Mbowe ‘awa mbogo’ kwa serikali kuchelewesha katiba mpya

LEO jioni, akihutubia wananchi wa Malampaka, Jimbo la Maswa Magharibi, mkoani Simiyu, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametoa msimamo wa chama chake kuhusu Katiba Mpya, huku akimtahadharisha Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwamba jaribio lolote la kujaribu kuchelewesha mchakato wa kupatikana katiba Mpya halikubaliki na linaweza kusababisha madhara makubwa kwa taifa.

Kwamba, kama serikali imedhamiria kuchelewesha kupatikana kwa Katiba Mpya, kwa kujifanya kuwa itaanza kwanza kutoa elimu ya katiba ya sasa kwa miaka mitatu, basi Chadema itakuwa imelazimishwa rasmi kuwaongoza wananchi kuidai Katiba Mpya kwa nguvu ya umma.

Mbowe, amesisitiza kuwa Chadema na Watanzania walio wengi hawatokuwa tayari kufanywa “mandondocha” kwa nchi yao kuendelea kuongozwa na Katiba mbovu, huku serikali ikijiandaa kuteketeza mabilioni ya fedha zao kuwapa elimu ya katiba, wakati kazi hiyo ilishafanywa na kukamilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba, kwa gharama kubwa.

Mbowe ametuma salaam kwa Rais Samia, akimtaka atambue kwamba Chadema haikuingia kwenye maridhiano kwasababu ya kukiogopa Chama cha Mapinduzi (CCM) wala serikali yake, bali iliongozwa na nia njema na busara ya kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana kupitia mchakato unao waunganisha wananchi wote na kujenga utengamano wa kitaifa.

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, ndiye aliyenukuliwa na vyombo vya habari hivi majuzi akisema kwamba suala la katiba mpya litaanza kwa serikali kutoa kwanza elimu ya katiba ya sasa kwa miaka mitatu, kauli iliyoashiria kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025 zitafanyika chini ya katiba ya sasa.

Wananchi wa kijiji cha Sakasaka, Jimbo la Kisesa, wilaya ya Meatu, mkoa wa Simiyu wakitoa maoni kwa Mbowe.

“Kuna Bwana mmoja mfupi, anajiita Waziri wa Katiba. Nimesikia Rais amembadilisha. Huyu Bwana mdogo aliyezaliwa mwaka 1971, ametangaza kwamba yeye na seriksli yake wametuchunguza Watanzania wote milioni 64, na kuona sisi wote hatuna akili, hatujui katiba na hatujui haki zetu, pamoja na elimu na maoni yote yale tuliyotoa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ya Jaji Warioba. Kwamba eti watatumia miaka mitatu kutoa elimu ya katiba ya sasa kwanza. Hivi kuna mtu asiyejua haki zake za katiba hapa? Hili jambo hatuko tayari,” alisema Mbowe

Tayari, kauli ya Ndumbaro imepingwa vikali na asasi za kiraia na wanaharakati mbalimbali nchini, wakionesha wazi kuwa hiyo ni njama ya serikali kupuuza maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Warioba na kujaribu kuchelewesha katiba Mpya kwa makusudi.

“Kuna muda wa kubembelezana. Chadema tumekuwa kwenye mazungumzo ya kutafuta maridhiano kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Timu ya CCM ikiongozwa na Kinana na timu ya Chadema ikiongozwa na Mimi Mbowe. Tumekuwa tunawatuliza wananchi, tukiwaambia wananchi tulieni kwanza tuzungumze.

“Ni lazima katiba mpya ipatikane sasa. Hatupo tayari kuona fedha zenu wananchi zikitafunwa eti kwa kutumika kutoa elimu ya katiba, wakati Warioba alishamaliza kazi hiyo na walishatumia fedha za umma.

Aliongeza kuwa Chadema haipo tayari kuona nchi ikiendelea kuongozwa na katiba ya sasa inayompa rais madaraka makubwa kupitiliza, kiasi cha kutoweza kushitakiwa hata akifanya jambo lolote linaloumiza nchi.

