Mbowe akasirishwa na serikali kuacha wanyamapori waue wananchi

KATIKA mkutano wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, leo kwenye kijiji cha Sakasaka, Jimbo la Kisesa, wilayani Meatu, mkoa wa Simiyu, wananchi wamelalamikia kukithiri kwa mauaji ya binadamu,mifugo hasa ng’ombe, uharibifu wa nyumba na mazao yao, unaofanywa na wanyamapori hususan tembo wanaotokea kwenye hifadhi ya wanyama pori ya Maswa (Maswa Game Reserve).

Wananchi hao wameeleza kwamba wamenyang’anywa silaha za kujilinda dhidi ya wanyama pori, hali inayowafanya wazidi kuishi kwa hofu kubwa.

Akionesha kukasirishwa sana na jambo hilo, Mbowe alisema, tatizo la mauwaji ya wananchi na uharibifu unaofanywa na wanyamapori si la wananchi wa Sakasaka pekee, bali pia limekithiri maeneo yote nchini yaliyo pembezoni mwa hifadhi, huku Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ikiwa haina ufumbuzi wowote juu ya suala hilo.

Alisema kitendo cha serikali kuamua wananchi wanyang’anywe hadi silaha za kujilinda ni cha kikatili na kisicho na utu wala ubinadamu na badala yake kinathibitisha jinsi serikali inavyothamini wanyama pori kuliko uhai wa raia.

Alisema mwenye wajibu wa kudhibiti wanyama pori wasivuke eneo la mbuga na kusababisha mauaji na uharibifu wa makazi ni serikali, lakini wanyama wanaachiwa wavuke mpaka huku wananchi wakiwa wamenyang’anywa haki yao ya kujilinda.

“Kati ya wanyamapori na binadamu, kitu cha kwanza ambacho serikali walipaswa kukilinda ni uhai wa binadamu. Ni uzembe wa serikali kushindwa kudhibiti wanyama pori halafu wakati huo huo unawazuia wananchi wasijilinde.

“Wananchi mngekuwa mnachukua silaha na kwenda mbugani kuuwa wanyamapori hilo lingekuwa ni kosa, lakini wanyama pori wanapovuka na kuwafuata kwenye makazi yenu hapo mna haki zote za kulinda uhai wenu. Hatua ya serikali kuwanyang’anya silaha za kujilinda haikubaliki,” alisema Mbowe.

Aliongeza kuwa jambo hilo limekithiri kote nchini kwasababu ya serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutumia njia za kizamani ambazo zimeweka tu umbali wa kisheria unaotenganisha mbuga na makazi ya binadamu, lakini bila kuweka kizuizi chochote dhidi ya wanyama.

“Jambo hili linahitaji ufumbuzi wa kisayansi, lakini naambiwa serikali imeweka mpaka wa umbali tu, kwamba wananchi msijenge, kuishi wala kufanya shughuli zenu ndani ya mita 500 zinazoelekea hifadhini.

“Hawajaweka uzio wowote wa kudhibiti wanyama. Mita 500 ni umbali mfupi, sawa na viwanja vitano tu vya mpira wa miguu. Sasa wanategemea eti tembo, fisi, nyati, Chui wafike sehemu waseme hapa ni mpaka wa mita 500, mimi mnyama sitakiwi kuvuka kwenda kwenye makazi ya binadamu. Huu ni ujinga huu,” alisema Mbowe na wananchi kuangua vicheko.

Alishauri kuwa serikali inapaswa kufanya utafiti wa kisayansi utaowezesha kuweka uzio kama uzio unaotumia umeme (electric fence), ili kudhibiti wanyamapori na binadamu kuingiliana.

“Sera ya CCM ya kudhibiti wanyamapori haitekelezwi kisayansi. Niwape mfano mdogo. Nenda Kenya hapo, kwa jirani zetu. Nao wana mbuga. Mbuga ambayo kwetu inaitwa Serengeti na Kenya pia ipo, kule kwao inaitwa Masai Mara. Wana mbuga pia inaitwa Tsavo, Mboseli na katikati ya jiji la Nairobi kuna hifadhi ya wanyamapori inaitwa Nairobi National Park, lakini kule huwezi kusikia eti Tembo, Fisi, Nyati wameingilia binadamu na kuwaua. Wenzetu mbuga zao zote zimepigwa uzio wa umeme, unaozuia wanyamapori wasiingilie binadamu na binadamu nao pamoja na mifugo yao wasiingilie wanyamapori.

“Ukienda Afrika Kusini nao pia wana mbuga. Nao wamepiga fence ya umeme (uzio). Msifikiri hapa kwetu haiwezekani. Inawezekana, wala siyo gharama kubwa. Wakibana matumizi ya kununua shangingi moja tu wanaweza kabisa kuweka fence na kulinda usalama wa raia dhidi ya wanyamapori. Sera sahihi ni kuweka uzio na maeneo ya mifugo yatengwe ili wananchi msilazimike kwenda kutafuta malisho mazuri ya mifugo yenu kwenye maeneo ya hifadhi,” alisema Mbowe

Imeelezwa kuwa wananchi wengi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hiyo japo kwa mbali, wamekuwa wakiingia hasara kubwa na ya mara kwa mara kwa mifugo yao kukamatwa na askari kwa madai ya kuingilia eneo la hifadhi.

Aidha, wananchi wanapouawa na wanyamapori, familia huishia kupewa kifuta machozi cha shilingi milioni tu, na wanapojeruhiwa na mnyamapori hupewa shilingi laki 5, pesa ambazo wananchi wamesema hawazitaki kwani hazilingani na thamani ya uhai na usalama wao.

Mwenyekiti huyo wa Chadema, mbali na kuitaka serikali kuchukua hatua za haraka kwa kujenga uzio wa umeme katika maeneo yote ya hifadhi nchini ili kulinda usalama wa raia na mali zao, pia amewaomba Watanzania wote wanaoishi pembezoni na hifadhi, kuzidi kujiunga na Chadema ili kujenga Chama imara kitakacho wakomboa, hususan kuboresha uchumi wa zao la pamba, miundombinu ya mifugo na kutatua tatizo kubwa la kukosa maji safi na salama.

Like