CRISTIANO Ronaldo, mmoja wa mabingwa wa mataji makubwa ya soka duniani, hivi sasa anatamba kwamba yu miongoni mwa wanadamu wenye furaha zaidi.
Furaha ya Ronaldo haitokani na mafanikio yake makubwa katika kusakata kabumbu na kuwa tajiri mkubwa kutokana na malipo manono anayopata kwa uchezaji wake au matangazo ya biashara, bali kufanikiwa kumshawishi kaka yake aache uraibu wa pombe na mihadarati.
Ronaldo ana mataji makubwa yenye heshima zaidi duniani; matano ya ligi ya mabingwa Ulaya, tuzo tano za mchezaji bora wa dunia wa Ballon d’Or, ubingwa wa Euro 2016 na mataji mengine mengi. Ni baba wa watoto wanne.
Kaka yake, Hugo Aveiro, anayetajwa kuwa “bingwa wa soka la vijana Ureno,” aliacha soka na kuwa bingwa wa ulevi wa pombe na mihadarati.
Hugo, ambaye ana miaka 10 zaidi ya Cristiano Ronaldo, alikuwa nyota wa soka mtaani kiasi kwamba jirani wa familia hiyo, Joel Santos, aliwahi kuliambia gazeti la The Sun la Uingereza kuwa alikuwa mahiri uwanjani akimiliki mpira zaidi ya mdogo wake, Cristiano Ronaldo.
Miaka ya mwisho ya 1990, Hugo aliendekeza matumizi ya pombe na mihadarati kupita kiasi. Kutokana na uraibu wa pombe, alijikuta akitelekeza kipaji na ndoto aliyokuwa nayo ya kuwa mchezaji mkubwa dunia.
Baba mzazi wa vijana hawa wawili, Jose Dinis Aveiro, alikuwa mlevi kupindukia, na kipindi mwanaye Hugo anazaliwa yeye alikuwa Angola akifanya kazi huko. Alifariki mwaka 2005 kutokana na ugonjwa wa ini uliosababishwa na unywaji wa pombe kupita kiasi.
Kutokana na baba yake kutokuwepo nyumbani, Hugo alipitia wakati mgumu katika kukua kwake mpaka akaacha shule akiwa na umri wa miaka 17. Alianza kufanya kazi viwandani na baadaye alifanya kazi za kupaka rangi majumbani. Wakati wote huo aliendelea kutumia pombe na mihadarati.
Katika jitihada za kumsaidia mwanaye, mama yake, Dolores Aveiro, alijitahidi kumshawishi kijana wake aache pombe na matumizi ya dawa za kulevya, lakini alikwama.
Baada ya Cristiano Ronaldo kuanza kuwika katika soka, aliona njia pekee ya kumshawishi kaka yake kuacha pombe ni kuingia naye mkataba ambao atalazimika kuutekeleza. Alikuwa menzi mkubwa wa soka.
Njia hiyo ilikuwa ni mkataba kwamba endapo atasaidia timu yake kushinda kombe la ligi ya mabingwa Ulaya, basi Hugo ataacha pombe na matumizi ya dawa za kulevya.
Mwaka 2014 Cristiano Ronaldo alishinda kombe la mabingwa wa ligi ya Ulaya kwa kuwalaza wapinzani wao wakubwa kutoka jiji moja; klabu ya Atletico Madrid kwa mabao manne kwa moja. Ronaldo ndiye alifunga bao la nne kwa mkwaju wa penati.
Baada ya ushindi huo, Ronaldo alitoka uwanjani na kumkimbilia kaka yake Hugo aliyekuwa uwanjani na kumkumbatia kwa bashasha kuu na kumwambia kuwa ilikuwa ni zamu yake kutimiza upande ahadi yao.
Cristiano alimchukua kaka yake na kumpeleka kwenye nyumba ya mafunzo kwa watu wenye uraibu. Hugo aliishi huko kwa miaka mitano na alifanikiwa kuacha kabisa matumizi ya pombe na dawa za kulevya.
Hugo alipomtebelea Ronaldo nyumbani kwake Jijini Madrid, akaona idadi kubwa ya mataji aliyokuwa nayo mdogo wake. Hugo alipata wazo la kujenga nyumba ya makumbusho yatakapowekwa mataji hayo.
Alimshauri mdogo wake kufungua nyumba ya makumusho ili mashabiki wake waweze kutembelea na kuwa karibu zaidi na nyota huyo wa mpira wa miguu duniani. Hugo alinukuliwa akisema, “Ndugu yangu ni shujaa mkubwa nyumbani Madeira, Ureno ana heshima kubwa hapa kutokana na mchango wake uliotukuka kwa Kisiwa hiki”.
Baada ya nyumba hiyo ya makumbusho kukamilika, Hugo akawa meneja mkuu wa jengo hilo la makumbusho binafsi ya mdogo wake, Cristiano Ronaldo iliyojengwa kwenye Mji wa Madeira ambako ndiko walikozaliwa ndugu hao. Hivi sasa pia Hugo anamiliki biashara ya ujenzi.
Kutokana na kisa hiki, ndugu hawa wawili wamekuwa karibu sana na huenda likizo pamoja. Lakini siyo vyema kuangalia mchango wa Ronaldo pekee kwa Hugo, bali Hugo pia ana mchango mkubwa kwenye maisha ya Cristiano.
Tatizo la uraibu wa pombe alilokuwa nalo Hugo lilimhuzunisha sana na kumfanya Cristiano kupambana zaidi hadi kuwa alipo sasa ili asije kuwa kama baba yake.