Askofu Mkatoliki ampinga Magufuli kuhusu uwepo wa Corona Tanzania. Asambaza waraka mzito kwa waamini

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Isaac Amani, ambaye huko nyuma amewahi kuonekana kama ni swahiba na mtetezi wa Rais John Magufuli, ameelemewa na uzito wa ushabiki usiozingatia sayansi, hasa kuhusu taarifa potofu zinazosambazwa na Magufuli kuhusu ugonjwa wa Corona.

Ameandika waraka kwa waamini wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha jana  – Januari 20 – ambao utasomwa makanisani Jumapili Januari 24. Tayari waraka huo upo kwenye mitandao ya kijamii na unawataka waamini kujilinda dhidi ya Corona na kupuuza kauli za “hakuna Corona Tanzania.”

Askofu Amani amekuwa mtetezi wa kauli za Rais Magufuli, lakini sasa, kwa waraka huu, ameona heri kuokoa uhai wa watu – kama Biblia inavyoelekeza – kuliko kukumbatia hatari ya kunena uongo juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Rais Magufuli amekuwa na msimamo kwamba Tanzana haina Corona kwa kuwa “Mungu ameiepusha nchi” baada ya maombi ya siku tatu aliyoitisha ili kumaliza ugonjwa huo.

Katika waraka huo, Askofu Amani anaandika: “Kutokana na hali halisi ya kuwepo na Corona katika jamii, sisi kama Taifa, inatupasa kujenga utamaduni na tabia mpya za kujinusuru kwa kuacha kutembea “pekupeku juu ya mbigili.”         

Katika waraka huo, askofu huyo anaufananisha ugonjwa wa Corona na mbigili, mimea yenye miiba inayomea mashambani, hasa wakati wa masika.

Askofu Amani alitoa waraka wake tarahe 20 Januari 2021, ukiwa na namba ya kumbukumbu ADA/PAS/1-1/2021/01, anwani ya posta ya sanduku la barua 3044 Arusha na simu nambari +255272544362 (mapokezi), +255272544361(ofisi), na +255272548004 (ofisi).

Katika waraka huo unaoonyesha kuelekezwa kwa mapadre, watawa na waamini walei, Askofu Amani anaelekeza kwamba waraka huo usomwe  katika makanisa yote katika Jimbo Kuu la Arusha keshokutwa – Jumapili, Januari 24, 2021.

“Lengo la waraka huu ni kumwalika kila mtu ajisimamie kwa usalama wake binafsi na kujali usalama wa wengine. Korona inatikisa ulimwengu wote na sisi tusijidanganye kiasi cha kutokuchukua tahadhari. Tusimjaribu Mungu kwa kufanya uzembe na afya zetu.

Askofu alimalizia waraka wake kwa kutoa tahadhari hii ili mwenye kujali ajue waraka umeandikwa kwa ajili ya kuhimiza kuwajibika na kushirikiana katika Yesu Kristo kwa jambo linalohusu uhai kwa kusoma alama za nyakati.

Waraka wa Askofu Amani unawataka waumini wote kuendelea kuzingatia masharti ya wataalam wa tiba juu ya kujikinga na ugonjwa wa Corona. Anayataja masharti hayo kuwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, na kutumia vitakasa mikono, Pamoja na kuvaa barakoa.

“Tulihimizwa kuendelea na matendo ya kuzuia maambukizi hasa kuzingatia usafi mpaka ugonjwa utakapoondoka kabisa. Kwa hiyo safari bado ipo,” anasisitiza Askofu Amani.

Tanzania iligundua kuwepo kwa mgonjwa wa kwanza wa Corona Machi 16, mwaka jana na serikali ilianza kutangaza maambukizi mapya, idadi ya waliowekwa karantini na wale waliopona.

Hata hivyo, baada ya siku 45, serikali ilisitisha kutoa taarifa na takwimu za ugonjwa huo baada ya kupokea maelekezo ya Rais Magufuli. Hadi hatua hii inafikiwa, Tanzania ilikuwa imerekodi wagonjwa 519 na vifo 21 pekee.

Shirika la Afya Duniani (WHO) na taasisi za kimataifa zimeendelea kuitaka Tanzania kuacha kuficha taarifa za ugonjwa huo na hata kukana kuwepo kwa Corona.

Like
2