NIMESOMA makala nne za Ndimara Tegambwage juu ya Ithibati na waandishi wa habari. Naendelea kujiridhisha kuwa huyu ni mwandishi wa viwango.
Makala ya kwanza: Ithibati na Press Card Kidijiti; Makala ya pili: Tabasamu la Waandishi wa Habari: Ni la Moyo au Shuruti? Makala ya tatu: PRESS CARD kwa Mwandishi wa Habari: Itolewe na Serikali au Mwajiri? Makala ya nne: Ithibati na Press Card: Pacha au Pachanga?
Utamu wa makala hizi ni jinsi mwandishi anavyojenga hoja ya utetezi wa waandishi wa habari wenzake na anavyoshona pamoja kazi ya kuandika habari na hoja muhimu ya haki ya kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.
Hakuna shaka kwamba Baraza la Habari Tanzania (MCT), chini ya Katibu Mtendaji Kajubi Mukajanga, halikukosea kumpa Ndimara tuzo ya maisha kwa kazi zake zilizotukuka.
Sasa kilichonisukuma kuandika haya ni kuhimiza waandishi wa habari kuwa wamoja; kusimama imara, kujadiliana – ambalo Ndimara anaita “kusemezana;” na kukutana na serikali, si kwa mapambano, bali kwa mjadala mzito juu ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 ambayo wamekuwa wakiilalamikia.

Hili laweza kuwa jepesi kwakuwa wakuu wa ithibati ni waandishi wa habari waelewa. Ni kweli wao wamekabidhiwa chombo waendeshe lakini wanaweza kuelewa vema pale panapouma na kupendekeza jinsi ya kuondoa mwiba.
Kwa mfano, Mwenyekiti Tido Mhado ni mtangazaji wa kimataifa wa viwango vyake; ni mwelewa. Wenzake wanne ni wanahabari au wamekuwa katika shughuli za habari. Watakuwa wanakumbuka vitabu kadhaa vya mwenzao Ndimara juu ya kutetea uhuru wa habari; hasa kijitabu kiitwacho: Uhuru wa Habari Kitanzini.
Sina uhakika kama Ndimara bado anakumbuka.alivyonikabidhi nakala ya kijitabu hicho uwanja wa ndege Mwanza mwaka 1993.
Nakumbuka ni hoja katika kijitabu hicho ambazo Ndimara alitumia kupigania uwepo wa Baraza la Habari la Waandishi wa Habari wenyewe ambalo limedumu kwa miaka 30 sasa. Ninakumbuka serikali ilikuwa imeandaa kuanzisha baraza lake, lakini ikaamua kuacha waandishi waanzishe chombo chao.
Uandishi kama wa Ndimara bado unahitajika sana nchini, na Mungu ampe miaka mingine mingi ili aendelee kusemezana na waandishi na wenye mamlaka.