MWANDISHI wa habari Godfrey Ng’omba, ripota wa Milard Ayo kutoka Arusha, amevamiwa na askari polisi leo wakati akirekodi tukio la wananchi kufunga Barabara ya Moduli katika eneo la Mbuyuni, Kata ya Makuyuni, wilayani Monduli. Wananchi walikuwa wakishinikiza kupatiwa majibu kuhusu kupotea kwa watoto wawili, tukio lililozua taharuki kubwa.
Watch another coverage of the same event
Wananchi hao walifunga barabara kwa lengo la kumzuia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, asipite akiwa anatokea ziara yake Monduli. Walitaka majibu ya haraka kuhusu watoto wao waliopotea.
Kwa maagizo ya Makonda, polisi walijaribu kumkamata mwandishi huyo alipokuwa akirekodi tukio, lakini aliwazidi nguvu. Msaidizi wa Makonda alishuka kwenye gari na kuwasaidia polisi kwa kuchukua kadi ya kumbukumbu ya kamera ya mwandishi huyo na kuondoka nayo.
Mashuhuda wa tukio hilo wanasema kuwa Makonda alipomuona mwandishi huyo akirekodi aliwaagiza polisi wamkamate ili habari za kufungwa kwa barabara na malalamiko ya wananchi yasiripotiwe katika vyombo vya habari.
“Tuliifunga barabara ili kupata haki zetu, tunataka kujua watoto wetu wako wapi, lakini badala ya kusaidiwa, wanatuletea polisi. Hatukubaliani na namna wanavyotunyanyasa,” alisema mmoja wa wananchi aliyekuwepo eneo hilo.
Tukio hili linarejesha kumbukumbu ya matukio ya watu kutoweka, wakiwemo waandishi wa habari, yaliyotokea miaka mitatu iliyopita, ambapo baadhi yao hadi leo hawajulikani walipo. Matukio ya aina hii yamekuwa yakiongezeka siku za karibuni, huku baadhi ya watuhumiwa wakihusishwa na maafisa wa polisi.
Hivi karibuni, tukio la kutekwa kwa kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Sativa liliripotiwa jijini Dar es Salaam. Sativa alipatikana akiwa amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi kichwani na kutelekezwa kwenye Hifadhi ya Katavi.
Aidha, vijana watatu, akiwemo Soka wa CHADEMA, walipigiwa simu na kuitwa kituo cha polisi. Walipokuwa njiani kuelekea kuitikia wito huo, walitekwa na hadi sasa hawajulikani walipo.
“Tunaishi kwa hofu kubwa sasa. Inaonekana hata kwenda polisi hatuko salama. Vijana wetu wanapotea na hakuna anayejua wanakopelekwa,” alisema mkazi mmoja wa Dar es Salaam wakati akichangia kwenye moja ya magroup ya mtandao wa kijamjii wa WhatsApp.
Matukio haya yameongeza wasiwasi kwa wananchi kuhusu usalama wao. Utekaji, kutoweka kwa watu, na hata mauaji sasa vimekuwa ni matukio ya kawaida kuripotiwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Tangu utawala wa awamu ya tano, Makonda amekuwa anatuhumiwa kuongoza vikosi vya “watu wasiojulikana” kuteka na kupoteza watu kwa sababu binafsi na kisiasa, huku akikingiwa kifua na wakubwa wake.
Jeshi la Polisi limekuwa likiahidi kufanya uchunguzi wa kina, lakini hadi sasa hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa hivi karibuni na Msema wa Jeshi hilo David Masime, uchunguzi unaendelea, lakini bado hakuna taarifa yoyote iliyotolewa hadharani.
Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano ili kusaidia polisi katika kukamata wahusika na kuhakikisha haki inatendeka.
Hali ya usalama imezidi kuwa tete, huku wananchi wakihofia maisha yao. Tanzania, ikiwa ni kisiwa cha amani, inapaswa kuhakikisha amani hiyo inadumishwa kwa kushirikiana na vyombo vya dola na kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mmoja.