Maswali Magumu: Kitabu Chako, Kitabu Chetu

UTAMBULISHO

SAFU ya Maswali Magumu iliyowahi kuchapishwa na magazeti ya Mwananchi Jumapili, Tanzania Daima Jumapili na MwanaHALISI kati ya mwaka 2002 na 2017 imezaa kitabu. Kimeandikwa kwa Kiswahili, na kinatafsiriwa kwa Kiingereza. Ndani ya siku 100 zijazo, kwenye tovuti hii, tunakuletea mtiririko wa kitabu hicho, sehemu kwa sehemu, kukutafakarisha baadhi ya masuala muhimu na magumu tuliyopitia katika miaka 20 iliyopita. Tunaonyesha uhusiano, tofauti na ufanano wa awamu tatu za utawala wa Tanzania chini ya marais watatu – Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, na John Magufuli. Wanafanana katika mambo yapi? Wanatofautiana katika mambo yapi? Na wanaunganishwa na mambo yapi?

Kitabu hiki, ambacho ni mkusanyo na uchambuzi wa makala zangu kadhaa, kinakusudia kuonyesha uzi mwembamba unaounganisha marais hawa watatu wenye tofauti nyingi katika malezi kisiasa, uzoefu kiuongozi, tabia na mienendo katika jamii, hulka za kiutawala na hata kimwonekano, lakini kimsingi wanarudiarudia mambo yale yale kwa staili na nyakati tofauti – na kila mmoja amedai, kwa wakati wake,kwamba anajenga Tanzania mpya.

Kila mmoja atakayesoma rasimu ya kitabu hiki katika tovuti hii, anaruhusiwa kutumia ukurasa huu kutoa maoni yake. Sehemu ya maoni hayo itatumika kuboresha sehemu mbalimbali za kitabu hiki kabla ya kukichapa rasmi na kukiingiza mtaani.

Kwa ushiriki huo, umma wa wasomaji utakuwa umestahili kumiliki kitabu, na kila mmoja atakuwa amestahili kukiita “kitabu changu.” Ni kweli. Hiki ni kitabu chetu. Tukiandike na kukisoma pamoja. Anza sasa kwa kubonyeza hapa chini.

Tunataka majibu sahihi.

Ansbert Ngurumo

Like
18