata na kusambaza maudhui; ajue ndiye anaelekezewa onyo hilo kwamba, “katika utendaji kazi wake, ahakikishe taarifa anazotoa haziweki kweupe (hazianiki) shughuli za Baraza la Mawaziri.

Kwa lugha ya kazi, Media House anaambiwa asifichue, asianike, asiweke peupe shughuli, vikao, kumbukumbu – (siri) za Baraza la Mawaziri.

Kawaida, kinachoitwa siri za Baraza la Mawaziri, ni shughuli zote za Baraza – wanaita Cabinet Proceedings: mwenendo, hoja, mijadala, uamuzi na taarifa – kwa maana ya vikao na yatokanayo ambayo Baraza lenyewe halijayatolea kauli hadharani.

Sasa anayepewa onyo la mapema, kwamba asithubutu “kufichua” siri za Baraza, ni yule jamaa waliyempa jina media house; mwenye leseni na ITHIBATI ya kutoa huduma ya kukusanya, kuchakata na kusambaza maudhui. Huenda ni wewe – mchapishaji, mtangazaji na msambazaji.

Aliyeshiriki kutunga siri, anayejua siri ameapishwa. Aliyekataa kuapa kwa “Kitabu cha Dini” – Biblia au Msahafu na hataki kutamka neno “naapa,” anapewa mbadala ambao ni tamko: “…nathibitisha na kutamka kwa dhati na unyoofu;” na kuacha kutamka maneno: “Mungu nisaidie.”

Wote hawa wanaoapa, wameona makabrasha ya vikao vya Baraza la Mawaziri. Wana kumbukumbu za yanayojadiliwa. Yanayoamuliwa. Yanayopitishwa.

Hao hao, wana kumbukumbu, hata za majina na sura za wachangiaji na wachagizaji; hata waliotaka kukwamisha mijadala – kama hilo lilikuwepo. Kwa ufupi, wana kumbukumbu za kumbukumbu zote. Wana siri. Wamekula yamini kulinda siri hizo.

Sasa tusemezane. Mwenye kampuni, chombo, kituo cha maudhui; au majukwaa mtandaoni, aliyechukua leseni, anapewaje tahadhari kisheria (onyo, angalizo) juu ya kuchapisha siri za Baraza la Mawaziri?

Hebu: Media House ajiepushe kuchapisha siri ambazo hana? Siri ambazo hajapewa? Siri ambazo hajatafuta? Ambazo hata hajaahidiwa? Ambazo hajashiriki kutunga? Ambazo hajui? Huu ni mzaha au nia mbaya?

Ajiepushe kwa kuwa siri zinaweza kupatikana bwerere mitaani? Zinanunulika? Kwakuwa walioapa kuzilinda siyo waaminifu? Kwakuwa ulizi wake ni goigoi? Kwamba Media House ndio njia pekee ambako siri za kuanika zaweza kupatikana?

Mbona kuna njia za kulinda siri – duniani kote: iwe kwa serikali, kampuni, shirika, taasisi, asasi, kundi la watu au mtu binafsi.

Kofuli imara la kufungia siri ni wewe binafsi au wale mlioapishana, kuendelea kuaminiana; na hata ikibidi kuapishana tena na tena; ili kiapo cha zamani kisichache. Kisipauke. Kisichakae. Kisisahaulike. Kisife.

Nani wale? Orchestre Bima Lee – bendi ya muziki wa dansa nchini. Wanafafanua hili vizuri. Waliimba: “Siri yako ni yako ee; Akishiriki mwingine si siri tena.”

Njia nyingine ya kuzuia mvujo ni kuwa na “siri salama.” Siri yenye manufaa kwa jamii. Ambayo haikupitishwa kwa hila wala husuda kwa mtu, kundi la watu au jamii.

Hii ni siri ambayo hata ikivuja, kila aliyeapishwa atabaki akijipiga kifua kwamba ililenga mema kwa watu wote; bali usiri wake lilikuwa suala la muda tu – lini chema kitawekwa sebuleni. Kwahiyo, ikivuja wanasema “haidhuru!”

Bali “siri” za hila na husuda haziwekeki. Hubana kifua. Hunyakua usingizi. Huwewesesha. Huleta ndoto za majinamizi. Husukuma “maagano” nje ya mifereji ya fahamu. Hutafuna ahadi. Hunyausha yamini. Hucheua kumbukumbu hadharani.

Turudi sasa kwa Media House (mwenye watangazaji, waandikaji, waandishi, wanahabari, waandishi wa habari, wachunguzi, watafiti na wasambazaji) aliyepewa leseni na ITHIBATI kwa shughuli zake.

Media House huyu ana uhusino gani na serikali mpaka sheria imtaje kuwa na uwezekano wa kuvujisha siri; hivyo kumtaka ahakikishe taarifa anazotoa hazifichui siri za Baraza la Mawaziri?

Je, huyu au hawa Media House wanahusika vipi na siri za Baraza la Mawaziri au hata za serikali kwa jumla mpaka watamkwe na sheria kwa njia ya kuonywa? Hakuna makundi mengine yawezayo kuwa na hamu ya kujua siri za Baraza la Mawaziri isipokuwa Media House? Kwani siri hutapakana kwa vyombo tu na mitandao; haziwezi kumwagika mitaani kama umbeya?

Hivi ni vitisho. Viliandaliwa rasmi kupitia sheria ili kujenga mazingira ya woga kwa Media House, waandishi wa habari na wananchi. Vinalenga kunyakua haki ya uhuru wa kutafuta, kupokea taarifa na kutoa maoni bila woga wala aibu.

Hii ni sheria iliyoandaliwa kama kitumbua. Unakisubiri jikoni. Mwokaji anakichomoa kwenye mafuta na kukubandika kiganjani.

Na ndivyo ilivyokuwa kwa Rais John Pombe Magufuli. Muswada ulipitishwa bungeni tarehe 5 Novemba 2016. Rais akausaini tarehe 16 – siku 11 tu tangu utoke bungeni. Haraka ya mshenga!

Bali kwa ufupi, mwenye siri ndiye anapaswa kulinda siri yake – kwa nguvu, stadi na utaalamu wowote ule. Akishindwa au akipuuza, ajiandae kukutana na siri yake mtaani. Sheria hii iachane na vitisho kwa Media House, jamii na mtu mmojammoja.

Like