Kwanini Kinana ameng’atuka ghafla?

KUNA mengi yanasemwa kuhusu hatima ya Komredi Abdulraham Kinana, aliyeng’atuka ukatibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye ndani na nje ya chama hicho ana upekee wa aina yake.

Wiki moja kabla Kinana hajajiuzulu,  kuna wakubwa wengi, wakiwamo wastaafu, waliingia na kutoka Ikulu kuteta na mwenyekiti wa CCM, John Magufuli. Miongoni mwao, Komredi Kinana na msaidizi wake, Humphrey Polepole, hawakuwamo.

Aidha, mwenyekiti wa CCM, aliteua Mizengo Pinda na Makongoro Nyerere kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, haraka haraka kiasi cha wahusika kukosea protokali za kichama na kiserikali pale ambapo Ikulu ilijigeuza kuwa ofisi ya CCM.

Hata kabla ya Kinana kujiuzulu rasmi, baadhi ya vyombo vya habari vilivujisha habari zake kwamba  alikuwa amekabidhi barua ya kujiuzulu. Kuna walioenda mbali na kusema alikuwa ameonekana ofisi ndogo ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, akiondoa na kuhamisha vifaa vyake binafsi.

Hiyo ilikuwa dalili ya kupisha mtu mwingine. Awali ulipotolewa wito wa vikao vya juu vya chama vitakavyofanyika Ikulu mwanzo wa wiki ile, wenye akili walijua kwamba vikao hivyo ndivyo angetumia kujiuzulu. Lakini, ingawa ni kweli hatimaye alitumia vikao hivyo kuaga, ukweli ni kuwa alishajiuzulu.

Kuondoka kwake kabla ya vikao hivyo, ni dalili kwamba mambo si shwari ndani ya chama hicho kikongwe kwa umri na mizengwe yake. Nini kinaweza kuwa kimetokea na kumlazimisha Komredi Kinana aondoke kwa njia hii? Nafikiria matatu.

Tangu Mwenyekiti wa CCM ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania amfukuze kazi Nape Nnauye kutoka nafasi ya uwaziri kwa kile kilichotafsiriwa kama kulinda mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda, uhusiano wa Komredi Kinana na mwenyekiti wake uliingia shakani.

Mafanikio ya Komredi Kinana katika kuongoza sekretariati ya CCM na kampeni za kunadi CCM hadi “ushindi wa goli la mkono”, yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na Nape Nnauye. Njia iliyotumika kumwondoa Nape haikumpendeza Kinana, hata kama hakusema hadharani. Ikumbukwe Komredi Kinana na Nape Nnauye ni wandani wa CCM kuliko nguvu iliyotumika kumwondoa Nape bila baraka za CCM.

Pili, kwa sababu zisizo wazi ndani ya chama na nje ya Chama Cha Mapinduzi, Komredi Kinana amekuwa akirukwa makusudi hata kwa kazi ambazo ni zake. Badala yake, Humphrey Polepole, ambaye ni katibu wa itikadi na uenezi, amekuwa ndiye anazifanya moja kwa moja na mwenyekiti wake.

Mathalani, uteuzi na uhamisho wa makatibu wa wilaya na mikoa, kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na katibu mkuu, imekuwa ikifanywa na Polepole. Kitendo hicho kilisababisha uvumi mbaya wa kuwa Komredi Kinana amewekwa katika kifungo cha ndani ya nyumba yake.

Hata kama anaweza kuwa aliridhia kwa siri kumwachia Polepole afanye kazi hizo, lakini lugha ya mwili wa Komredi Kinana ilisema mengi kuliko mdomo wake.

Tatu, katika shughuli ya kuhakiki mali za chama, ambayo mwenyekiti aliteua tume na kuipa madaraka makubwa, Komredi Kinana hakushirikishwa wala hakufurahishwa nayo. Yeye alikwishaandaa mpango mzuri wa kisayansi zaidi wa kuweza kubaini mali hizo na kuziendesha kwa manufaa zaidi.

