NAMFAHAMU Prof Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu Mstaafu aliyeaga dunia majuzi. Nilikuwa karibu naye kwa miaka kadhaa. Alinisikiliza na nilimsikiliza. Sasa ametutoka.
Katika mengi, yeye ni mhanga wa serikali ya awamu ya nne na ya tano. Katika kumwombolezea, nimechagua “mrengo” huu ili nimliie vizuri, vile vile niwasaidie wasomi wengi waliojazwa serikalini hivi sasa.
Wasipokuwa makini, wataondoka serikalini wakijutia uamuzi wao.
Nimewasikia baadhi ya rafiki zangu waliomtaja Prof. Ndulu katika ushiriki wake kwenye wizi wa fedha za “escrow.” Mimi najitolea kumtetea bila kumtakasa.
Tukubaliane kuwa wasomi wetu sasa wanaongozwa na kushauriwa na wanasiasa, hasa watawala, katika kazi zao. Wanaitwa, hawaendi wenyewe kwa wakubwa.
Wakifika wanaambiwa cha kufanya. Waliapa kutii na kutunza siri. Ni kitanzi chao cha kudumu – viapo, utii na kutunza siri. Kwa hiyo, hata kwa Prof Ndulu, ukiondoa muda aliofanya kazi nje ya nchi, haya ndiyo yamekuwa maisha yake.
Wakati akiwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), kuna siku Rais John Magufuli alienda ghafla BoT. Jana yake, Prof. Ndulu alikuwa ameomba ruhusa kwenda Ifakara kumwona mama yake mgonjwa. Rais alimruhusu huku akijua kesho yake anaenda kwa kushtuikiza pale BoT.
Prof Ndulu akiwa njiani alipigiwa simu na wenzake kuwa wameona watu wengi wa usalama wamejaa benki na kuna uvumi kuwa “jamaa” anakuja ghafla.
Alisimamisha gari na kumpigia simu rais. Rais akakiri kuwa ni kweli anaenda BoT. Alimkumbusha kuwa alimpa ruhusa ya kwenda Ifakara kumwona mama mgonjwa. Rais akamjibu kama Ifakara ndipo BoT, basi aende. Prof Ndulu aligeuza na kurudi Dar es Salaam. Alifika BoT, na baada muda mfupi Rais Magufuli aliingia.
Katika ziara hiyo Rais alimdhalilisha gavana mbele ya watumishi wa BoT na vyombo vya habari.
Baadaye kuna rafiki yangu alimtembelea gavana na kumkuta amesononeka. Juzi Prof Ndulu alipofariki dunia, rafiki yangu huyu alinisimulia alichomweleza: “Nilimshauri ajiuzulu kuliko kusubiri kudhalilishwa zaidi. Alitetemeka wakati wote. Hakupata ujasiri wa kujiuzulu. Alibaki kwenye kusitasita mpaka alipoondolewa bila shukrani na kukejeliwa hadharani.”
Itakumbukwa kuwa ni gavana huyu huyu aliyehusishwa na uidhinishaji wa fedha za Tegeta Escrow. Tofauti ya hii na ile ya kudhalilishwa na awamu ya tano ni kwamba katika awamu ya nne walikubaliana na kuridhika kuwa fedha zile hazikuwa za serikali.
Hilo alisimamia mpaka mauti yake. Waliohusika na sakata hilo, akiwamo rais wa awamu ya nne, wanaamini hadi leo kuwa fedha ile si za serikali.
Wasomi na wataalam wengi hapa nchini wanafanyishwa, au wanajiruhusu kufanyishwa, kazi za kishetani kwa kuogopa kusema kweli na kusimamia taaluma zao.
Ni utimilifu wa msimamo wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa “mtu mwenye akili akikushauri jambo la kipumbavu nawe ukijua ni la kipumbavu ukalikubali anakudharau.”
Wasomi wametelekeza taaluma, sasa wanaimba nyimbo za kisiasa. Usishangae kesho rais akamteua mtu kama Kasheku Mshukuma kuwa waziri, akamwagiza Prof. Luoga wa BoT kufanya mambo kinyume cha taaluma yake, naye atakubali.
Ndiyo maana Corona inatumaliza tukiwa kwenye ubishi wa ama tuvae au tusivae barakoa. Ndiyo maana waziri wa afya anajifunika ushungi na kujifukiza utadhani ni mganga wa kienyeji.
Ndiyo maana madaktari wamemtoa mgonjwa hospitalini – Dk Philip Mpango – ili azungumze na waandishi wa habari, wakamleta bila barakoa, anaongea huku akiwakoholea hata wenyewe waliomleta, ambao nao hawajavaa barakoa.
Wanajua kuwa wanamtesa, lakini hawajali. Wanafahamu wanaweza kuambukizwa kwa uzembe huu lakini hawajali. Wanajua hata waandishi wa habari wanaweza kuambukizwa lakini hawajali.
Ni hivi: Wasomi wetu hawana uhuru. Hawatumii tena taaluma yao. Wanafuata amri.
PUMZIKA KWA AMANI PROF. NDULU, MHANGA WA WATAWALA WABABE!