SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Mwanza, Dk. Anthony Diallo, kudokeza kuwa chama chao kimewahi kuteua mgombea urais mwenye historia ya ugonjwa wa kichaa, umoja wa vijana wa chama hicho umemkaripia kwamba kauli yake ni ya kifedhuli.
Katika mahojiano na Star TV kwenye kipindi cha AJENDA, jana Ijumaa Julai 9, 2021, Diallo, ambaye pia amewahi kuwa waziri katika awamu zilizopita, alisema:
“Mtu ana-matter; ni mtu. Kwa nchi hizi za Kiafrika asikudanganye mtu. Katiba inaweza kuwekwa hapo pembeni akaendelea na mambo zake (yake)… Nadhani tuwe waangalifu tu…katika kuchagua. Hii.. hii.. muwe na track record, mm; huko nyuma tulishachagua watu walishakwenda hospitali, kwenye, kwenye hospitali za vichaa…sasa mtu ana track record ya Mirembe halafu mnawachia achukue nchi? Unajuaje kesho ita, anaweza kunanii?”
Kutokana na kauli hiyo ya Diallo, Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi, akizungumza kutoka mkoani Songwe katika majumuisho ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, amewataka viongozi wa CCM kuwa na nidhamu wakati wote.
Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, yupo ziarani akizungukia mikoa kujitambulisha kwa wanachama tangu alipoteuliwa na chama chake kushika wadhifa huo mwezi Mei mwaka huu.
Kihongosi alihoji kwanini Diallo hakusema wakati ule na kwanini hakuondoka CCM alipogundua kuwa wana mgombea mwenye kichaa.
Akasisitiza: “Viongozi wawe na nidhamu, CCM ni kubwa kuliko mtu.”
Kwa zaidi ya saa 20 mfululizo hadi tunaenda mitamboni, kauli hiyo ya Diallo ndiyo imetawala mijadala ya kisiasa nchini Tanzania katika mitandao ya kijamii na vijiwe vya kahawa.
Inatarajiwa kuwa mjadala kuhusu kauli yake utazidi kupamba moto kwa siku kadhaa zijazo.
Tayari kuna tetesi kuwa wakubwa ndani ya chama wameudhika kwa kauli ya Diallo, na kwamba upo uwezekano akaitwa kujieleza kwenye vikao vya juu vya chama hicho.
Taarifa zilizoifikia SAUTI KUBWA zinasema kuwa hata kauli ya Kihongosi si yake bali ametangulizwa tu. Hata hivyo, wapo wanaCCM waandamizi ambao wanasema wamefurahishwa na Diallo kulisema hili maana wamekaa nalo moyoni kwa miaka mitano, na hawakuwa na pa kulisemea.
Mmoja wao, kwa sharti la kutotajwa jina, ameiambia SAUTI KUBWA: “Kimsingi, tulikuwa tumetumbukia shimoni, chama na nchi vyote vilikuwa vinaeleka kuzama, licha ya propaganda za vyombo vya habari kuonyesha tuko sawa.”