MGOMBEA Ubunge wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Jimbo la Kibamba, Edward Kinabo, amesema mgombea ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Angellah Kairuki hana jipya kwa jimbo la Kibamba, kwani ana rekodi ndefu ya kushindwa kazi katika nafasi mbalimbali alizoshika serikalini.
Akihutubia wananchi katika vijiwe mbalimbali vya kata ya Kibamba kupitia kampeni yake ya kupita mitaani ‘mobile campaign,‘ Kinabo alisema.
“Sasa amekuja huyu mama anataka aonekane ni mtu mpya. Lakini mimi nawaambia hana upya wowote. Huyu bibi waliemleta ameshakuwa waziri kwenye wizara nyingi sana. Wanamweka wizara hii anashindwa wanampeleka wizara nyingine, wanamtoa nyingine wanampeleka nyingine. Ameboronga kote, halafu anakuja Kibamba kutaka ubunge. Hatoshi!” alisema Kinabo.

Akizungumzia ahadi za Kairuki, Kinabo alisema:
“Kama alishindwa kujenga barabara za lami alipokuwa waziri, hana sababu ya kudanganya wananchi kwamba atajenga barabara za lami katika ubunge. Tuachane na usanii.”
Mwanasiasa huyo machachari amesema mwisho wa longolongo za CCM katika jimbo la Kibamba ni tarehe 28 Oktoba, na kwamba tarehe 29 Oktoba wananchi wa Kibamba watatoa hukumu dhidi ya ahadi zile zile za CCM zisizotekelezeka. Akasisitiza:
“Huyu bibi kwasababu ni mgeni kwenye jimbo hili, hajui kama chama chake kilishatoa ahadi hizo hizo anazotoa sasa. Sasa wamemuingiza mkenge, wamemuandikia orodha ndefu ya barabara na kila barabara anasema ataweka lami.”
“CCM ndiyo iliyo madarakani, ndiyo inayokusanya na kutumia kodi zetu. Huu si wakati wa CCM kurudia ahadi zile zile za miaka nenda, miaka rudi. Mwisho wa Kairuki na CCM kujenga barabara za lami ni tarehe 28 Oktoba. Oktoba 29 ni siku ya hukumu, siyo siku ya kupigia kura uwongo ule ule wa miaka yote, ” alisema Kinabo.

Kinabo ambaye pia ni Katibu wa Sekretariati ya Chaumma Taifa na Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma wa chama hicho, amewaomba wakazi wa Kibamba wamchague kwa kura nyingi kuwa mbunge wa jimbo hilo ili akawape uwakilishi makini na kusukuma uwajibikaji katika kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo ya Kibamba.