Mbowe amvaa Majaliwa, NIDA

– Ni kuhusu ubaguzi wanaofanyiwa wananchi Kagera.
– Agusia rushwa katika mkataba wa bandari
– Wenje, Pambalu ‘wazaa na CCM’ Wilayani Kyerwa

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amechukua hatua ya kuzungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ili akomeshe kilichoitwa ubaguzi wanaofanyiwa wananchi wengi wa mkoa wa Kagera na mikoa mingine ya mpakani, wa kunyimwa haki yao ya kupatiwa vitambulisho vya Taifa.

Vitambulisho hivyo huandaliwa na kutolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)

Mbowe ameyasema hayo wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Mabira, Murongo na Nkwenda, wilayani Kyerwa, katika mfululizo wa mikutano ya Operesheni ya Chama hicho yenye ujumbe wa Katiba Mpya: Okoa Bandari Zetu, inayoendelea mkoa wa Kagera.

*”Kila tulipopita mkoa huu wa Kagera, nimekuta manunguniko ya wananchi kutopewa vitambulisho vya NIDA. Na suala hili nilikutana nalo pia Kigoma. Wananchi wa mipakani mnabaguliwa kwa kutiliwa shaka uraia wenu.

Baada ya mkutano huu nitampigia simu Waziri Mkuu nitamuuliza kwanini wananchi wa mikoa ya mipakani wananyimwa haki yao ya kupewa vitambulisho.Chadema tunataka ashughulikie suala hili”*, alisema Mbowe.

Malalamiko ya wananchi kutopewa vitambulisho vya NIDA yametamalaki karibu mkoa wote wa Kagera, ikiwemo Bukoba Mjini, Misenyi, Karagwe, Kyerwa, ambapo wananchi wamedai kunyimwa.

Baadhi ya wananchi wamedai kunyimwa vitambulisho hivyo, wakidaiwa siyo raia.

Akizungumzia suala la mkataba tata wa uwekezaji wa bandari baina ya Tanzania na Dubai, Mbowe alisema serikali ya CCM imegawa bandari zote kwa mwekezaji kwa kuingia mkataba usio na ukomo wala faida iliyo wazi kwa nchi, na kwamba isingewezekana mkataba huo kuingiwa bila kuwepo nguvu ya rushwa.

*”CCM wameishiwa fikra. Wamekabidhi bandari 58 na wamekiri wameshindwa kuziendesha. Kwa jinsi mkataba ule ulivyo, ni ngumu kwa mtu mwenye akili timamu kusaini bila kuwepo rushwa ndani yake.

Chadema hatupingi uwekezaji wala Waarabu bali tunapinga mkataba unaomilikisha urithi wa watoto wetu bila ukomo na bila faida zilizo wazi*, alisema Mbowe.

Akizungumzia matatizo ya wananchi wa Kyerwa, Mbowe aliwahakikishia kuwa serikali itakayoundwa na Chadema itawakwamua kutoka katika umaskini kwa kujenga mtandao bora wa barabara za vijijini na kuwaondolea vikwazo vyote vya kuuza mazao yao hususani kahawa, popote pale wanapotaka ikiwemo nje ya nchi.

“Umaskini wa kipato uliopo Kyerwa ni janga la nchi nzima. Ni msiba wa nchi nzima.Tunapaswa kuumaliza msiba huu kwa kuizika CCM,” alisema Mbowe na kushangiliwa na wananchi wa Nkwenda.

Wilaya ya Kyerwa ni mzalishaji wa mazao mengi ya chakula na biashara, ikiwemo kahawa, ndizi, mahindi, maharage, maharage ya soya, mihogo, magimbi, viazi na karanga, lakini changamoto ya barabara mbovu na wakulima kuzuiwa kuuza mazao yao nchi jirani kumeelezwa kuwa sababu kubwa ya umaskini wa wilaya hiyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar wa chama hicho, Salum Mwalimu, Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Ezekiel Wenje na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA), John Pambalu, waliishambulia serikali ya CCM kwa kushindwa kuiletea maendeleo Kyerwa kwa zaidi ya miaka 62 ya uhuru.

“Dubai waliogawiwa bandari na CCM, ni nchi ndogo yenye watu milioni tatu tu, lakini kwa kuwa ina viongozi wenye fikra nzuri, leo tumeishia kuwapa bandari zetu zote 58 watuendeshee,” alisema Wenje.

“Dubai, nchi isiyo na mito wala maziwa, wameweza kubadilisha maji ya bahari kuwa maji yanayofaa kunywa, lakini CCM wameshindwa kuwaletea maji safi ya kunywa licha ya kuwa tuna ziwa Victoria. Na hapa, kwasababu ya sera mbovu za CCM za kuongeza kodi bila kujali wananchi, mfuko wa simenti (saruji) ni Shilingi 23,000 wakati Kenya simenti ni 12,000 ya Tanzania.

“Mnapowaona wamevaa suti, wanaitwa waziri fulani, rais fulani au mbunge fulani wa CCM, msifikiri wana akili kutuzidi. Sisi tuna akili kuliko wao. Tupeni hii nchi Chadema, iwe kama Dubai,” alisema Wenje na kushangiliwa na wananchi wa Mabira.

Kwa upande wake, Mwalimu Pambalu, Mwenyekiti wa BAVICHA, akitumia msemo wa Kihaya, wenye maana ya “Mbwa akikaribia kufa hupoteza uwezo wa kunusa,” alisema CCM ni mithili ya Mbwa anayekufa, kwani imepoteza uwezo wa kunusa matatizo ya wazi ya wananchi ikiwemo tatizo la maji ambalo halipaswi kabisa kuwepo ndani ya mkoa wenye ziwa Viktoria.

“Wahaya mna msemo, “Oruita embwa lubanza enyindo , kwamba Mbwa huanza kufa kwa kupoteza uwezo wa kunusa.CCM ni sawa na Mbwa anayekufa, CCM imepoteza uwezo wa kunusa, CCM haioni shida yenu ya maji na wala hailioni ziwa Victoria. Itoeni CCM madarakani, tayari imekufa,” alisema Pambalu na kushangiliwa na wananchi wa Nkwenda.

Mikutano ya Chadema ya Operesheni +255 yenye ujumbe wa “Katiba Mpya:Okoa Bandari Zetu,” inaendelea tena kesho.

Tangu kuanza kwake, Operesheni hiyo, imevutia maelfu ya wananchi kusikiliza na kujisajili kwa wingi kuwa wanachama wa Chadema.

Like