KILE kilichotarajiwa kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa kimegeuka uchafuzi tena kama ilivyokuwa 2019. Wapinzani walishiriki wakiwa wanajua matokeo. Ila walitaka kuthibitisha na kusisitiza jambo kwa vitendo. Rekodi imewekwa. Sasa itumike ipasavyo.
Bahati mbaya, watawala wanadhani wameshinda. Wanajipongeza. Bahati mbaya zaidi, wapo wafuasi na wanachama wa upinzani wanaojilaumu na kulaumiana, wakiteswa na propaganda za watawala. Wengine wanasubiri amri kutoka kwa viongozi wao wa ngazi ya taifa. Wengine wanasubiri tamko la “hatushiriki tena hadi iwepo tume huru ya uchaguzi.” Wengine wanasubiri amri za viongozi wao ngazi ya taifa ili “wachukue hatua” dhidi ya wachafuzi wa uchaguzi. Wengine wanataka chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kushawishi vyama vingine navyo visusie uchaguzi mkuu ujao. Ni maoni mazuri ya kizalendo.
Lakini kwa wote hao, nina ushauri ufuatao:
1. Kuchukua hatua ni wajibu wa wananchi si wa viongozi wa vyama.
2. Chama chochote hakina uwezo wa kushawishi vyama vingine – hivyo vya CCM – kugomea uchaguzi.
3. Chama hakina uwezo wa kuzuia uchaguzi. Kama kingekuwa na uwezo huo, kingeutumia kushinda.
4. Watawala hawatakubali kutoa tume huru ya uchaguzi eti kwa vile wapinzani hawataki kugombea. Sahau!
5. Kususia uchaguzi hakujawahi kusaidia msusaji kupata haki yake. Walau sina taarifa yoyote ya mahali popote.
6. Wananchi bado wamelala, ila wanatafuta kujificha nyuma ya viongozi wa chama taifa, na kutafuta mtu wa kulaumu. Siku wananchi wakitoka usingizini, yote haya yatakoma. Siku wakiamua, viongozi watakwenda kutuliza ghasia. Ghasia haipangwi, na wananchi hawaamrishwi kama gwaride. Ukiona viongozi wanaamrisha wananchi, ujue wamehemka na tayari wameshakwama. Hakuna kitakachotokea.
7. Kufokafoka na matamko makali ya viongozi havitasaidia kutisha watawala. Wameshayazoea, na wanajua ni maneno makali tu. Hawajali. Na hata wanapofanya uchafu wao, tunanywea na kulalama. Wanajua. Na watafanya tena.
8. Kinachohitajika ni mkakati, mkakati, mkakati. Mkakati mbadala, si uchaguzi tu. Unahitajika mkakati wa kimya ambao ukiiva na ukiibuka tu, kazi imekwisha.
9. Tusikate tamaa, na tusisubiri wengine watufanyie kazi. Si nyepesi, na hakuna mwingine wa kuifanya bali kila mmoja wetu, pale alipo.
10. Hakuna wakati wananchi tunahitaji umakini na umoja kama sasa – umoja wa nia; umoja wa sauti. Tutafakari. Ili kutafakari vema, tutulize vichwa kwanza. Asiyetaka umoja na mshikamano katika hali hii ndiye mchawi wetu. Umoja kwanza. Mikakati baadaye. Ushindi utapatikana.