Inaendelea ilipoishia katika toleo lililopita:
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limesema ukaguzi wa mashine za kamari unafanywa na kampuni walizoingia nazo mkataba zikiwa katika nchi zitokako kabla hazijasafirishwa chini ya program iitwayo; Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC).
TBS imesema kuwa linafanya ukaguzi wa mashine zinapoingizwa nchini bila kujali zinakwenda kutumika mkoa gani, na kwamba kuanzia Februari 2023 mpaka Disemba 2023,walikagua mashine 3340 zilizoingia nchini bila kujali zimekwenda kutumika mkoa gani.
Wakati hali ikiwa hivyo, bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 iliongeza ushuru kwa asilimia 20 katika mashine za michezo ya kubahatisha zinazoingizwa nchini.
Pamoja na kuwapo faida zitokanazo na michezo ya kubahatisha, kuna hasara kadhaa za kiuchumi.
Donald Bubelwa ambaye ni mtaalam wa uchumi na fedha, anasema hatua ya vijana wakiwamo wasomi kuingia kwenye uraibu wa kamari kunaweza kupunguza nguvukazi na kushusha pato la taifa (GDP) kwakuwa akili zao wamezielekeza kwenye kamari na kuifanya kuwa chanzo chao cha mapato.
Halmashauri hazipati tozo ya kamari
Katika mitaa ya Manzese, Mwananyamala, Kigogo na Tandale, kila baada mita 20 hadi 30 kuna mashine za kubeti jambo ambalo linachangia vijana wengi kushiriki.
Kutapakaa kwa kamari kila kona jijini Dar es Salaam haijazisaidia halmashauri zake kuingiza mapato yoyote kutokana na sbiashara hizo.
Mmoja wa watendaji ambaye alikataa kutajwa jina lake kwa maelezo kuwa hajaruhusiwa na mkurugezi wa Manispaa ya Kinondoni, amesema sheria za serikali za mitaa haziitambui michezo ya kubahatisha kama chanzo cha mapato kwenye halmashauri zao.
“Hatuna miguu ya kusimamia kupata kodi au tozo kutokana kwenye vituo vya michezo ya kamari vilivyotapakaa kwenye mitaa yetu, kanuni zinazoongoza sekta hii zipo nje ya uwezo wetu, ninadhani sheria inapaswa kuangaliwa upya, hizi biashara zinapaswa kuwa chini ya halmashauri zetu”amesema mtendaji huyo”
Kwa mujibu wa sheria, Ofisi za Serikali za mitaa zinahudumia waombaji wa leseni za vileo, maduka ya bidhaa mbalimbali, mighahawa, salooni, viwanda, gereji, masoko na nyinginezo huku sekta ya michezo ya kubahatisha ikiishia GBT na Brela.
Msemaji wa Manispaa Kinondoni, Aquilinus Shiduki amesema kamari ni michezo ambayo inaratibiwa na chombo kingine nje ya mfumo wa manispaa.
“Kamari ni michezo ambayo inaratibiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha na kusajiliwa Brela. Manispaa hatuna mwongozo wowote uliotolewa na Bodi juu ya usimamizi wa michezo hiyo ya kamari kwenye halamshauri zetu.”amesema Shiduki.
Kwa upande wake, Msemaji wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu amesema manispaa hawahusiki na hawana miongozo yoyote ya uanzishwaji wa biashara zozote za kamari.
“Kama watendahi wamekwambia hawahusiki na uanzishwaji wa biashara zote za kamari katika mitaa yao wapo sahihi, sisi kama manispaa hatuna miongozo yoyote ya michezo ya kubahatisha kwani wana Bodi yao pamoja na Brela, hao ndiyo wanahusika”amesema Tabu.
Kwa upande wa ajira, hakuna ushahidi wa wazi unaoonyesha kwamba uwekezaji wa michezo ya kubahatisha umepanua soko la ajira nchini kama moja ya sharti la uwekezaji nchini.
Ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umasikini Tanzania (REPOA) ya 2019, inasema kuwa vyuo vyetu nchini vinatoa wahitimu milioni 1 kila mwaka ikilinganisha na nafasi 250,000 zinazotolewa serikalini kila mwaka.
Aidha Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) katika ripoti yake ya mwaka 2017/2018, inaonesha kuwa ajira katika sekta binafsi ilishuka kutoka nafasi 239,017 mwaka 2016/2017 hadi ajira 137.054.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) hawakuweza kujibu maswali yetu yaliyotaka kujua endapo kuna sheria au kanuni mahsusui za uwekezaji wa michezo ya kubahatisha nchini.