“Mbali na rais, sasa hivi hata spika wa bunge, akifanya madudu kiasi gani hawezi kushitakiwa. Ndiyo maana wanafanya watakavyo. Tunataka katiba itakayoleta uchaguzi huru na haki kwa maslahi ya taifa. Mijitu iliyoingia madarakani kwa wizi wa kura haiwezi kamwe kulinda raslimali na maliasili zetu. Ndiyo maana wamegawa kila kitu kwa wageni bila hofu kwasababu katiba hii mbovu imewapa kinga ya kutoshitakiwa.

“Ukisoma taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG), mabilioni ya fedha za wananchi yanatafunwa tu. Utafikiri tumepeleka mapanya bungeni na serikalini.

“Kwa katiba hii, unaweza kusema rais wa Tanzania ana mamlaka na madaraka makubwa kuliko Mungu. Yeye ndiye anayeteua karibu kila mtu serikalini. Anateua mawaziri, makatibu wakuu, majaji wote, wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashaur, wakuu wa idara za serikali, mashirika ya umma, anateua makamishina wa Tume ya uchaguzi wakati na yeye ni mshindani katika uchaguzi. Hatuwezi kuendelea kuwa na katiba inayolimbikiza mamlaka na madaraka yote kwa mtu mmoja. Katiba mpya ni lazima,” alifafanua Mbowe.

Alisema anajua kuwa CCM inaogopa katiba mpya kwasababu kukiwa na katiba itakayoweka misingi ya uchaguzi huru na haki, chama hicho hakiwezi kushinda.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa Chadema haipo tayari kamwe kuona nchi ikiendelea kuchezewa.

Akihitimisha hoja hiyo, Mbowe aliwapigisha wananchi kura ya maoni akiwauliza kama wapo tayari wapewe kwanza elimu ya katiba ya sasa kwa miaka mitatu, lakini hakuna hata mwananchi mmoja aliyenyoosha kidole kukubaliana na suala hilo.

Wananchi wote walionekana dhahiri kuhitaji katiba mpya hivi sasa.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na kuhutubiwa na viongozi wengine wa Chama hicho, akiwemo Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mwenyekiti wa Chama hicho, Kanda ya Ziwa Victoria, Gimbi Massaba na wajumbe wa Kamati Kuu, Grace Kihwelu na Patric Ole Sosopi.

Kwa upande wake, Kigaila alizungumzia uchumi wa zao la Pamba, akibainisha kuwa wakulima wa pamba wanapata pesa kidogo wanapouza pamba yao, kwasababu ya kuwepo kwa makato mengi, yakiwemo makato ya pembejeo za kilimo, malipo ya ada kwa vyama vya msingi (AMCOS), na tozo na ushuru ambavyo kwa pamoja hufikia makato ya zaidi ya Shilingi 1,000 kwa kila kilo moja ya pamba.

Kigaila alisema makato yote hayo ndiyo yanayomuumiza mkulima kwa kufanya apate shilingi 1,060 tu hivi sasa kwa kila kilo moja ya pamba, wakati angeweza kuuza kwa zaidi ya shilingi 2,600.

Akifafanua zaidi alisema makato hayo si halali, bali ni mbinu tu ya serikali kujipatia fedha kwa kumnyonya mkulima.

Kigaila alifafanua zaidi akisema:

“Kwa mfano, wanawakata Shilingi 300 kwenye kila kilo moja ya pamba, wanadai ni makato ya kuwaletea mbolea na pembejeo za kilimo. Wanapowakata Shilingi 300 kwa kilo, maana yake, kwa tani 3 za Pamba, kila mkulima anakuwa amekatwa shilingi 600,000. Na kwa tani 10 za Pamba, kila mkulima atakuwa amekatwa Shilingi Milioni Tatu.Je, kuna pembejeo mkulima anapewa zinazofikia gharama ya Shilingi Milioni Tatu? Hakuna eeh?

“Serikali ya CCM inawaibia fedha zenu za Pamba. Huu ni wizi..Wanawaibia kwenye Pamba na wanawaibia kwenye mradi wao wa kumvalisha kila ng’ombe hereni kama wasichana. Ni wezi. Achaneni kabisa na CCM. Tunawaomba mjisajili kwa wingi kuwa wanachama wa Chadema ili muweze kujikomboa kwa kuiondoa CCM madarakani na kukomesha wizi huu,” alisema Kigaila.

Mikutano ya Chadema ya Oparesheni +255 inaendelea tena kesho katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Simiyu.

Like