Utekaji wapinzani waendelea Zanzibar

Mipango ya kuvuruga uchaguzi Zanzibar sasa imeingia katika hatua mpya, ilitoanza kuzoeleka Tanzania Bara. Ni utekaji wa wagombea au wasaidizi wao au viongozi wa chama.

Baada ya juzi kumteka Naibu Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo, Nassor Mazrui, baadaye akaokotwa porini siku hiyo hiyo, leo asubuhi watu wanaoaminika kuwa kutoka Idara ya Usalama wa Taifa, wamemvamia na kumteka mpanga mikakati ya ushindi wa chama cha ACT -Wazalendo, Hamad Masoud Hamad.

Inaelezwa kuwa Hamad, ambaye ni mtaalamu wa mawasiliano na takwimu, alitekwa leo alfajiri na watu wanaodaiwa kuwa maofisa wa Idara ya Usalama, wakati akiwa uwanja wa ndege wa Wete.

Inaelezwa kuwa akiwa uwanja huo wa ndege alivamiwa na watu asiowafahamu wakamwamuru aondoke nao.

Nje kidogo ya uwanja walimuingiza kwenye gari na kutokomea kusikojulikana. Gari lililombeba ni aina ya Landrover. Namba za usajili za gari hilo hazikufahamika mara moja.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema kuwa Hamad alipiga kelele, lakini alizibwa mdomo na mmoja wa watekaji hao.

Inaelezwa kuwa Hamad ndiye aliyepangwa kuwa “kiongozi mkusanya taarifa zote za kura” siku ya uchaguzi.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Pemba, Omar Ali Shehe amesema kuwa baada ya wao kufuatilia jambo hili, hatimaye waliambiwa kuwa yupo katika kituo cha Polisi.

Amesema hana taarifa za sababu za kukamatwa kwake, ingawa tangu jana kulikuwa na tetesi za kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho cha upinzani.

Polisi wamegoma kueleza kilichotokea hadi sasa.

Like