Pia SAUTI KUBWA ilitaka kupata ufafanuzi kuhusu kiwango (threshold) cha mtaji kwa wawekezaji wa michezo ya kubahatisha kutoka nje na ni kampuni ngapi za kigeni mpaka sasa zilizosajiriwa kuendesha michezo ya kubahatisha kwa kipindi cha miaka miwili.
Aidha Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) hawakujibu swali letu lililotaka kufahamu idadi ya kampuni zilizosajiliwa kuwekeza kwenye michezo ya kubahatisha kwa mwaka 2021/2022 na 2023/2024?
Boniphace Mgaya ni mwanafunzi wa Sheria Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es salaam (TURDACO), anasema madhara ya kamari kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ni mengi hasa kwa mataifa yanayoendelea kiuchumi ikiwemo Tanzania.
Anasema vijana wengi wa vyuo vikuu wanaingia kusoma huku wakiwaza mafanikio ya haraka, hivyo kujiingiza kwenye kucheza kamari kama njia ya mkato.
“Matangazo ya kampuni za ‘kubeti’ ni tatizo, yanahamasisha vijana wengi kuamini kwamba kuna washindi wa hadi milioni 500 hata zaidi ya hapo. Matokeo yake ni kuwadumaza, kupumbaza akili za vijana.”
“Mwenzangu mmoja alianza kubeti tangu mwaka 2018; kila siku anatumia si chini ya Shilingi 3000 mpaka 5000; mwaka jana alishinda Shilingi 800,000, alifurahi sana, lakini ukipiga hesabu fedha aliyotumia muda wote huo ni zaidi ya Shilingi milioni 5, lakini hakuliona hilo kwa sababu amepumbazika”anasema Mgaya.
Mgaya anaishauri Serikali iangalie upya utaratibu wa utoaji vibali kwa kampuni za kamari pamoja na matangazo yanayohusiana nayo kwakuwa baadhi ya wanafunzi wanaingia vyuoni wakiwa chini ya miaka 18, na hawajakomaa kwenye maamuzi yao.
Mwanafunzi mwingine Rhoda Julius ambaye ni kiongozi wa Serikali ya wanafunzi TURDACO anasema ingawa Serikali imeongeza fedha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu baadhi yao wanazitumia kwenye kamari na mwishowe wanataabika kwa kufilisiwa na kamari.s
“Baadhi ya wanafunzi wenzetu tayari wapo kwenye uraibu wa kamari, wamekuwa wakija kwangu kuniomba niwatetee kwa uongozi wa chuo waruhusiwe kufanya mitihani baada ya kukosa ada. Ukichunguza zaidi unabaini fedha walizimalizia kwenye kamari wakitarajia kupata zaidi”anasema Rhoda.
Anwar Athman mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema “Nimewahi kucheza. Nilijaribu mara ya kwanza, niliweka 200 kubashiri timu 14, nikipatia kwa usahihi nishinde milioni 51, sikufanikiwa.
“Ni kitu ambacho kisichowezekana! Eti uweke Shilingi 200 ushinde milioni 51. Naweza kusema ni kitu kigumu kwa sababu tangu nianze kucheza kamari, sikuwahi kuona hata watu wanaonizunguka wakishinda,” anasema Anwar na kuongeza:
“Betting sio mtaji wa kumfanya mtu ‘atoboe’ vijana mtaa mzima wanashinda kwenye betting, utasikia tu matangazo ya fulani ameshinda, lakini hujawahi kushinda wewe, jirani au rafiki yako wa karibu, kwa nini?”
Sophia Ismail mkazi wa Manzese Tip Top ni wakala wa ‘dubwi bonanza’ anasema aliletewa mashine na Wachina, lakini baadaye familia yake ilimshauri kuachana nayo kwani inakiuka misingi ya imani yao ya dini ya Kiislam.
“Wakati nalipokea nilielezwa kuwa ile mashine ina visahani (trey) vyenye uwezo wa kubeba sarafu zenye thamani ya Shilingi 60,000, na linapojaa unawapigia wanakuja kulichukua, wanakuachia Shilingi 9000, fedha ambayo imejumuishwa kwenye umeme unaotumika kwenye mashine hiyo.