TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazoathirika kwa uamuzi wa kugomea sera ya uraia pacha.
Wanasiasa wa chama tawala wamekuwa mstari wa mbele kupinga mabadiliko yoyote kisera ambayo yangenufaisha Watanzania wengi walio nje ya nchi ambao kwa sababu za kisiasa, kiuchumi au kitaaluma, wamejikuta wanahitaji uraia wa nchi nyingine – jambo ambalo lina faida kwao binafsi na nchi zao, kama yalivyo mataifa mengi duniani yenye sera hiyo.
Wachezaji wa soka ni miongoni mwa makundi yaliyoathirika mno. Kwa jinsi sera ilivyo leo, raia yeyote wa Tanzania akiamua kuchukua uraia wa nchi nyingine, kwa sababu yoyote, lazima akane uraia wa Tanzania.
Kwa sababu hiyo, baadhi ya wachezaji wa soka wameamua kuchukua uraia wa nchi nyingine ili wapate kutumia fursa zilizowafikia.
Mfano wa hivi karibuni ni Meshack Seleman, aliyewahi kuchezea Mbeya City na Tanzania Prisons miaka mitano iliyopita, na sasa anakipiga Malawi Premier League katika Klabu ya Nyasa Big Bullets nchini Malawi.
Meshack ni mzaliwa wa Tanzania. Baba yake ni Mtanzania wa Mbeya. Mama yake ni mzawa wa Karonga, Malawi.
Amejikuta akiamua kucheza timu ya Taifa ya Malawi – The Flames – kama suluhisho binafsi kwani kutokana na kanuni za FIFA, mchezaji anaweza kuchezea timu ya taifa la mzazi wake mojawapo, akitarajiwa kuwa na uraia huko.
Mchezaji mwingine mwenye uraia wa Tanzania ambaye hakutaka kuchezea timu ya taifa hilo, Taifa Stars, ni Abdallah Salim anayekipiga katika timu ya Sports Club Villa (SC Villa) inayoshiriki Premier League nchini Uganda.
Ni miongoni mwa wachezaji wanaokubalika kwa mashabiki wa timu hiyo huku wakimpa jina la utani “Mwarabu,” kutokana na asili yake, na tayari ameshachezea timu ya Taifa ya Uganda chini ya miaka 23 dhidi ya Saudi Arabia.
Iwapo Tanzania haitabadili sera na sheria zake kuhusu suala jili, kuna uwezekano wakapoteza vipaji vingi vya michezo ambavyo vitachukua uraia wa nchi yoyote itayowahakikishia fursa ya kucheza soka la kulipwa.