KATIBU Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, amesema chama hicho kikiingia madarakani kitaongeza uwekezaji wa kimkakati katika sekta nzima ya kilimo ili kupambana na hali ya umaskini nchini.
Mwalimu amesema licha ya takwimu kuonesha kuwa uchumi unakua, bado ukuaji huo haujaweza kuleta tija ya kuridhisha katika kupunguza umaskini wala kupunguza pengo la vipato baina ya walionacho na wasionacho.
Mwalimu ameyasema hayo leo katika mjadala wa Cafe Talk uliofanyika jioni hii katika hoteli ya Serena na kushirikisha viongozi mbalimbali wa kiserikali na vyama vya siasa.
Kiongozi huyo amesema uchumi wa Tanzania ulikua kwa 5.5% mwaka jana na unatarajiwa kukua zaidi hadi kufikia 6% mwaka huu lakini bado hali ya umaskini wa wananchi ipo juu.
“Ni kweli uchumi mpana unakua lakini bado ukuaji huo haujawagusa wananchi wa kawaida. Kwa mfano, Ripoti ya mwaka huu ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Biashara na Maendeleo Duniani (UNCTAD), inaonyesha bado 26.4% ya Watanzania wapo chini ya msitari wa umaskini wa Taifa, kwa maana ya kushindwa kumudu mahitaji ya kimaisha ya Shilingi 49,320 kwa mwezi,” alisema Mwalimu na kuongeza,
“Na utafiti ule ulipotumia kigezo cha kimataifa cha kupima umaskini wa kupindukia (international extreme povery line), ambacho ni mtu kuishi chini ya kipato cha dola 2.15 kwa siku, imeonekana kuwa 44.9% ya Watanzania wapo kwenye umaskini huo wa kupindukia.”
Akijibu swali juu ya Chaumma itafanya nini ili kuondokana na hali ya umaskini, mwanasiasa huyo alisema, kilimo ndiyo kitakuwa kipaumbele kikuu kwani sekta hiyo inaajiri zaidi ya 65% ya Watanzania.
“Tutawekeza zaidi kwenye kilimo ili angalau kifikie ukuaji wa 10%, kwasababu kilimo ndiyo sekta inayogusa watu wengi, tuna ardhi ya kutosha na mazingira mazuri ya kijiografia,” alisema
Akigusia mikakati ya Chaumma katika kunyanyua kilimo, Mwalimu alisema, chama hicho kitaongeza bajeti za kila mwaka za kilimo ili zisaidie kuongeza upatikanaji nafuu wa pembejeo za kilimo, kuongeza eneo linalotumika kwa kilimo cha umwagiliaji pamoja na kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza thamani na kuvutia masoko na bei nzuri, zitakazosaidia wakulima kujikwamua kutoka kwenye umaskini wa kipato.
“Tuna ardhi kubwa na nzuri inayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini eneo linalotumika ni hekta milioni moja,” alisema Mwalimu akirejea takwimu mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazoonesha kuwa ina jumla ya hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lakini bado hazijatumika kikamilifu.
“Kama Taifa tunapaswa kuachana na sera ya CCM ya kuhodhi soko la mazao kwa kutumia serikali na AMCOs, kwani sera hiyo imechochea ulanguzi na kuwanyima wakulima wetu fursa ya kupata bei nzuri za mazao yao,” alisema.
“CHAUMMA kupitia sera yetu ya kujenga uchumi wa soko la kijamii tutafungulia fursa za masoko kutoka kwa wanunuzi wa ndani na nje ya nchi na kuweka uangalizi wa kutosha wa kuhakikisha hakuna mwananchi anayelanguliwa wala kunyonywa,” alifafanua Mwalimu.
Hoja ya kiongozi huyo wa Chaumma kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwenye kilimo ili kuharakisha kasi ya kupunguza umaskini, iliungwa mkono na Kamishina wa Serikali anayesimamia ubia baina ya sekta ya binafsi na sekta umma (PPP), David Kafulila, ambaye alisema utafiti uliowahi kufanywa na shirika la REPOA ulithibitisha kuwa iwapo sekta ya kilimo itakua kwa ukuaji wa 10% kwa miaka mitatu mfululizo, basi umaskini utapungua kwa kasi kubwa.