JOHN Swinton (pichani), aliyekuwa kiongozi mkuu wa chumba cha habari cha gazeti lenye nguvu na heshima kubwa duniani, The New York Times (1860 to 1870), alipoombwa kutoa salamu kwa “vyombo huru vya habari” katika Klabu ya Waandishi wa Habari ya New York, alisema haya:
“Hakuna kitu kama hicho, katika kipindi hiki cha historia ya dunia, hapa Marekani, kama vyombo huru vya habari. Mnajua hivyo na mimi ninajua hivyo. Hakuna hata mmoja wenu anayeweza kuandika maoni yake ya kweli; na kama mngeandika, mngekuwa mnafahamu mapema kwamba kamwe yasingechapishwa. Ninalipwa kila wiki kwa kuzuia maoni yangu ya kweli kutokeza kwenye gazeti nililonalo.
Wengi wenu mnapata mishahara kama hiyo kwa mambo kama hayo; na kama atakuwepo mjinga yeyote miongoni mwenu, anayeweza kuandika maoni ya kweli, hakika atakuwa nje mitaani akitafuta kazi nyingine. Ikiwa ningeruhusu maoni yangu ya kweli yaonekane katika toleo moja la gazeti langu, ndani ya saa ishirini na nne kazi yangu ingepotea.
Kazi ya mwandishi wa habari ni kuharibu ukweli; kusema uongo waziwazi; kupotosha; kukashifu; kuabudu utajiri mchafu wa kishetani na kuuza nchi yake na jamii yake kwa mkate wake wa kila siku. Mnajua hivyo na mimi ninajua hivyo; sasa ni upumbavu gani huu wa kutaka nitolee vifijo vyombo huru vya habari?
Sisi ni zana na vikaragosi vya watu matajiri nyuma ya pazia. Sisi ni wanasesere – wao wanavuta nyuzi na sisi tunacheza. Talanta zetu, matarajio yetu, na maisha yetu yote, ni mali ya wanaume wengine. Sisi ni makahaba kiakili.
****************************************************(
Andiko hili ni sehemu ya mchango wa Ndimara Tegambwage katika mjadala kwenye kundi sogozi la Maswali Magumu.