Mwenyekiti wake hakumsikiliza, akateua watu wageni kabisa wasiojua chama kufuatilia mali hizo. Matokeo yake, hata yeye alihojiwa kama mwizi huku baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakimtuhumu waziwazi kuhusu kuhujumu mali za chama.

Kibaya zaidi, vyanzo vinasema, Komredi Kinana alijisikia vibaya kuhojiwa na watu kama Albert Msando aliyejiunga na CCM hivi karibuni akitokea chama cha ACT-Maendeleo alikokuwa akitokea Chadema. Huyu “mtalii” wa kisiasa kumdhalilisha mtendaji mkuu wa chama, halikuwa jambo jepesi kupokelewa na Komredi Kinana.

Ukiondoa wazee kama Pius Msekwa, Philip Mangula na John Malecela, hakuna mwana CCM mwingine anayeijua CCM kama Komredi Kinana. Kwa historia yake, ameshiriki kumwingiza madarakani Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli.

Anafahamu kashfa nzito nzito na migogoro iliyokaribia kuzamisha chama, ambazo alizikabili akashiriki kukiokoa kwa kutumia nguvu za nje na ndani. Kumshughulikia mtu wa namna hii hata kama hayuko juu ya sheria, inahitajika hekima na busara inayotokana na kumbukumbu za taasisi yenyewe.

Akiwa ni msomi makini wa uchumi na mwanajeshi wa kusomea, Komredi Kinana ni mnyenyekevu aliyekalia hazina kubwa ya ujuzi na historia ya chama na serikali zake zote. Komredi Kinana ni hodari wa diplomasia, mwenye uwezo wa kubakia katika uhusiano na mahasimu wake kisiasa bila kuathiri maslahi ya Chama.

Uwezo huo, umempa fursa ya kuwasiliana na vijana wenzake wa zamani kama Jakaya Kikwete, Edward Lowasa, Isidory Shirima, Christian Mzindakaya, Jenerali Ulimwengu, hayati Victor Kimesera, na hata hayati Samwel Sitta na wengine wengi. Hilo halikumzuia kuwasiliana na wakuu wa nchi wastaafu kama Mzee Ali Hassan Mwinyi, Amani Karume, Benjamin Mkapa na hata Salmin Amour.

Wakati wote akiwasiliana na kuhusiana nao, hakuwaachia shaka yoyote kuwa anawaheshimu na kutii ushauri wao. Uamuzi wake wa kustaafu ujumbe wa kamati kuu lakini ghafla akabadili na kupokea wajibu wa kuwa katibu mkuu wa chama, ulitokana na utii wake kwa wazee hao.

 

Si mara nyingi historia za vyama vya ukombozi kuwageuza makomredi kuwa wasaliti huku wasaka tonge wakiabudiwa na kuitwa wazalendo. Ng’atuka kwa amani Komredi Kinana. Wanaojua historia watakutendea haki.

Like
24
5 Comments
  1. Mutayoba Arbogast 7 years ago
    Reply

    Pole na mihangaiko ya ughaibuni na mola akutie nguvu na moyo wa uvumilivu. Ahsante kwa kazi nzuri ya uchambuzi. Nitafurahi sana kupata makala zako kupitia e mail yangu.
    Ahsante, na tuko pamoja

    3

    0
  2. Paul Msafiri Mrema 7 years ago
    Reply

    NI tafuta hi kupata makali zako kupitia email yangu

    0

    0
  3. languneno 7 years ago
    Reply

    ✅✅✅✅

    0

    0
  4. Boniphace william 7 years ago
    Reply

    Makala nzur,napenda kupata kwenye mail angu

    0

    0
  5. Chidy 7 years ago
    Reply

    Napenda kupata makala zako kupitia e-mail yangu

    0

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.